Waziri
wa Elimu na Mafunzo ya Amali Riziki Pembe Juma amesema wakati umefika
sasa kwa walimu wa skuli kutumia zaidi zana na vielelezo katika
kufundisha wanafunzi badala ya kutumia chaki, mdomo na ubao pekee.
Alisema
iwapo vitendea kazi na vielelezo vitatumika vizuri na kwa muda sahihi
kuna uwezekano mkubwa kiwango cha ufahamu kwa wanafunzi wengi kuongezeka
na kufanya vizuri kwenye mitihani yao ya Taifa na kuinua kiwango cha
elimu.
Waziri
wa Elimu alitoa maelezo hayo Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA)
Kampasi ya Nkrumah kwenye ufunguzi wa Maonyesho ya zana za kufundishia
na kujifunzia katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Katibu Mkuu wa
Wizara hiyo Dk. Idrissa Muslim Hija.
Alisema
matumizi ya zana na vielelezo ni muhimu sana katika kumuandaa
mwanafunzi kukabiliana na mitihani yake na amebainisha kuwa utaratibu
uliozoeleka wa mwalimu kukaa mbele ya darasa na chaki ni potofu kwa sasa
na inachangia kushuka kiwango cha elimu.
Alishauri
kutumika mpango wa Maendeleo ya Elimu ya kutengeneza na kutumia zana
zinazopatikana katika mazingira yaliyotuzunguka ambazo zinagharama
nafuu.
Alisema
vifaa hivyo vilivyotengenezwa na wanafunzi wanaosoma kada ya ualimu
Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar vinatrajiwa kuwa suluhisho kwa baadhi ya
wanafunzi wa skuli wenye ufahamu mdogo katika masomo.
Aliongeza
kuwa Serikali inaendelea kufanya juhudi ya kuongeza vifaa vya
kufundishia na kujifunzia lakini kutokana na idadi ya wanafunzi
kuongezeka kwa kasi, kuna umuhimu kwa walimu waliopatiwa mafunzo ya
kutengeneza vifaa hivyo kuuedeleza katika skuli watakazo pangiwa baada
ya kumaliza chuo.
Mkuu
wa Skuli ya Elimu ya SUZA Dk. Maryam Jaffar Ismail alisema wanafanya
juhudi ya kuwaandaa walimu wanaosoma chuoni hapo kutengeneza zana za
kusomeshea kwa kutumia vitu vilivyopo katika mazingira yaliyowazunguka
ambavyo havina gharama kubwa ili kuwasaidia wanafunzi wao na kuongeza
ufanisi katika kazi hiyo.
Alisema
tokea walipoanza mpango huo miaka mitano iliyopita ufanisi wa
kutengeneza vifaa umekuwa ukiongezeka na wamekuwa kigenzo kwa vyuo vikuu
vya nchi jirani kutaka kuja kujifunza .
Akielelezea
changamoto inayoikabili kada ya elimu nchini ni vijana wengi kukataa
kujiunga na kada hiyo na wanaojiunga ni vijana wanaokosa masomo katika
fani nyengine jambo ambalo alisema sio sahihi.
Akitoa
neno la shukrani katika maonyesho hayo, Mkufunzi wa Mradi wa
kutengeneza zana za kufundishia na kujifunzaia wa SUZA Maalim Said Yunus
alisema vifaa vyote wanavyotumia kutengeneza zana za kufundishia na
kujifunzia vinaweza kupatikana sehemu yeyote ya Zanzibar bila kutumia
gharama kubwa.
Alisema
hatua ya kutengeneza zana hizo itaziba pengo la upungufu wa vifaa vya
kufundishia na kujifunzia unaozikabili skuli nyingi za Zanzibar ambavyo
vimekuwa vikiagizwa na Serikali kwa gharama kubwa.
Katibu
Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Dk. Idrissa Muslim Hija
akipata maelezo ya chombo kinachotumika kupitisha umeme kutoka kwa
mwanafunzi Husna Sharif wa Sekondari ya SUZA katika maonyesho ya zana za
kufundishia na kujifunzia yaliyofanyika Kampasi ya Nkrumah.
Mkufunzi wa somo la kutengeneza zana za kufundishia na kujifunzia wa
SUZA Maalim Said Yussuf akieleza Mradi huo unavyoendelea kuwaandaa
walimu wanafunzi wanaosomo chuoni hapo katika maonyesho yaliyofanyika
Kampasi ya Nkrumah.
Baadhi ya walimu wanafunzi wanaosoma SUZA wakifuatilia ufunguzi wa
maonyesho ya zana za kufundishia na kujifunzia yaliyofanyika Kampasi ya
Nkrumahi
Mkuu
wa Skuli ya Elimu ya SUZA Dk. Maryam Jaffar Ismail akizungumza katika
ufunguzi wa maonyesho ya zana za kufundishia na kujifunzia yaliyofanyika
Kampasi ya Nkrumah.
Katibu
Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali (katikati waliokaa) akiwa
katika picha ya pamoja na Wawakilishi wa Taasisi mbali mbali za Zanzibar
na Tanzania Bara walioalikwa ufunguzi wa maonyesho ya zana za
kufundishia na kujifunzia yaliyofanyika Kampasi ya Nkrumah. Picha na
Ramadhani Ali
No comments:
Post a Comment