Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)
inatarajia kufanya zoezi la uandikishaji wa Wapiga Kura kwa majaribio
katika Kata mbili za Kibuta iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya
Kisarawe, Mkoani Pwani na Kihonda katika Halmashauri ya Manispaa ya
Morogoro, Mkoani Morogoro.
Taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Tume
Jaji (Rufaa) Semistocles Kaijage Jijini Dar es Salaam leo (Jumanne
Tarehe 26.03. 2019) imesema Uandikishaji huo wa Majaribio utakaoanza
Machi 29, hadi Aprili 04, 2019 utafanyika katika vituo 20 vya
kuandikisha Wapiga Kura ikiwa ni vituo 10 katika kila Kata.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa uandikishaji
huo unalenga katika kuvifanyia majaribio vifaa na mfumo wa Uandikishaji
Wapiga Kura ili kubaini changamoto kabla ya kuanza rasmi kwa zoezi hilo.
Imezitaja
sifa za watu watakaoandikishwa katika uandikishaji huo kuwa ni raia wa
Tanzania aliyetimiza umri wa miaka 18 au atakayetimiza umri wa miaka 18
siku ya Uchaguzi Mkuu ujao.
Aidha uandikishaji huo hautawahusu raia
walio chini ya kiapo cha utii wa nchi nyingine, aliyebainika kuwa hana
akili timamu au yuko kizuizini kama mhalifu mwenye ugonjwa wa akili au
yuko kizuizini kwa ridhaa ya Rais.
Taarifa hiyo imeendelea kutaja watu ambao
hawatahusika katika majaribio hayo ya uboreshaji kuwa ni mtu
aliyehukumiwa adhabu ya kifo na mahakama au anatumikia kifungo
kinachozidi miezi sita pamoja na mtu aliyepoteza sifa za kuandikishwa
kuwa Mpiga Kura chini ya Sheria za Uchaguzi au Sheria nyingine yoyote
inayohusu makosa ya uchaguzi.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi pia
inawajulisha wakazi wa Kata hizo zinazofanya Uandikishaji wa Majaribio
na ambao walijiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mwaka
2015 kuwa wanaweza kutumia fursa hiyo kuhakiki taarifa zao katika vituo
walivyojiandikishia.
Wakati huo huo Tume inatoa fursa kwa
Vyama vya Siasa kuweka Wakala mmoja katika kila kituo cha Kuandikishia
Wapiga Kura kwa lengo la kushuhudia na kujiridhisha juu ya taratibu
zitakazotumika pamoja na changamoto zitakazojitokeza ili ziweze kupatiwa
ufumbuzi kabla ya zoezi rasmi la Uandikishaji.
Tume imevitaka Vyama vyenye nia ya kuweka
Mawakala katika uandikishaji huu wa Majaribio kuwasilisha orodha ya
majina ya Mawakala na vituo walivyopangiwa kwa Maafisa Waandikishaji wa
Halmashauri za Kisarawe na Manispaa ya Morogoro.
Kadhalika Vyama vimetakiwa kuwasilisha
nakala mbili za barua za utambulisho zikiwa na picha mbili na nakala
mojawapo kati ya Kitambulisho cha Taifa au Kadi ya Mpiga Kura, Pasi ya
Kusafiria au Leseni ya Udereva na kwamba kila Chama kitagharamia Wakala
wake.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo wakati wa
uandikishaji huo wa majaribio Tume ya Taifa ya Uchaguzi itatumia
runinga, redio, mitandao ya kijamii na magari ya matangazo kwa ajili ya
kutoa Elimu ya Mpiga Kura ili kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi
na kushiriki katika zoezi hilo.
Mwenyekiti wa Tume Mheshimiwa Kaijage
kupitia taarifa hiyo amewaomba wakazi wa Kata za Kibuta na Kihonda
kujitokeza kwa wingi katika Uandikishaji huo wa majaribio na kutoa
ushirikiano kwa Tume wakati wote wa utekelezaji wa jukumu hilo muhimu
kwa mustakabali wa demokrasia ya Taifa.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi hufanya
uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa mujibu wa Ibara ya 74
(6) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoipa Tume mamlaka
ya kusimamia na kuratibu uandikishaji wa Wapiga Kura katika Uchaguzi wa
Rais na Wabunge wa Jamhuri ya Muungano pamoja na Madiwani kwa Tanzania
Bara.
Tume kwa mujibu wa Kifungu cha 15(5) cha
Sheria ya Taifa ya Uchaguzi Sura ya 343 na Kifungu cha 21(5) cha Sheria
ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa Sura ya 292 inapaswa kuboresha Daftari
la Kudumu la Wapiga Kura mara mbili kati ya Uchaguzi Mkuu mmoja na
unaofuata.
No comments:
Post a Comment