RAIS
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein,
akikagua gwaride maalum llililoandaliwa kwa ajili ya Ufunguzi wa Bunge
la Afrika Mashariki katika viwanja vya Baraza la Wawakilishi Chukwani
Zanzibar.(Picha na Ikulu)
RAIS
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein,
akisalimiana na Spika wa Bunge la Afrika Mashariki Martin Ngoga,
alipowasili katika viwa vya Baraza la Wawakilishi Chukwani
Zanzibar.(Picha na IKULU)
RAIS
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein,
akiwa na Spika wa Bunge la Afrika Mashariki Martin Ngoga wakiingia
katrika ukumbi wa Mkutano kwa ajili ya Ufunguzi.(Picha na Ikulu)
RAIS
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein,
akihutubia wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Afrika Mashariki
lililofanyika katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani Zanzibar
leo.(Picha na Ikulu)
Baadhi ya wabunge wa bunge la Afrika Mashariki wakisikiliza hotuba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani Zanzibar leo.(Picha na Ikulu)
RAIS
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein
amesema kuwa suala la kupambana na rushwa lina umuhimu mkubwa katika
maendeleo ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki hasa
ikizingatiwa kwamba vitendo hivyo vinazorotesha uchumi na maendeleo.
Dk.
Shein aliyasema hayo leo huko katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi,
Chukwani mjini Zanzibar wakati akizindua Mkutano wa Nne wa Bunge la
Afrika Mashariki (EALA) ambapo kwa mwaka huu unafanyika hapa Zanzibar.
Katika
maelezo yake Rais Dk. Shein alieleza kuwa kuwepo kwa Mswada wa rushwa
katika mkutano wa Bunge hilo mwaka huu kuna umuhimu mkubwa kwani
utasaidia katika kupambana na vitendo vya rushwa ambavyo vimekuwa
vikiathiri sana uchumi na maendeleo ya nchi na wananchi wake.
Amesema
kuwa Mkutano huo ambao katika Miswada yake ambapo miongoni mwao
kutakuwepo Mswada huo ambao utajadiliwa unakwenda sambamba na juhudi
mbali mbali zinazochukuliwa na nchi wanachama katika kuendeleza
mapambano dhidi ya rushwa na uhujumu wa uchumi.
Alieleza
kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika jitihada zake za
kukomesha vitendo vya rushwa imeunda Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu
Uchumi Zanzibar (ZAECA) kwa lengo la kushughulikia suala zima la
kupambana na rushwa.
Alisema
kuwa juhudi hizo zinaendelea kwa mashirikiano ya pamoja na wananchi
hatua ambayo imepelekea Mamlaka hiyo kuweza kupiga hatua kubwa.
Aliongeza
kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Awamu ya Tano
inayoongozwa na Rais Dk. John Pombe Joseph Magufuli imeongeza juhudi
zaidi katika kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa kwa kuweka mikakati
mbali mbali.
Alisema
kuwa Serikali zote mbili ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimeimarisha usimamizi wa sheria na
kuongeza Bajeti katika sekta ya sheria sambamba na kuongeza wataalamu
ili kusimamia kesi zinazohusiana na rushwa.
Hivyo,
Rais Dk. Shein alisema kuwa juhudi hizo zitasaidia sana pamoja na zile
sheria zitakazotungwa na Bunge hilo ambazo zote kwa pamoja zinaweza
kufikia lengo lililokusudiwa.
Aidha,
Rais Dk. Shein alisisitiza suala zima la kuzingatia umhimu wa maadili
na tabia njema katika kutekeleza majukumu ya viongozi hao hasa katika
wakati huu ambao teknolojia na mifumo ya maisha imebadilika na baadhi ya
wakati hupelekea Wabunge kufanya vitendo ambavyo vinahitaji umakini na
maamuzi ya busara ili waweze kulinda hadhi yao.
Alisema
kwamba inatia moyo kuona kwamba Ukanda wa Afrika Mashariki ni miongoni
mwa Kanda zinazoongoza katika ukuaji mzuri wa uchumi duniani ambapo
katika mwaka wa 2017 uchumi ulikuwa kwa asilimia 4.6 ikilinganishwa na
mwaka 2016 ambapo uchumi ulikuwa asilimia 4.4.
Alieleza
kuwa hayo ni mafanikio makubwa ambayo yanapaswa kuendelezwa huku
akisisitiza kuwa kutokana na Afrika ya Mashariki kuwa na zaidi ya watu
milioni 162 hali hiyo inapelekea kuwepo kwa soko kubwa la bidha mbali
mbali pamoja na huduma muhimu.
Pia,
alieleza kuwa Afrika Mashariki ina ardhi kubwa yenye kilomita za mraba
1.82 milioni ambayo ni vyema rasilimali hiyo ikatumika vizuri ili iweze
kuleta tija kwa nchi wanachama.
Vile
vile, Rais Dk. Shein alipongeza juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na nchi
wanachama katika kuhakikisha kwamba Jumuiya hiyo inafikia malengo yake
hasa katika suala zima la kukuza uchumi, uimarishaji wa utawala Bora,
uismarishaji wa sheria pamoja na uimarishaji wa amani na utulivu.
Rais
Dk. Shein ameeleza kutiwa moyo sana na juhudi za Umoja huo za kuimarisha
lugha ya Kiswahili ambayo hivi sasa imekuwa ni lugha inayounanisha
wanachama katika shughuli mbali mbali za kiuchumi na kijamii.
