Mbunge
wa Jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara, amesema changamoto ya upungufu wa
maji kwa jamii ya wafugaji wa Kata tatu za Orkesumet, Edonyongijape na
Langai itapatiwa ufumbuzi Mei mwakani baada ya mradi mkubwa wa maji wa
mto Ruvu kukamilika.
Millya
aliyasema hayo jana wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha
Lormorjoi kwenye ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo, kusikiliza
kero, changamoto, malalamiko na kuongea na wananchi.
Alisema
mradi huo mkubwa wa maji kutoka mto Ruvu wilayani Same utagharimu kiasi
cha sh 41.5 bilioni pindi utakapokamilika mwakani. Alisema tangu dunia
iumbwe na Mungu, jamii ya wafugaji haijawahi kupata mradi mkubwa wa maji
kama huo utakaokuwa mkombozi kwao. Alisema anamshukuru Rais John
Magufuli kwa kufanikisha mradi huo mkubwa kwani utakuwa msaada wenye
kuhitajika mno kwenye jamii hiyo ya wafugaji.
"Hivi
sasa mkandarasi yupo kwenye eneo la mradi akiendelea kufanya kazi yake
ili kufanikisha shughuli hiyo ambayo itakamilika mwaka ujao," alisema
Ole Millya. Hata hivyo, kaimu mkurugenzi wa halmashauri hiyo Celestine
Silayo alisema mradi huo utawanufaisha pia wakazi wa pembezoni mwa kata
ya Orkesumet kwani walishabainisha kwenye andiko lao.
Silayo
alisema baadhi ya vitongoji vya kata za Langai na Edonyongijape ambavyo
havijawekwa kwenye mradi huo vitaingizwa ili navyo viweze kunufaika na
mpango huo. Mkazi wa kijiji cha Lormorjoi, Julius Saitoti alitoa ombi
kwa mbunge huyo kuhakikisha mradi huo mkubwa wa maji unapita pia kwenye
kijiji chao kwa faida ya jamii na mifugo yao.
Saitoti
alisema jamii ya eneo hilo ina uhitaji mkubwa wa mradi huo ambao kwa
kiasi kikubwa utawanufaisha na wao hivyo wasisahaulike pindi
ukikamilika. Mradi huo mkubwa wa maji wa mto Ruvu ukikamilika unatarajia
kuwanufaisha zaidi ya watu 50,000 wa kata za Orkesumet, Langai na
Edonyongijape, pamoja na mifugo yao.
Mbunge wa jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara James Ole Millya (kushoto)
akimsikiliza Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo Jackson Sipitieck
(aliyevaa shati la kijani) wakati wakikagua majengo ya hospitali ya
wilaya hiyo iliyotengewa kiasi cha shilingi bilioni 1.5
Baadhi
ya wataalamu wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara,
wakitoa maelezo ya miradi mbalimbali iliyofanyika kwenye kata ya Komolo
kwa mbunge wa jimbo hilo James Ole Millya.
Mbunge wa jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara, James Ole Millya akizungumza kwenye mkutano wake na wananchi wa eneo hilo.
No comments:
Post a Comment