Waziri
wa Afya Hamad Rashid Mohammed amewataka Madaktari kufanya utafiti wa
kina ili kujua kiwango cha maradhi ya kinywa na meno na namna ya
kupunguza maradhi hayo katika jamii.
Waziri
Hamad ameyasema hayo katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Afya ya
Kinywa na Meno duniani iliyofanyika Mnara wa Kumbukumbu ya Mapinduzi
Kisonge mjini Zanzibar.
Amesema
utafiti huo utaweza kusaidia kutoa taaluma zaidi kwa Walimu
wanaofundisha watoto wakiwa skuli na hivyo kuwajengea uwezo wa kujikinga
na matatizo ya kutoboka kwa meno na kuvimba fizi.
Amefahamisha
kuwa kufanyika kwa utafiti huo kutasaidia kupatikana kwa takwimu sahihi
na kuweza kujua ukubwa wa maradhi hayo na kupatiwa ufumbuzi wake.
Aidha
amewataka wananchi kuvitumia Vituo vya afya na hospitali za serikali
kupata huduma zilizobora ili kuondoa matatizo yanayowakabili.
“Nia
ya Serikali ni kuwa na taifa la watu wenye afya ni vyema kupima afya
zetu angalau mara mbili kwa mwaka katika Vituo vya afya vilivyokaribu
nasi,” alieleza Wazri Hamad
Aidha
Waziri huyo wa Afya aliwaomba wananchi kufanya usafi wa kinywa pamoja
na kuwafundisha watoto namna ya kupiga mswaki ili kuepuka matatizo
kutoboka kwa meno na kutoa harufu katika kinywa.
“Asilimia
90 ya matibabu ya maradhi haya tunayo wenyewe, tiba zaidi ni kuwa
wasafi, hivyo nawaomba sana kuzingatia usafi maana afya ni usafi”
alisisitiza Waziri Hamad.
Waziri
Hamad alitumia fursa hiyo kuwasisitiza Wananchi kuchangia damu kwa
lengo la kusaidia jamii na kuokoa maisha ya wagonjwa ambao wanakabiliwa
na tatizo la kupoteza damu.
Aidha
amewasisitiza madaktari na wahudumu wa afya kuwa Wazalendo na kufanya
kazi kwa bidii pamoja na lugha nzuri wakati wa kuwahudumia wananchi.
Nae
Mkuu wa Kitengo cha Meno na Kinywa Hospitali ya Mnazimmoja Dk Semeni
Shaaban Mohamed kuwa amesema asilimia 90 ya wananchi wana matatizo ya
meno ni vyema kwa jamii kuwa na utamaduni wa chunguza afya ya meno ili
kuepuka madhara ya kutoboka na kung’oka.
Aidha
ameeleza kuwa kitengo chake kinakabiliwa na upungufu wa vifaa vya
upasuaji pamoja na kuiomba serikali kupeleka huduma za meno katika vituo
vidogo vidogo vya afya ili kuondoa usumbufu kwa wananchi kufuata huduma
katika hospitali hiyo.
Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Mohamed akizungumza na wananchi na
Madaktari katika maadhimisho ya siku ya kinywa na meno Duniani
yaliyofanyika Mapinduzi Square Michenzani Mjini Zanzibar, (kushoto)
Naibu Waziri wa Afya Harusi Said Sleiman na kulia ni Mkuu wa Kitengo cha
Meno na Kinywa Hospitali ya Mnazimmoja Dkt. Semeni Shaban Mohd.
Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Mohamed akiwa na mmoja wa madaktari
wa kujitolea kutoka Finland Prof. Ana Pucar akionyesha jinsi ya kupiga
msuwaki katika maadhimisho ya siku ya kinywa na meno Duniani.
Daktari bingwa wa meno Zanzibar Iddi Suleiman akifanyia uchunguzi wa meno mtoto Rashid Msote.
Baadhi
ya wananchi waliojitokeza katika maadhimisho ya siku ya kinywa na meno
Duniani wakiwa kwenye foleni kwa ajili yakwenda kufanyiwa uchunguzi wa
kinywa na meno.
Timu ya madaktari wa kujitolea kutoka Finland wakiwa na furaha katika
siku ya afya kinywa na meno Duniani iliyoadhimishwa Mapinduzi Square
Michenzani Mjini Zanzibar. Picha na Makame Mshenga
No comments:
Post a Comment