Na Josephine Majura, WFM, Dodoma
Serikali
imeeleza kuwa mikakati inayoendelea kutekelezwa na kuratibiwa katika
Mkoa wa Kagera ni pamoja na kutenga maeneo ya uwekezaji yenye ukubwa wa
hekta 58,000 kwa ajili ya kuanzisha viwanda vya kusindika na kuongeza
thamani ya mazao ya kilimo (Agro Processing Industries) hususani viwanda
vya kusindika nyama, maziwa, asali, ndizi, miwa, kahawa na samaki.
Hayo
yameelezwa Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango
Dkt. Ashatu Kijaji, alipokua akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti
Maalaum Mhe. Halima Bulembo, aliyeuliza mkakati wa Serikali wa kuwa na
miradi maalum ya kuondoa umasikini kwa Watu wa Kagera ambao ndio Mkoa
pekee unaopakana na nchi nyingi zaidi za EAC na hivyo kuufanya kuwa Mkoa
wa kimkakati kibiashara.
Alivitaja
baadhi ya viwanda hivyo kuwa ni Kagera Fish Co. Ltd na Supreme Perch
Ltd vinavyosindika minofu ya samaki, Kagera Sugar Co. Ltd na Amir Hamza
Co. Ltd vinavyosindika miwa na kahawa, na Kiwanda cha Mayawa
kinachosindika Mvinyo ya Rosella na juisi.
"
Kampuni ya Josam imepatiwa eneo lenye ukubwa wa hekta 500 katika ranchi
ya Kikulula na tayari imejenga bwawa kwa ajili ya kuvuna maji pamoja na
kuanza ufugaji wa ng'ombe wa maziwa wapatao 100 hadi sasa" aliongeza
Dkt. Kijaji
Dkt.
Kijaji alieleza kuwa mkakati wa kutekeleza miradi maalum ya kuondoa
umasikini katika Mkoa wa Kagera imeainishwa kwenye Mpango wa Maendeleo
wa Miaka Mitano 2016/2017 – 2020/2021, Mpango Mkakati wa Mpango wa
utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo na Mipango ya Mkoa wa Kagera kwa
ujumla.
“
Miradi yote ya kiuchumi na kijamii inayotekelezwa na Serikali na Sekta
Binafsi katika mkoa wa Kagera, na mikoa mingine ni kwa ajili ya kuondoa
umaskini na kuboresha maisha ya wananchi”, alisema Dkt. Kijaji.
Aidha,
aliainisha baadhi ya mikakati inayoendelea kutekelezwa na kuratibiwa na
Serikali katika mkoa huo kuwa ni pamoja na kuimarisha usafiri wa
majini kwa kukamilisha ujenzi wa meli kubwa itakayotoa huduma ya usafiri
na usafirishaji kati ya Bukoba na Mwanza.
Dkt.
Kijaji aliongeza kuwa Serikali imeendelea kuimarisha miundombinu ya
barabara kama vile barabara kwa kiwango cha lami ya Kyaka – Bugene (km
59.1), Kagoma – Lusahunga (Km. 154), Ushirombo – Lusahunga (Km. 50).
Alizitaja
barabara nyngine zinazojengwa katika ukanda huo kuwa ni barabara ya
Nyakanazi - Kibondo (km 50), ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 40
pamoja na barabara ya Kyamyorwa - Buzirayombo (km 120).
“Kitaanzishwa
kiwanda cha kuchakata madini ya bati katika wilaya ya Kyerwa ifikapo
Juni, 2021 ambapo Kampuni ya Tanzaplus Minerals na African Top Minerals
ltd zimeonesha nia ya kuwekeza katika sekta hiyo na tayari zimeanza
kuleta mitambo ya uchenjuaji" aliongeza Dkt. Kijaji
Aliutaja
mradi mwingine wa sekta ya madini kuwa ni uendelezaji na uwekezaji wa
madini ya Nikeli Kabanga katika Wilaya ya Ngara ifikapo Juni mwaka 2021.
Mbunge
wa Ilolo Mhe. Venance Mwamoto, aliuliza mpango wa Serikali wa
kukarabati barabara za mkoa wa Kagera kwakuwa una viwanda vingi ili
viweze kufikika kwa urahisi na kurahisisha biashara ndani na nje ya
nchi.
Akijibu
swali la nyongeza Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe.
Atashasta Nditiye alisema kuwa Serikali imeshapeleka fedha katika mkoa
huo na tayari imetoa tangazo la kutafuta Wakandarasi kwa ajili ya
ukarabati wa barabara hizo.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji (Mb)
No comments:
Post a Comment