Na Veronica Simba – Manyara
Waziri
wa Nishati Dkt. Medard Kalemani ametoa karipio kwa mameneja wa Shirika
la Umeme Tanzania (TANESCO) ambao wamekaidi agizo alilolitoa kuhakikisha
wanawaunganishia umeme wananchi waliolipia huduma hiyo kwa wakati na
kuwataka wajisalimishe makao makuu ya Shirika hilo Mei 5 mwaka huu,
wakiwa na barua za kuachia nyadhifa zao.
Akizungumza
na wananchi wa kijiji cha Dosidosi wilayani Kiteto, Mkoa wa Manyara,
jana Aprili 25, akiwa katika ziara ya kazi, Waziri Kalemani alisema
hawezi tena kutoa msamaha kwa mameneja ambao hawajawaunganishia umeme
wateja kwa wakati kuanzia kipindi cha nyuma hadi kufikia mwezi uliopita
(Machi).
“Siwezi
kusamehe tena mameneja ambao hawajawaunganishia umeme wateja kwa muda
mrefu. Hii ni kwa sababu wamesababisha kuleta kero kwa wateja, usumbufu
pamoja na kupotezea mapato Shirika la Umeme,” alisisitiza Waziri.
Katika
hatua nyingine, Waziri alikerwa na hali aliyoishuhudia katika kijiji
cha Nchinira wilayani humo, ambapo nguzo za umeme zinaonekana kusimikwa
kwa muda mrefu pasipo kutundikwa nyaya ili kuwaunganishia wananchi.
Kufuatia
hali hiyo, Waziri Kalemani alilazimika kutoa onyo kali kwa mkandarasi
anayetekeleza Mradi wa Umeme Vijijini wilayani humo pamoja na kumtaka
Meneja wa TANESCO wa Wilaya kuwasilisha maelezo makao makuu ya Wizara,
Dodoma ni kwanini eneo hilo halijaunganishiwa umeme ilhali nguzo
zilishasimikwa kitambo.
“Natoa
onyo kwa Mkandarasi. Maeneo yote mliyosimika nguzo; sitaki kuona nguzo
zimesimama bila kuwa na nyaya na bila kuwaunganishia umeme wananchi. Ni
marufuku. Nguzo zikisimikwa, zitundikiwe nyaya na wananchi waunganishiwe
umeme.”
Waziri alielekeza eneo hilo liwe limeunganishiwa umeme ifikapo wiki ijayo.
Aidha,
akiwasha umeme katika shule ya sekondari iliyopo Kijiji cha Dodisdosi,
Waziri Kalemani alitoa wito kwa walimu na viongozi mbalimbali wa ngazi
za vijiji na mitaa nchi nzima, kulipia gharama za uunganishaji umeme ili
Taasisi mbalimbali za Umma katika maeneo yao, hususani shule zipatiwe
nishati hiyo muhimu.
Alisema
siyo vema shule ikakamilika ujenzi na kuanza kutoa huduma kwa takribani
miaka miwili au zaidi ikiwa haina umeme kwani inaweza kusababisha uduni
wa maendeleo ya elimu katika shule husika.
“Uwepo
wa umeme katika shule husaidia kuongeza hali ya ufaulu kwani pamoja na
mambo mengine, kwa sababu walimu wataweza kufanya vizuri zaidi
maandalizi yao ya kufundisha,” alifafanua.
Waziri
aliwaeleza wananchi wa Kiteto kuwa vijiji vyote vya Wilaya hiyo pamoja
na vitongoji vyake, ambavyo havijaunganishiwa umeme, vitapata nishati
hiyo kwani viko katika orodha ya Mradi wa Umeme Vijijini, Awamu ya Tatu,
Mzunguko wa Kwanza ambao unatarajiwa kukamilika Juni mwakani.
Hata
hivyo, alisema serikali imemuagiza Mkandarasi husika kuhakikisha
anakamilisha kazi ya kuviunganishia vijiji vyote umeme kabla ya Septemba
mwaka huu ili libaki zoezi la kuunganishia umeme wananchi ambalo nalo
litatakiwa kukamilika ndani ya kipindi cha mkataba wake.
Katika
ziara hiyo ya kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme wilayani Kiteto,
Waziri Kalemani alifuatana na viongozi mbalimbali akiwemo Mbunge wa
Jimbo husika Emmanuel Papian, Kaimu Kamishna wa Nishati Juma mkobya,
mameneja wa TANESCO wa Kanda na Wilaya pamoja na wataalamu mbalimbali
kutoka wizarani na REA.
Waziri
wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (mwenye shati la bluu), akizungumza na
mafundi wanaounganisha umeme katika kijiji cha Osteti wilayani Kiteto,
Mkoa wa Manyara, akiwa katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa
miradi ya umeme wilayani humo, Aprili 25, 2019.
Mafundi
wakiunganisha umeme katika nyumba ya mmoja wa wakazi wa kijiji cha
Osteti wilayani Kiteto, Mkoa wa Manyara. Taswira hii ilichukuliwa Aprili
25, mwaka huu wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati, Dkt. Medard
Kalemani (hayupo pichani) kijijini humo kukagua utekelezaji wa miradi
mbalimbali ya umeme.
Waziri
wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (katikati), akitoa maelekezo kwa
Mkandarasi anayetekeleza Mradi wa Umeme Vijijini wilayani Kiteto, akiwa
katika ziara ya kazi wilayani humo, Aprili 25, 2019 kukagua utekelezaji
wa miradi mbalimbali ya umeme na kuzungumza na wananchi.
Waziri
wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (katikati) akikata utepe kabla ya
kuwasha rasmi umeme katika kijiji cha Dosidosi wilayani Kiteto, mkoani
Manyara akiwa katika ziara ya kazi, Aprili 25, 2019.
No comments:
Post a Comment