Wafanyabiashara
na wajasiriamali wametakiwa kutumia fursa ya kutangaza biashara zao
kupitia mkutano wa 39 wa jumuiya ya maendeleo wa nchi za kusini mwa
Afrika (SADC) mkutano unaotarajiwa kufanyika nchini tarehe 17 na 18
Agosti mwaka huu.
Akizungumza
na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Waziri wa Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi amesema
kuwa kwa mara ya pili SADC wanatembelea Tanzania na hiyo ni baada ya
taifa kupewa jukumu la kuwa mwenyeji wa mkutano wa 39 wa umoja wa nchi
za kusini mwa Afrika huku Rais Magufuli ambaye kwa sasa ni makamu
mwenyekiti wa umoja huo atakuwa mwenyekiti kwa muda wa mwaka mmoja
akipokea kijiti kutoka Namibia.
Profesa
Kabudi amesema kuwa mkutano wa namna hiyo ulifanyika nchini mwaka 2003
na Rais wa awamu tatu Benjamin Mkapa alihudumu kama mwenyekiti kwa mwaka
2003/2004.
Amesema
kuwa mkutano huo utaanza na maadhimisho ya wiki ya viwanda ya SADC na
kuwataka wajasiriamali na wafanyabiashara kutumia fursa hiyo katika
kujitangaza.
Aidha
amesema kuwa majukumu ambayo mwenyekiti atakuwa nayo ni pamoja na
kusimamia utekelezaji wa shughuli zote za kikanda, kusimamia mikutano ya
kisekta kama vile afya na elimu.
Kwa
upande wake naibu katibu mtendaji kutoka SADC Balozi Joseph Nourrice
amesema kuwa wana amini katika ushirikiano na kufanya kazi kwa pamoja
katika kuhakikisha nchi zilizopo katika umoja huo zina piga hatua.
Mkutano
huo utakaokutanisha wakuu wa nchi 16 utaanza kwa mikutano ya ndani
itakayoanza tarehe 6 Agosti kabla ya kuhitimishwa tarehe 18 mwezi huo na
masuala mbalimbali nyeti na ya kidharura kama mafuriko na maafa katika
nchi za Malawi, Zimbabwe na Msumbiji yatajadiliwa.
No comments:
Post a Comment