Na Peter Haule, WFM, Dar es Salaam
Serikali imezuia Sh. bilioni 5.5 ambazo
zilipaswa kutumika kutekeleza mradi wa kimkakati wa Soko la Magomeni,
lililoko wilaya ya Kinondoni, Jijini Dar es Salaam kutokana na
kucheleweshwa kwa utekelezaji wa mradi huo licha ya kupewa fedha za
kutosha kwa awamu ya kwanza.
Hatua hiyo imechukuliwa na Naibu Waziri
wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji baada ya kutembelea na kukagua
ujenzi wa mradi huo unaotarajia kugharimu shilingi bilioni 9 na kukuta
ujenzi wake unasuasua.
Dkt Kijaji
alisema kuwa Serikali, imeipatia Manispaa ya Kinondoni shilingi bilioni
3.5 tangu mwezi Mei, 2018 kwa ajili ya kutekeleza mradi huo ambao
ungepaswa ukamilike ndani ya miezi tisa tangu kusainiwa kwa mkataba wa
ruzuku hiyo lakini ameshangaa kutomkuta mkandarasi kwenye eneo la
ujenzi.
“Serikali inasitisha kutoa kiasi cha Sh.
bilioni 5.5 mpaka watakapo dhihirisha wako tayari kuwahudumia wananchi
na kutekeleza dhamira njema ya Mhe.Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, ya
kuwahudumia wananchi wake”, alieleza Dkt. Kijaji.
“Jana Manispaa ya Ilala wametuangusha
kwenye usimamizi wa mradi wa Machinjio ya kisasa ya Vingunguti
tumerejesha shilingi bilioni 3 Hazina na leo Manispaa ya Kinondoni nao
wametuangusha na tunalazimika kuzizuia fedha hizo sh. bilioni 5.5 mpaka
tujiridhishe na maendeleo ya ujenzi” alisisitiza Dkt. Kijaji.
Awali, akitoa maelezo ya mradi huo kwa
niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Kinondoni, Mhandisi wa
Manispaa hiyo Justin Lukaza, ameeleza kuwa Manispaa hiyo imeingia
mkataba wa kujenga soko hilo litakalo kuwa na ghorofa tatu na Kampuni ya
Group Six International na kwamba ujenzi ungekamilika katika kipindi
cha miezi sita ijayo na kutofautiana maelezo na mwakilishi wa Mkandarasi
ambaye alimweleza Dkt. Kijaji kuwa ujenzi huo ungechukua muda wa miezi
12.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya
Kinondoni Bw. Daniel Chongolo, amekiri kuwa kuna uzembe umefanywa na
watendaji wa Manispaa ya Kinondoni uliosababisha mradi huo kuchelewa
kuanza na kumwomba Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji
ampe muda mfupi wa kurekebisha kasoro hizo.
Alisema kuwa tayari kuna hatua mbalimbali
zilichukuliwa kwa maafisa waliofanya uzembe katika utekelezaji wa mradi
hapo awali na hakujua kama bado kulikuwa na uzembe uliokuwa unaendelea
baada ya kuchukua hatua hizo kwa sababu aliamini watendaji
waliokabidhiwa kusimamia ujenzi wa mradi huo walijifunza kutokana na
makosa ya wenzao walioondolewa kusimamia mradi huo
“Mimi nakubaliana na wewe (Naibu Waziri
wa Fedha) kwamba kuna uzembe na kazi yetu sisi ni kuhakikisha
tunarekebisha haya makosa na nichukue dhamana na tutawajika na watu hawa
na nitalazimika kutumia dhana ya punda mwenye mzigo na mwenye punda
anaye mchapa bakora ili punda aende” alisisitiza Bw. Chongolo.
Baadhi ya wakazi wa Kinondoni
wameipongeza Serikali kwa ufuatiliaji wa miradi ya wananchi na
kusikiliza kero zao wakitolea mfano wa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango,
Dkt. Ashatu Kijaji, na kwamba hatua hiyo inaleta uwajibikaji wa
watendaji ambao walijenga mazoea ya kuzembea kwa makusudi kusimamia
miradi ya wananchi na kuahidi kuendelea kumuunga mkono Mheshimiwa rais
Dkt. John Pombe Magufuli katika kuliletea Taifa maendeleo.
Mradi wa Soko la Kisasa la Magomeni ni
miongoni mwa miradi 22 iliyopewa ruzuku na Serikali katika Mpango wa
Awamu ya Kwanza wa kuziwezesha Mamlaka za Serikali za Mitaa kujitegemea
kimapato ambapo zaidi ya shilingi bilioni 147 zilitolewa na Wizara ya
Fedha na Mipango kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo.
No comments:
Post a Comment