Na Greyson Mwase, Pwani
Mwenyekiti
wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amewataka wachimbaji wa madini
ya ujenzi aina ya kokoto katika mkoa wa Pwani kuwa na Mpango wa
Ufungaji Mgodi utakaotumika kama mwongozo wa kuhakikisha mazingira
yanaachwa yakiwa katika hali salama mara baada ya kumalizika kwa
shughuli za uchimbaji wa madini hayo.
Profesa
Kikula aliyasema hayo tarehe 21 Februari, 2019 katika nyakati tofauti
alipofanya ziara yake katika migodi inayojishughulisha na shughuli za
uchimbaji wa madini ujenzi aina ya kokoto iliyopo katika Wilaya ya
Bagamoyo mkoani Pwani yenye lengo la kutembelea wachimbaji wa madini
hayo pamoja na kusikiliza na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili.
Profesa
Kikula katika ziara hiyo akiwa ameambatana na Kamishna - Tume ya
Madini, Dkt. Athanas Macheyeki, wataalam kutoka Makao Makuu ya Tume ya
Madini jijini Dodoma, Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dar es
Salaam, Ofisi ya Afisa Migodi Mkazi wa Lugoba pamoja na waandishi wa
habari, Profesa Kikula alitembelea migodi ya Sisti Mganga, Gulf Concrete
Company Limited na Yaate Company Limited iliyopo katika Wilaya ya
Bagamoyo.
Akizungumza
katika nyakati tofauti mara baada ya kutembelea migodi hiyo, Profesa
Kikula aliwataka wamiliki wa migodi kuhakikisha wanakuwa na mipango ya
ufungaji migodi mapema badala ya kusubiri mpaka shughuli za uchimbaji
madini zinapomalizika hivyo kufanya zoezi la ufungaji wa migodi kuwa
gumu huku wakiacha mazingira yakiwa hatarishi.
“Ninapenda
kuwakumbusha kuwa suala la kuwa na Mpango wa Ufungaji wa Migodi ni la
lazima kulingana na Sheria ya Madini pamoja na kanuni zake, hivyo
ninawataka kuhakikisha mnakuwa na mpango ili kuhakikisha mashimo
hayaachwi wazi,” alisema Profesa Kikula.
Awali
akiwa katika mgodi unaomilikiwa na Sisti Mganga Profesa Kikula
alielezwa mafanikio ya mgodi huo ikiwa ni pamoja na kokoto za mgodi huo
kutumika katika ujenzi wa daraja la Mto Wami uliopo mkoani Pwani, reli
ya kisasa ya standard gauge na utengenezaji wa marumaru kwa ajili ya
soko la ndani ya nchi.
Katika
hatua nyingine Mganga alitaja changamoto zinazoukumba mgodi huo kuwa ni
pamoja na tozo kubwa kutoka katika halmashauri na tozo nyingine
zinazotozwa na kijiji cha Kihangaiko pasipo kuwa na risiti pamoja na
ukosefu wa vifaa vya kisasa.
Profesa
Kikula alisema kuwa, suala la tozo litafanyiwa kazi kwa kuliwasilisha
mamlaka za juu kwa ajili ya kufanyiwa kazi na kusisitiza kuwa nia ya
Serikali kupitia Tume ya Madini, ni kuhakikisha wachimbaji wa madini
hususan wadogo wanafanya kazi katika mazingira mazuri yenye faida kubwa
huku wakilipa kodi mbalimbali Serikalini pasipo vikwazo vyovyote.
Wakati
huo huo, akiwa katika mgodi wa uzalishaji wa kokoto wa Gulf Concrete
Limited Profesa Kikula alitoa mwezi mmoja kwa uongozi wa mgodi huo
kuhakikisha wanarekebisha kasoro ya mazingira kwa kuhakikisha vumbi
linalotoka wakati wa shughuli za uchimbaji wa kokoto halisambai kwani
linaathiri wananchi wa vijiji vya jirani katika mgodi huo.
