Mwenyekiti wa Tume Jaji (Rufaa) Semistocles Kaijage |
Tume
ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza uchaguzi mdogo wa madiwani kwenye
kata sita (6) zilizopo kwenye halmashauri sita (6) katika mikoa sita
(6) ya Tanzania Bara.
Mwenyekiti
wa Tume Jaji (Rufaa) Semistocles Kaijage amesema Jijini Dar es Salaam
leo (Jumanne 09.04.2019) kwamba uchaguzi huo utafanyika tarehe 19 Mei
mwaka huu.
Akisoma
taarifa kwa umma iliyotolewa na Tume, Jaji Kaijage amesema kwamba fomu
za uteuzi wa wagombea zitatolewa kati ya tarehe 15 hadi tarehe 19,
Aprili mwaka huu.
Aidha
Mwenyekiti huyo wa Tume amesema kwamba uteuzi wa wagombea pia
utafanyika tarehe 19, Aprili mwaka huu na kampeni za uchaguzi
zitafanyika kuanzia tarehe 20, Aprili hadi tarehe 18 Mei mwaka huu.
Alifafanua kwamba uchaguzi katika kata hizo, utafanyika sambamba na Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Arumeru Mashariki.
“Tume
inapenda kuvikumbusha Vyama vya Siasa na wadau wote wa Uchaguzi
kuzingatia Sheria, Kanuni, Maadili ya Uchaguzi, Taratibu, Miongozo na
Maelekezo yanayotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi wakati wa kipindi
chote cha Uchaguzi huu mdogo,” alisema Jaji Kaijage.
Awali
Jaji Kaijage alisema kwamba maamuzi ya kutangaza uchaguzi kwenye kata
hizo yamefanyika baada ya Tume kupokea taarifa kutoka kwa Waziri mwenye
dhamana na Serikali za Mitaa ambaye kwa kutumia mamlaka aliyopewa chini
ya Kifungu cha 13(1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura
ya 292 aliitaarifu Tume juu ya uwepo wazi wa nafasi hizo.
Alisema kwamba nafasi hizo wazi zimetokana na vifo vya Madiwani watano (5) na mmoja (1) kujiuzulu.
Kata
hizo ni pamoja na Uwanja wa Ndege iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya
Mpanda Mkoani Katavi, Kitobo iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi
Mkoani Kagera, Kyela iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Kyela Mkoani
Mbeya, Mikocheni iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni Mkoani Dar
es Salaam, Mvuleni iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Lindi Mkoani Lindi
na Manda iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma.
No comments:
Post a Comment