Tanzania ili iweze kufikia hatima ya
kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi , ofisi ya Taifa ya
takwimu ishirikiane vyema na taasisi pamoja na mashirika ya utafiti
katika kuhakikisha tafiti zinazofanyika zinatoa takwimu sahihi.
Rai hiyo imetolewa leo Jijini Dodoma na
Waziri wa nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mhe.
January Makamba wakati wa uzinduzi wa semina ya wadau kuhusu uanzishwaji
wa ushirikiano wa Kitaifa na Kimataifa wa uzalishaji, usambazaji na
utumiaji wa takwimu za mazingira na mabadiliko ya tabia ya nchi.
”Ripoti zifanane, vitu vyote vyaweza
kuharibiwa lakini sio takwimu, kwani ndio kioo cha kila jambo duniani,
utofauti ukionekana kwenye ripoti itakwamisha wadau na serikali kwenye
mipango ya maendeleo,” amesema Makamba
Mbali na ushirikiano, amesisitiza
watafiti kujengeana uwezo katika kuhifadhi na kuchambua takwimu ili
kufikisha ujumbe kwa walengwa, kwani uchambuzi huo huchangia maamuzi
sahihi ya mipango ya maendeleo.
Aidha, ameitaka ofisi ya Taifa ya Takwimu
na wadau wengine wa kitaifa na kimataifa katika masuala ya tafiti
kuhusu mazingira, wajikite katika kutoa elimu kwa umma juu ya
visababishi na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi, kwani uhafifu wa
uelewa juu ya mazingira unasababisha wananchi kuwa vyanzo vikuu vya
tatizo.
Kwa upande wake Mtakwimu Mkuu wa
Serikali, Dkt. Albina Chuwa, amesema lengo kuu la takwimu za tafiti juu
ya mazingira ni kuhakikisha zinapatikana taarifa rasmi ili kuwasaidia
watunga sera nchini na duniani kote katika kukabiliana na mabadiliko ya
tabia ya nchi.
“Kama takwimu zikiwa sahihi, na za
kutosha, tatizo la tabia ya nchi litakomeshwa kwani hakutakuwepo na
mkanganyiko wa kujiuliza ni nini sababu kuu ya tatizo wakati kila kitu
kitakuwa wazi,” amesema Dkt. Chuwa.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Taifa cha
Takwimu Benedict Mugambi, akizungumza katika ufunguzi wa semina hiyo,
amesema, kuna uhusiano mkubwa kati ya watu, mazingira na uwepo wa
mabadiliko ya tabia ya nchi, hivyo watu wanapaswa kuelimishwa juu ya
utunzaji wa mazingira mahali wanapoishi.
”Katika sensa ya watu na makazi sehemu
yenye watu wengi kuna uharibifu zaidi wa mazingira unaopelekea uwepo wa
mabadiliko ya tabia ya nchi kuliko penye watu wachache,” amesema Mugambi
Mwakilishi kutoka Shirika la Kimataifa la
Maendeleo la Serikali ya Ujerumani (GIZ), Samwel Sudi amesema takwimu
za mazingira zikitumika vyema zinachagiza uwepo wa maendeleo, kwani
taarifa hizo zinasaidia wadau wa maendeleo na serikali kutekeleza mambo
mbalimbali yanayohusu mabadiliko ya tabia ya nchi.
”Tunajitahidi kuweka mikakati ya
kuhakikisha ulimwenguni kote tunakuwa na njia za kuzuia uharibifu wa
mazingira unaosababisha mabadiliko mbalimbali ya nchi ikiwemo mafuriko,
ukame na hewa chafu, hii itasaidia kuwepo kwa maendeleo katika nyanja
zote” amesema Victor Ohuruogu Mwakilishi kutoka Ushirikiano wa Kimataifa
wa Takwimu kwa Maendelelo Endelevu (Global Partinership for Sustainable
Development Data- GPSDD)
Suala la mazingira na hali nzuri ya tabia
ya nchi si la nchi moja pekee, wakati Tanzania ikiweka mikakati ya
kutumia takwimu kukabiliana nalo, wadau wa kimataifa nao wanalipigania
kuhakikisha duniani kote hali inatengamaa.
No comments:
Post a Comment