Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa onyo
kali kwa baadhi ya Maafisa Elimu wa Mikoa na Wilaya wanaoshirikiana na
walimu kujihusisha na wizi, udanganyifu na uvujaji wa mitihani waache
mara moja tabia hiyo na mwenendo huo kwa sababu unalivunjia heshima na
hadhi Taifa.
“Kamati za Mitihani za Mikoa na Wilaya
ziendelee kusimamia sheria, kanuni na taratibu bila ya woga, upendeleo
na tusiyumbishwe na hatua za kinidhamu na kiutumishi kwa mujibu wa
sheria.Hatua ziendelee kuchukuliwa dhidi ya wote wanaobainika kukiuka
sheria, taratibu na miongozo inayotolewa”.
Waziri Mkuu ametoa onyo hilo leo
(Jumanne, Machi 26, 2019) wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Sita wa
Umoja wa Maafisa Elimu Mikoa na Wilaya (REDEOA), uliofanyika kwenye
ukumbi wa chuo cha Mipango jijini Dodoma. Kauli mbiu ya mkutano huo inasema “Elimu Bora Itatufikisha Katika Uchumi wa Kati Ifikapo 2025”
Amesema Baraza la Mitihani la Tanzania
(NECTA) ni chombo ambacho kwa muda mrefu kimejijengea sifa kubwa sana
nchini na barani Afrika, ambapo Serikali imewekeza kiasi kikubwa cha
rasilimali ili kukifanya chombo hiko kuwa imara na cha kisasa.
Waziri Mkuu amesema hali hiyo imezifanya
nchi mbalimbali kuja nchini kujifunza masuala ya upimaji na uendeshaji
wa mitihani. “Nimejulishwa pia hivi sasa hapa nchini wapo Viongozi wa
Mabaraza ya mitihani kutoka nchi za Afrika Mashariki”.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema suala
la tatizo la nidhamu mbaya ya wanafunzi ni jukumu la walimu wote, hivyo
wanatakiwa watekeleze majukumu yao ya kufundisha, kulea, kuwaongoza na
kuwaendeleza wanafunzi kimwili, kiakili na kiroho kwa uadilifu na
kuzingatia sheria.
Waziri Mkuu amesema Serikali
imesikitishwa sana na matukio ya hivi karibuni ya athari ya viboko kwa
wanafunzi shuleni ikiwemo kuvunjwa mikono, kuachwa na makovu pamoja na
tukio la kifo cha mwanafunzi Sperius Eradius wa shule ya msingi Kibeta
Mkoani Kagera.
“Ninatambua si kusudio la walimu
kuwadhuru wanafunzi lakini tukubaliane kuwa kuna udhaifu katika
utaratibu wa utoaji na usimamizi wa adhabu ya viboko shuleni. Maafisa
Elimu kawakumbusheni walimu wote nchini wazingatie mwongozo wa kutoa
adhabu shuleni chini ya kifungu cha 61 cha sheria ya Elimu sura 353
pamoja na kanuni zake”.
“Adhabu ya viboko itatolewa iwapo
patatokea utovu mkubwa wa nidhamu au kosa kubwa litakalofanywa ndani au
nje ya shule ambalo litaishushia shule heshima. Na adhabu hii itatolewa
kwa kuzingatia umri, jinsia na afya ya mwanafunzi. Nina hakika
tukisimamia utaratibu, matukio haya yaliyoanza kuonekana yatakoma”.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi
OR-TAMISEMI, Selemani Jafo amewapongeza maafisa Elimu wa Mikoa na Wilaya
hao kwa sababu wanafanya kazi kubwa ambayo imechangia kupandisha ufaulu
wa kidato cha sita na cha nne nchini. Amewasisitiza waendelee kufanya
kazi kwa bidii.
Naye, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amewataka maafisa hao wawe wanatoa taarifa sahihi kuhusu idadi ya wanafunzi kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia.
Awali, Mwenyekiti wa REDEOA, Germana Mung’aho amesema umoja wao unatekeleza majukumu yao ya kusimamia elimu kikamilifu nchini, lengo likiwa ni kumuunga mkono Rais Dkt. John Magufuli, ambaye anasisitiza watu wafanye kazi.
Amesema umoja huo una wanachama zaidi ya 400 na ulianzishwa ili kusimamia utoaji wa elimu nchini. Katika mkutano huo wanatarajia kujadiliana changamoto mbalimbali za sera ya elimu na namna ya kuzipatia ufumbuzi.
Kadhalika, Mwenyekiti huyo ameiomba Serikali iwapatie magari maafisa hao watakayoyatumia kwa ajili ya kufuatilia maendeleo ya elimu kwenye maeneo yao ya kazi, ambapo Waziri Mkuu amesema suala hilo linashughulikiwa.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 – Dodoma,

JUMANNE, MACHI 26, 2019.
No comments:
Post a Comment