Serikali
imehimiza halmashauri nchini kupima maeneo ya vijiji ili kuwamilikisha
wananchi ardhi kwa nia ya kuwapatia hati za kimila na wakati huo
kupanga matumizi bora ya ardhi katika maeneo hayo kwa lengo la kuepuka
migogoro ya ardhi na kuwawezesha wananchi kiuchumi.
Kauli
hiyo imetolewa jana tarehe 12 Februari 2019 na Naibu Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula wakati wa kutoa hati
21 kwa wananchi wa Mamlaka ya Mji mdogo wa Katoro uliopo wilaya ya Geita
mkoa wa Geita pamoja na kutoa Ramani za Urasimishaji kwenye wilaya za
Chato na Geita wakati wa ziara yake ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli
ya serikali kupitia kodi ya ardhi.
Alisema
suala la kupima vijiji ni la lazima na halmashauri zinapaswa kuchukua
hatua za kuwapimia wananchi kwa lengo la kuwawezesha kiuchumi lakini
pia kuleta salama ya miliki ya maeneo yao kwa kuwa kutofanya hivyo
kutasababisha kuwepo migogoro ya mipaka pamoja na kiwanja kimoja
kumilikishwa kwa watu wawili (double allocation).
Akigeukia
suala la urasimishaji, Dkt Mabula alizitaka halmashauri za wilaya ya
Geita kuhakikisha zinarasimisha maeneo yaliyojengwa kiholela na
kusisistiza kuwa salama ya eneo la mtu haliishii kuwekewa vigingi bali
kinachotakiwa ni mtu kumilikishwa ili aweze kuitumia ardhi hiyo kujiinua
kiuchumi kwa kuwa anaweza kuitumia hati yake kwa ajili ya kukopea fedha
benki,
Aidha,
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alikabidhi ramani
za urasimishaji kwa wakurugenzi wa halmashauri mbili za wilaya ya Geita
pamoja na ile ya Chato kwa nia ya kuendesha zoezi la urasimishaji
katika maeneo ya halmashauri hizo.
Sambamba
na hilo Dkt Mabula alishuhudia utiaji saini makubailiano ya kupatiwa
kiasi cha shilingi milioni 180 kwa halmashauri ya wilaya ya Geita kwa
ajili ya kutwaa maeneo mapya ya halmashauri hiyo ambapo alieleza kiasi
hicho cha fedha kitumike kuepuka kero wakati wa kutwaa maeneo hayo.
Kwa
mujibu wa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, fedha
zilizosainiwa ni kama mkopo na halmashauri husika inatakiwa kuuza
viwanja na kurejesha fedha hizo ndani ya miezi mitatu na kubainisha kuwa
Wizara imetengewa shilingi bilioni 7 kwa ajili ya kuzikopesha
halmashauri mbalimbali nchini ili kutwaa maeneo.
Alisisitiza
kuwa ni marufuku kuchukua eneo la mtu bila kulipa fidia na kubainisha
kuwa sheria ya mwaka 2016 inaweka wazi kuwa ukitwaa eneo ndani ya miaka
miwili kama hujalipa fidia basi mwenye eneo anaruhusiwa kubaki na eneo
lake na kiasi cha riba kinaongezeka kila baada ya miezi sita.
Mkurugenzi
wa Halmashauri ya wilaya ya Geita Ally Kidwaka alisema pamoja na
Halmashauri yake kuwa na miji midogo yenye wakazi 50,000 lakini Mji
Mdogo wa Katoro ndiyo unaokuwa kwa kasi na sasa umefikia wakazi wapatao
laki moja. Alisema kutokana na mji huo kukuwa kwa kasi wataalamu wa
upimaji wanatakiwa kuongezwa katika mji huo ili kuepuka changamoto za
urasimishaji maeneo ya mji huo.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Halamashauri ya Wilaya ya Geita Elisha Lupuga
alisema Mji wa Katoro pamoja na kukuwa kwa kasi kwa muda mrefu lakini
ulichelewa kupatiwa mamlaka ya Mji jambo lililochelewesha maendeleo
katika mji huo. Hata hivyo, alisema pamoja na wananchi wa Mji wa Katoro
kuwa na uwezo wa fedha na nyumba nzuri lakini wamekuwa wazito kutoa
fedha kwa ajili ya kupimiwa maeneo yao jambo linalosababisha mji
kutopangika vizuri.
Naibu
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula
akizungumza na wananchi wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Katoro katika mkoa wa
Geita wakati wa kutoa hati za ardhi kwa wananchi wa mji huo kwenye
ziara ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya
ardhi. Kulia kwa Waziri ni Mkuu wa Wilaya ya Chato Mhandisi Ntemi
Musafiri na kushoto ni Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Geita Ally
Kidwaka.
Mkuu
wa wilaya ya Chato Mhandisi Ntemi Musafiri akizungumza wakati wa zoezi
la kutoa hati za ardhi kwa wananchi wa Mji Mdogo wa Katoro mkoani Geita
uliofanywa na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt
Angeline Mabula wakati akihamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali
kupitia kodi ya ardhi. Kulia ni Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Ziwa
Makwasa Biswalo.
Baadhi
ya wananchi wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Katoro mkoani Geita
wakimsikiliza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt
Angeline Mabula wakati akihamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali
kupitia kodi ya ardhi.
Naibu
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula
akitoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Chato mkoa
wa Geita Eliurd Mwaiteleke alipomkabidhi ramani kwa ajili ya zoezi la
urasimishaji katika halmashauri hiyo wakati Naibu Waziri akiwa katika
ziara ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya
ardhi.
Naibu
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula
akimkabidhi hati ya ardhi mmoja wa wakazi katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa
Katoro mkoani Geita Dohoi Shimiyu wakati alipotoa hati 21 kwa wakazi wa
Mji huo akiwa katika kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali
kupitia kodi ya ardhi.
Naibu
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiwa
katika picha ya pamoja na wananchi wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Katoro
mkoani Geita waliopatiwa hati za ardhi wakati Naibu Waziri akiwa katika
ziara ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya
ardhi. Wa tatu kushoto aliyekaa ni Mkuu wa Wilaya ya Chato Mhandisi
Ntemi Musafiri na wa tatu Kulia aliyekaa ni Mwenyekiti wa halmashauri ya
wilaya ya Geita Elisha Lupuga
Mkuu
wa idara ya Ardhi na Maliasili katika Halmashauri ya Wilaya ya Chato
mkoa wa Geita Deogratias Matiya akimuonesha Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba
na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula eneo la uwekezaji la
Lubambagwe (Chato Beach) wakati Naibu waziri akiwa katika ziara ya
kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi mkoani
Geita, Kulia ni Meneja wa Shirika la Nyumba mkoa wa Kagera Benit
Masika.
Mkuu
wa wilaya ya Chato Mhandisi Ntemi Musafiri akimuonesha Naibu Waziri wa
Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula eneo
lililopangwa kwa ajili ya makazi katika uwanja wa ndege wa Chato mkoani
Geita wakati Naibu waziri alipotembelea eneo hilo kwa nia ya
kuhamasisha mpango wa matumizi bora ya ardhi ili kuzuia ujenzi holela
eneo linalozunguka uwanja huo.Na Munir Shemweta, KATORO
No comments:
Post a Comment