Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,
akizungumza, katika mkutano wa Pili wa Pamoja wa Mtandao wa Vyombo vya
Udhibiti wa Nyuklia kwa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa
Afrika (SADC) Aprili 29, 2019.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
amezitaka taasisi zinazofanya uhakiki na upimaji bidhaa nchini
zijirekebishe na ziongeze kasi ya utoaji matokeo kwa wateja.
“Kumekuwa na malalamiko kutoka
mipakani juu ya bidhaa zinazochukuliwa ili zikapimwe kwamba zinachukua
muda mrefu. Punguzeni urasmi huo ili kufanya sekta ya biashara iweze
kwenda kwa haraka zaidi. Tume yako (TAEC), TBS na TFDA ni miongoni mwa
taasisi zinazolalamikiwa na wawekezaji na wafanyabiashara. Tumieni fursa
hii kujirekebisha na kuharakisha utoaji wa matokeo,” amesema.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,
akisalimiana na Meneja Muandamizi wa Kituo cha Kimataifa cha Sayansi na
Teknolojia na Mshauri wa Masuala ya Kidiplomasia (ISTC), Dkt. Kamen
Velichkov, baada ya kufungua mkutano wa Pili wa Pamoja wa Mtandao wa
Vyombo vya Udhibiti wa Nyuklia kwa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za
Kusini mwa Afrika (SADC) Aprili 29, 2019.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo
(Jumatatu, Aprili 29, 2019) wakati akizindua maabara ya Maabara ya
kisasa ya Teknolojia ya Nyuklia ya Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania
(Tanzania Atomic Energy Commission -TAEC) iliyopo Njiro, jijini Arusha.
“Nafahamu kuwa hii Tume inafanya
kazi kwa karibu na bandari vituo vya mipakani ili kudhibiti ubora wa
bidhaa zinazoingizwa nchini. Naamini kuanzia sasa mtaharakisha upimaji
wa bidhaa na vifaa na kutoa majibu ya vipimo haraka,” amesema.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akikata utepe wakati alipozindua Maabara ya Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania Aprili 29, 2019.
Waziri Mkuu ameitaka Bodi na
Menejimenti ya Tume, waendelee kubuni na kuibua miradi mingine zaidi ya
matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia. “Angalieni uwezekano wa
kuanzisha kinu cha utafiti kinachotumia teknolojia ya nyuklia (Research
Reactor); mtambo wa kuongeza thamani na ubora wa vitu mbalimbali ikiwemo
matunda na mazao mbalimbali (multi-purpose irradiator); na mtambo wa
kuzalisha dawa za kuchunguza na kutibu maradhi ya saratani
(accelerator).”
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,
akiweka jiwe la msingi, wakati alipozindua Maabara ya Tume ya Nguvu za
Atomiki Tanzania Aprili 29, 2019.
Amesema kwa kufanya hivyo, maabara
hiyo na watumishi wake wataongeza mchango wa teknolojia ya nyuklia
kwenye ustawi wa jamii na ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Amesema anatambua kwamba Tume ya
Nyuklia Tanzania inakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo uhaba wa
wafanyakazi na ufinyu wa bajeti ya ujenzi wa maabara awamu ya pili.
“Serikali inazichukua changamoto hizo na itaendelea na juhudi za
kuzitafutia ufumbuzi kadiri hali ya kiuchumi itakavyoruhusu,” amesema.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,
akioneshwa kifaa cha kupimia mionzi na Mkurugenzi wa Kinga ya Mionzi,
Dkt Firm Banzi, baada ya kuzindua Maabara ya Tume ya Nguvu za Atomiki
Tanzania Aprili 29, 2019.
Waziri Mkuu ameishukuru Jumuiya ya
Ulaya kwa msaada wa vifaa vya maabara hiyo vyenye thamani ya Euro
milioni 2.2 (sawa na sh. bilioni 7.5) na kwamba Serikali itaendelea
kuwapa ushirikiano katika sekta mbalimbali.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu
ameiagiza Bodi na uongozi wa Tume hiyo wawapandishe vyeo watumishi
watatu wa tume hiyo ambao aliwapa vyeti na zawadi ya sh. milioni moja
kila mmoja kwa kukataa rushwa na kutokubali vitisho walivyopewa.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,
akioneshwa kifaa cha kupimia vifaa vya kupimia mionzi na Mkurugenzi wa
Kinga ya Mionzi, Dkt Firm Banzi, baada ya kuzindua Maabara ya Tume ya
Nguvu za Atomiki Tanzania Aprili 29, 2019.
“Nimefurahi sana kuona watumishi
watatu ambao ni wazalendo na wamekataa kupokea rushwa au kukubali
vitisho walivyokuwa wakipewa na kuamua kusimamia misingi ya kazi zao.
Hii zawadi mliyowapa haitoshi.”
“Watumishi hawa ni mfano wa kuigwa
na wengine. Mwenyekiti wa Bodi waongeze fedha nyingine kila mmoja sh.
milioni mbili ili jumla iwe milioni tatu na wapandishwe vyeo huko waliko
ili iwe motisha zaidi kwao. Sijui muundo wenu ukoje, lakini nataka
nipate taarifa ya utekelezaji wa haya maamuzi kesho kutwa, baada ya Mei
mosi,” amesisitiza.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,
akimkabidhi cheti na pesa kwa kutambua uaminifu wao kwa Mtafiti wa
Mionzi Daraja la Pili, Machibya Matulanya baada ya kuzindua Maabara ya
Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania Aprili 29, 2019.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu
awape vyeti na zawadi, Mwenyekiti wa Bodi, Dk. Najat Mohamed aliwataja
watumishi hao kuwa ni Machibya Matulanya wa kituo cha Mtwara na mpaka wa
Kilambo (Tanzania) na Msumbiji; Patrick Simpokolwe na Geofrey Kalolo wa
kituo cha Tunduma (Tanzania) na Zambia.
Machibya Matulanya ambaye cheo
chake ni mtafiti wa mionzi daraja la pili (Radiation Health Physics
Research Officer II) amekuwa akitegewa mitego ya rushwa na kupokea
vitisho kutoka wa wafanyabiashara na watumishi wa Serikali.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,
akizungumza na wananchi waliohudhuria kwenye uzinduzi wa Maabara ya Tume
ya Nguvu za Atomiki Tanzania Aprili 29, 2019.(Picha na Ofisi ya Waziri
Mkuu).
…………………….
Patrick Simpokolwe ambaye cheo
chake ni mkaguzi wa usalama wa mionzi daraja la pili (Radiation Safety
Inspector II) na Geofrey Kalolo ambaye ni mtumishi wa kujitolea
(volunteer) naye pia anafanya kazi kama mkaguzi wa usalama wa mionzi
daraja la pili. Wote kwa pamoja walipokea vitisho walipozuia mzigo
kutoka Zambia wenye thamani ya zaidi ya milioni 20 usiingizwe nchini.
No comments:
Post a Comment