Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) akijibu swali bungeni leo tarehe 8 Mei 2019 wakati wa mkutano wa kumi na tano wa Bunge la Bajeti Jijini Dodoma.
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma
|
Serikali
kwa kushirikiana na taasisi za sekta binafsi imeendelea kutoa elimu ya
kilimo bora inayojumuisha matumizi sahihi ya mbolea za asili, viuatilifu
vya asili, mbegu bora na hifadhi ya mazingira ili kuzalisha mazao kwa
tija na kuwa na kilimo endelevu.
Naibu
Waziri wa Kilimo, Mhe Omary Mgumba (Mb) ameyasema hayo Bungeni Jijini
Dodoma leo tarehe 8 Mei 2019 wakati akijibu swali la Mbunge wa Chambani,
Mhe Yussuf Salim Hussein aliyetaka kufahamu Serikali imeweka mikakati
gani ya kutoa elimu ya mbolea ya asili kwa wakulima na hatua Serikali
inayoichukua ili kuona kuwa Tanzania ni nchi inayoongoza kwa kuzalisha
mazao yasiyotumia mbolea za viwandani.
Alisema
kuwa katika kutekeleza mpango wa muda mrefu wa matumizi sahihi ya
virutubisho vya udongo, Serikali kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo
Tanzania (TARI) inafanya utafiti wa afya ya udongo katika Kanda zote
saba za kiikolojia za kilimo nchini.
Utafiti
huo unalenga kubaini aina za virutubisho na tabia za udongo katika
maeneo mbalimbali nchini ili kuweza kutoa elimu kwa wakulima kuhusu
kiasi, aina na matumizi sahihi ya mbolea za viwandani na asili. Utafiti
huo umeanza kwa kuchukua sampuli za udongo katika Kanda za Nyanda za Juu
Kusini, Kanda ya Kati, Kanda ya Kaskazini na sehemu ya Kanda ya
Mashariki (Mkoa wa Morogoro) na utaendelea katika maeneo mengine nchini
na kukamilika Juni 2020.
Alisema, kwa
kutambua ongezeko la mahitaji ya mazao na bidhaa za kilimo
zinazozalishwa kwa kutumia mbolea za asili na viuatilifu vya asili,
Serikali imeboresha mtaala wa mafunzo katika vyuo vya kilimo ambapo mada
za kilimo hai na hifadhi ya mazingira zimejumuishwa ili kuwawezesha
maafisa ugani na wakulima kupata elimu hiyo.
Mhe Mgumba aliongeza kuwa Serikali
kwa kushirikiana na Tanzania Organic Agriculture Movemet (TOAM),
Sustainable Agriculture Tanzania (SAT), Ecology Agriculture chini ya
SWISSAID, Zanzibar Organic Producers (ZANOP), Tanzania Alliance for
Biodiversity (TABIO) na TANCERT inatoa elimu ya kilimo hai kwa wakulima
na kutoa vyeti vya ubora wa mazao kwa ajili ya masoko maalum. Baadhi ya
mazao ambayo yanazalishwa katika mfumo wa kilimo hai hapa nchini ni
pamoja na kakao, kahawa, pamba na viungo.
Kadhalika, akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe
Easter Michael Mmasi aliyetaka kufahamu kuhusu ushiriki wa wanawake
kwenye sekta ya kilimo, Mhe Mgumba alisema kuwa Sekta ya Kilimo
inajumuisha sekta ndogo za kilimo mazao, mifugo, uvuvi na misitu.
Bajeti
za Wizara za Sekta ya Kilimo zinajumuisha bajeti za Wizara za sekta
husika, Bodi za mazao na Taasisi mbalimbali zilizo chini ya Wizara za
Kisekta. Utekelezaji wa bajeti hizo huwawezesha wanaume na wanawake
katika shughuli za kilimo. Wanawake wanachangia asilimia 90.4 ya
nguvukazi ya wanawake inayotumika katika shughuli za kilimo na kuchangia
wastani wa asilimia 70 ya mahitaji ya chakula nchini.
Mhe
Mgumba alisema kuwa katika kutatua changamoto hizo Serikali inaendelea
kusimamia utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi
ya mwaka 2004 kupitia mifuko ya uwezeshaji ikiwemo Mfuko wa Maendeleo wa
Wanawake (Women Development Fund – WDF) ambao huchangiwa asilimia 4 ya
mapato ya Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kila mwaka. Katika mwaka
2017/2018, jumla ya Shilingi 15,633,312,764.91 zimetolewa kwa vikundi
2,919 vya wanawake na vijana vyenye jumla ya wanawake wajasiriamali
29,190 katika Halmashauri mbalimbali nchini.
No comments:
Post a Comment