Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) inatarajia kufanya upandikizaji wa
ULOTO (bone marrow transplant) mwishoni mwaka huu ikiwa ni utekelezaji
wa azma ya Serikali ya kupunguza idadi ya wagonjwa wanaokwenda
kutibiwa nje ya nchi na kugharimu fedha nyingi.
Katika kufanikisha upandikizaji huu, wataalam 11 wa MNH wanatarajiwa
kwenda nchini India katika Hospitali ya Apollo iliyopo Chennai kwa
kipindi cha mwezi mmoja ambako watajifunza kwa vitendo jinsi ya
kufanya upandikizaji wa ULOTO.
Katika kuhakikisha huduma hii inafanyika hapa nchini, Serikali imetoa
Tshs. 6.2 bilioni na kati ya hizo, Tshs. 3.7 bilioni zimetumika
kufanya maandalizi ya kununua vifaa na kuweka miundombinu ya kutoa
huduma ya upandikizaji wa ULOTO.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Mkurugenzi wa Huduma za Tiba,
Dkt. Hedwiga Swai amesema wataalamu wanaosafiri kwenda India ni
madaktari bingwa watatu wa magonjwa ya damu, watalaam wa maabara
watatu, waandisi watatu wakiwamo wa ufundi, ujenzi na vifaa tiba,
mtalaamu wa fedha ambaye atafanya uchambuzi wa gharama halisi za
huduma hii.
Dkt. Swai amesema mtalaam mwingine ni wa manunuzi ambaye atafanya
uchambuzi yakinifu wa dawa na vitendanishi vinavyotumika na
upatikanaji wake ili huduma ya upandikizaji ULOTO itakapoanza iwe na
mzunguko wa upatikanaji wa vifaa ambao hauna changamoto.
Amesema tayari wauguzi watatu, watalaam wa saratani ya watoto watatu,
mfamasia mmoja na watalaamu wengine wawili wa damu wamepata mafunzo ya
huduma hiyo katika Hospitali ya Apollo iliyopo New Delhi India kwa
kipindi cha miezi mitatu.
Dkt. Swai amesema wataalam hawa wanatarajia kurejea nchini Julai, 2019
na kwamba gharama za kupeleka watalamu hawa kwenye mafunzo ni Tshs. 91
milioni zikijumuisha gharama za mafunzo, nauli, fedha za kujikimu
pamoja na gharama nyingine za mafunzo. Fedha hizi zote zitalipwa na
Muhimbili ili kujenga uwezo wa watalaamu wake.
Amefafanua kwamba uwepo wa huduma hii hapa nchini, itasaidia wananchi
wengi kutibiwa hapa nchini, kujenga uwezo kwa wataalamu wa ndani na
kupunguza mzigo kwa Serikali kupeleka wagonjwa nje ya nchi kwani
gharama za kufanyia hapa zitashuka kufikia kiasi cha chini ya asilimia
50 kwa mgonjwa mmoja.
Amesema takwimu za Muhimbili zinaonyesha wagonjwa takribani 130 hadi
140 wanahitaji huduma ya kupandikizwa ULOTO kwa mwaka na pia, zaidi ya
theluthi mbili ya wagonjwa hao hufariki dunia kwa kukosa huduma hii.
Dkt. Swai amesema nje ya nchi, huduma hii inagharimu kiasi cha Tshs.
200 milioni kwa mgonjwa mmoja ambaye anapandikizwa ULOTO kutoka kwa
ndugu yake wakati akipandikizwa ULOTO wake mwenyewe si chini ya Tshs.
150 milioni,” amesema Prof. Museru.
Naye Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Damu, Dkt. Stella Rwezaura amesema
hatua ya kwanza ya kupandikiza ULOTO ni kumuandaa mgonjwa ambaye
chembechembe zake za damu zina tatizo kama saratani, selimundu au
wagonjwa ambao mifupa yao imekuwa ikishindwa kuzalisha damu.
Amefafanua kwamba chembechembe zinazotumika kupandikiza ULOTO ni
chembechembe mama za kuzalisha damu ambazo hupatikana kwenye ULOTO
(Pluripotent Haemopoietic Stem Cells) au chembechembe mama kutoka
kwenye kitovu cha mtoto mchanga (umbilica cord blood) au kondo la
nyuma la mama.
“Njia ambayo hutumika mara nyingi ni ile ya upandikizaji wa
chembechembe mama za damu (HSCT) kutoka kwenye ULOTO,” amebainisha
Dkt. Rwezaura.
Dkt. Rwezaura amebainisha kuwa huduma hii hufanyika kwa kuwapa tiba
maalum wagonjwa ili kuua chembechembe zote zenye matatizo na kisha
kupandikiza chembechembe mpya zilizopo kwenye ULOTO kutoka kwa ndugu
yake mwenye vinasaba vinavyofanana au chembechembe mpya zilizozalishwa
kutoka kwa mgonjwa mwenyewe baada ya kupata tiba maalum. Huduma hii
ndiyo tiba pekee inayoweza kuponya wagonjwa wenye matatizo hayo,”
amesema Prof. Rwezaura.
Tanzania itakua nchi ya kwanza kupandikiza ULOTO katika Ukanda wa
Afrika Mashariki na pia nchi ya sita katika Bara la Afrika. Kwa sasa
huduma hii Afrika inatolewa Afrika ya Kusini, Tunisia, Misri, Komoro
na Nigeria.
Mbali na kuanzishwa kwa huduma hii, hadi kufikia Juni, 2019, MNH
imeweza kupandikiza figo kwa wagonjwa 43, na wagonjwa 339 wamenufaika
na tiba radiolojia (interventional radiology), na watoto 21
wamepandikizwa vifaa vya kusaidia kusikia (cochlear implant).
Mkurugenzi
wa Huduma za Tiba katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dkt.
Hedwiga Swai akizungumza na waandishi wa habari kuhusu MNH kupeleka
wataalam nchini India kwa ajili ya kujifunza upandikizaji wa ULOTO kwa
wagonjwa ambaye chembechembe zake zina tatizo kama saratani au
selimundu. Kushoto ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Damu wa MNH, Dkt.
Stella Rwezaura.
Baadhi
ya wataalam wa MNH wakimsikiliza Mkurugenzi wa Huduma za Tiba wa MNH,
Dkt. Hedwiga Swai wakati akizungumza na waandishi wa habari leo.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Damu wa MNH, Dkt. Stella Rwezaura akifafanua jambo kwa waandishi wa habari leo.
Baadhi ya waandishi wa habari wakifuatilia mkutano leo kuhusu upandikizaji wa ULOTO.
Wataalam wa MNH wakiwa katika picha ya pamoja kabla ya kuondoka
nchini kwenda India kujifunza kwa vitendo upandikizaji wa ULOTO.
No comments:
Post a Comment