Alieleza
kuwa Zanzibar inathamini sana fursa iliyopewa ya kuwa Makamo Makuu ya
Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki na kuahidi kuwa fursa hiyo
itaitumia vizuri ili kuhakikisha malengo yaliokusudiwa yanafikiwa.
Dk.
Shein alimuhakikishia Spika wa Bunge hilo Martin Ngonga kuwa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuwa mstari wa mbele katika kuendeleza
na kuitangaza lugha ya Kiswahili na kufahamisha kwamba kupitia Baraza
la Kiswahili la Zanzibar (BAKIZA) imekuwa ikiandaa makongamano mbali
mbali ya Kiwahili ambayo yanajumuisha wataalamu kutoka sehemu mbali
mbali duniani.
Alisema
kuwa hatua hiyo ina lengo la kukiimarisha na kukuza matumizi sahihi ya
Kiswahili fasaha kwa kuangalia kwamba Zanzibar ndio chimbuko la Kswahili
sanifu.
Rais
Dk. Shein alisema anaamini kwamba Jumuiya hiyo inaweza kuwa eneo muhimu
la kiuchumi duniani, hivyo jitihada zaidi zinahitajika katika
utekelezaji wa malengo makuu yaliopangwa na Jumuiya hiyo ikiwa ni pamoja
na kushajiisha uekezaji, kuendeleza sekta ya utalii, viwanda, elimu na
kutilia mkazo suala zima la kuongeza ajira na kuimarisha miundombinu.
Pamoja
na hayo, Rais Dk. Shein aliitaka Jumuiya ya Afrika Masharik kupitia
Bunge lake hilo kuchukua jitihada katika kupambana na vitendo mbali
mbali vyenye kuathiri uchumi ikiwemo suala zima la utakasishaji wa
fedha.
Vile
vile, Rais Dk. Shein alieleza haja ya kuendeleza teknolojia ya Habari na
Mawasiliano huku akiwasisitiza Wabunge wa Bunge hilo kufanya kazi kwa
mashirikiano mazuri na Mabunge mwengine ya nchi wanachama ili kuweza
kufanya kazi kwa ufanisi mzuri zaidi.
Aidha,
Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kulipongeza Bunge hilo kwa kufanya
mkutano wake huo hapa Zanzibar na yeye kupata fursa kwa mara ya pili
kuufungua mkutano huo na kutoa shukurani zake kwa kuweza kukaa pamoja na
chombo hicho muhimu cha kutunga Sheria.
Rais
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kumpongeza Spika wa Bunge hilo kwa
kuchaguliwa kuwa Spika wa tano na kuweza kukiongoza chombo hicho huku
akiwapongeza Wajumbe wote wa Bunge hilo kwa kuchaguliwa kukiongoza
chombo hicho muhimu katika Afrika Mashariki.
Pamoja
na hayo, alisifu utaratibu wa Bunge wa kufanya mikutano katika miji ya
nchi wanachama jambo ambalo linapelekea wananch kufahamu majukumu ya
chombo hicho ambapo alisema utaratibu huo unaenda sambamba na falsafa ya
kuweka umoja na mshikamano kwa watu wa Afrika Mashariki.
Sambamba
na hayo, Rais Dk. Shein ameleza kufurahishwa kwake na moja ya Miswada
ambayo itajadiliwa katika Bunge hilo ambayo ni pamoja na Mswada wa vita
dhidi ya rushwa, masuala ya kijinsia,ulemavu pamoja na mada nyengine
zitakazojadili vitendo vya ugaidi vilivyojitokeza nchini Kenya.
Nao
Wabunge hao walitoa shukurani kwa Rais Dk. Shein kwa heshima kuwa
aaliyowapa ya kwenda kuzindua mkutano wao huo na kueleza kufurahishwa
kwa kiasi kikubwa na hotua aliyoitoa ambayo imewapa matumaini makubwa.
Nae
Spika wa Bunge hilo Martin Ngoga alitoa shukurani kwa Baraza la
Wawakilishi Zanzibar pamoja na uongozi wake chini ya Spika wa Baraza
hilo Zubeir Ali Maulid kwa mashirikiano mazuri wanayoyapata ambayo ni
chachu katika utekelezaji wao wa kazi.
Aidha,
Spika huyo alieleza umuhimu wa lugha ya Kiswahili katika Umoja huo
pamoja na Wajumbe wa Bunge hilo na kueleza mikakati waliyoiweka katika
kuhakikisha lugha hiyo inatumika vyema ndani ya Bunge hilo pamja na nchi
zote za Jumuiya hiyo.
Nae
Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid alieleza mashirikiano
mazuri yaliopo kati ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar na Bunge hilo
Afrika Mashariki na kueleza mafanikio makubwa yaliopatikana katika
mashirikiano hayo.
Katika
uzinduzi huo wa Mkutano wa (EALA) ambao unatarajiwa kuwa wa siku 10
moja, viongozi mbali mbali walihudhuria akiemo Spika wa Bunge hilo
Martin Ngoga, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd,
Wenyeviti na Mawaziri wa Nchi za Jumuiya ya Nchi za Afrika Mashariki,
Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Zubeir Ali Maulid, Spika Mstaafu
Pandu Ameir Kificho, Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu,
Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Wajumbe wa Bunge
hilo la Afrika Mashariki.
No comments:
Post a Comment