Alisema
ni vyema wakazingatia Sheria ya Mazingira kwani vumbi mbali na kuathiri
wananchi wanaoishi katika vijiji vya jirani linaweza kuathiri
wafanyakazi wa mgodi huo.
Aidha,
alituaka mgodi huo kuendelea kuhakikisha unatoa huduma kwa jamii
inayozunguka mgodi huo na kutumia huduma za ndani ya nchi kama vile
bidhaa pamoja na ajira kwa wazawa.
Katika
hatua nyingine, Profesa Kikula akiwa katika mgodi wa kuzalisha kokoto
wa Yaate Co. Limited, mbali na kuupongeza mgodi kwa kuaminiwa na kupewa
kazi ya kusambaza kokoto kwenye mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa ya
standard gauge unaotelekezwa na kampuni ya Yapi Merkezi na kutoa huduma
mbalimbali kwa jamii inayouzunguka mgodi huo pamoja na ajira, aliutaka
mgodi huo kuendelea kununua bidhaa/huduma kutoka kwa wananchi.
“Kutoa
huduma bora kwa wananchi wanaozunguka mgodi kunaboresha mahusiano na
kupunguza migogoro ya mara kwa mara inayoweza kujitokeza.
Awali
akielezea mafanikio ya mgodi, Mkurugenzi Mtendaji wa Yaate Co. Limited,
Eugen Mikongoti alisema mradi umenufaisha watanzania wengi kwa
kuchangia maendeleo ikiwa ni pamoja na ulipaji wa zaidi ya shilingi
bilioni 1.31 ambazo zimelipwa kama ushuru wa madini kati ya kipindi cha
mwezi Juni, 2018 hadi Januari, 2019 na shilingi milioni 338.8
zilizolipwa kama mrabaha.
Alieleza
mafanikio mengine kuwa ni pamoja na utoaji wa fursa za ajira kwa
watanzania hususan vijana wanaozunguka mgodi na kuziwezesha kampuni
zinazomilikiwa na wazawa kushiriki katika miradi mikubwa hivyo
kuzijengea uwezo wa kitaalam na kupata fursa.
Mikongoti
alitaja mafanikio mengine kuwa ni pamoja na kuwezesha maendeleo ya
wanachi wanoishi karibu na mgodi kupitia huduma za jamii ambapo mpaka
sasa mgodi huo unaendelea na ujenzi wa nyumba za watumishi na kuhudumia
wananchi katika zahanati iliyopo mgodini.
Katika
hatua nyingine Mikongoti alipongeza kazi kubwa zinazofanywa na Tume ya
Madini chini ya Mwenyekiti wake Profesa Kikula ikiwa ni pamoja na
kuwatembelea, kuwapa elimu na kutatua changamoto mbalimbali.
Mwenyekiti
wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula (kulia) pamoja na Kamishna-Tume
ya Madini, Dkt. Athanas Macheyeki (katikati) wakiangalia moja ya bidhaa
zinazotengenezwa na mgodi unaomilikiwa na Sisti Mganga uliopo katika
Wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani tarehe 21 Februari, 2019 ikiwa ni sehemu
ya ziara yake katika mkoa huo yenye lengo la kukagua shughuli za
uchimbaji wa madini ya kokoto, kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji.
Kushoto ni mmiliki wa mgodi huo, Sisti Mganga.
Mmoja
wa watendaji wa mgodi wa kuzalisha kokoto wa Gulf Concrete Company
Limited, ulipo katika Wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani, Ramesh
Annlahamadu (kushoto) akifafanua jambo kwa Mwenyekiti wa Tume ya Madini,
Profesa Idris Kikula (katikati) mara alipofanya ziara kwenye mgodi huo
ikiwa ni sehemu ya ziara yake katika mkoa huo yenye lengo la kukagua
shughuli za uchimbaji wa madini ya kokoto, kusikiliza na kutatua kero za
wachimbaji tarehe 21 Februari, 2019. Kulia mbele ni Kamishna – Tume ya
Madini, Dkt. Athanas Macheyeki.
No comments:
Post a Comment