Matokeo chanyA+ online




Wednesday, March 13, 2019

NAIBU WAZIRI MASAUNI AOKOA MILLIONI MIA MBILI ZA JPM

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (katikati), akitembelea maeneo ya Chuo cha Taaluma ya Polisi ambacho hivi karibuni kimepokea Shilingi Milioni Mia Saba kutoka kwa Rais Dkt. John Magufuli kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya chuo hicho,Wengine ni viongozi wa chuo.

Jeshi la Polisi nchini limeelekezwa kutumia wafungwa ili kuweza kuokoa kiasi cha Shilingi Milioni Mia Mbili  kati ya Milioni Mia Saba zilizotolewa na Rais Dk. John Magufuli   katika Mradi wa Ujenzi wa Mabweni na Madarasa ya  Chuo cha Taaluma ya Polisi kilichopo  Kurasini jijini Dar es Salaam.
Maelekezo hayo yametolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni alipotembelea majengo chakavu ya chuo hicho baada ya kupokea kiasi cha Shilingi Milioni Mia Saba alizoahidi Rais Dkt. John Magufuli akihutubia katika mahafali ya kuhitimisha Mafunzo ya Kozi za Uofisa na Ukaguzi Msaidizi  chuoni hapo mwishoni mwa mwaka jana 

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, akizungumza na Askari Polisi ambao ni wanafunzi katika Chuo cha Taaluma ya Jeshi la Polisi, wakati alipotembelea chuoni hapo kufuatilia maandalizi ya awali baada ya jeshi hilo kupokea kiasi cha Shilingi Milioni Mia Saba kutoka kwa Rais Dkt. John Magufuli kwa ajili ya ujenzi wa chuo hicho.Ziara hiyo imefanyika leo jijini Dar es Salaam.
“Wizara ina taasisi ya magereza ambayo ina nguvu kazi ya kutosha, na Rais alishaagiza wafungwa watumike katika shughuli za uzalishaji, sioni sababu ya kutumia kiasi hicho cha pesa kuwalipa vibarua wa nje, naagiza muwasiliane na Jeshi la Magereza pamoja na kikosi cha ufundi kilichopo ndani ya Jeshi la Polisi ili muweze kuona ni vipi mnaokoa kiasi hicho”alisema Masauni
Akitoa taarifa ya awali ya ujenzi huo, Mkuu wa Chuo cha Taaluma ya Polisi, Naibu Kamishna Anthony Rutashuburugukwa alitaja  majengo yatakayojengwa kuwa ni ghala la chuo, madarasa matatu,bweni moja la askari wa kiume na bweni lingine la askari wa kike.
Wakizungumza kwa masharti ya kutotajwa majina wanafunzi wa chuo hicho walimshukuru Rais Dkt. Johh  Magufuli kwa kiasi cha fedha alichotoa ili kuweza kujenga sehemu mbalimbali za chuo hicho ikiwemo mabweni ambayo wamekiri ni chakavu na si rafiki kwa matumizi ya binadamu.

No comments:

Post a Comment