Serikali imesema kuwa
kati ya kipindi cha mwaka 2013 hadi Mei 2019 imetaifisha mali za wahalifu zenye
thamani ya Tsh. Bilioni 93.16 zilizokamatwa kwenye sekta za Madini, Maliasili
na Sekta ya fedha (Upatu) ikiwa ni sehemu ya kudhibiti uhalifu kwenye maeneo
mbalimbali nchini.
Uhalifu huo unaodaiwa
kukithiri katika miaka ya nyuma na ambao sasa unaendelea kudhibitwa unatajwa kuliingizia
Taifa hasara ya Mabilioni ya fedha, hatua iliyoifanya Serikali kuudhibiti kwa
kutaifisha mali za wahusika wa uhalifu huo.
Hayo yalibainishwa leo (Jumatano
Juni 12, 2019) Jijini Dar es Salaam na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan
wakati akifungua mkutano wa maadhimisho ya miaka kumi tangu kuanzishwa kwa
Umoja wa Urejeshaji wa Mali Zinazohusiana na uhalifu wenye jumla ya nchi wanachama 16.
Samia alisema hivi sasa
Serikali ya Tanzania inapanga mikakati ya kuondokana kabisa na uhalifu huo
kutokana na sera ya kudhibiti Rushwa pamoja na kuanzisha mahakama maalum
zitakazoshughulikia ufisadi Nchini Tanzania.
“Sisi Tanzania
tunaimarisha Sera zetu za kupambana na Rushwa na Ufisadi, tunaenda sambamba na
umoja wetu huu wa ARINSA hivyo tunazishauri nchi zingine ambazo zipo kwenye
umoja huu na bado hazijatunga Sera na Sheria ziharakishe mchakato ili twende
sawa” alisema Samia.
Kwa upande wake Waziri
wa Sheria na Katiba, Balozi Augustine Mahiga alisema mkutano huo pamoja na
mambo mengine utazungumzia mikakati ya pamoja ya kudhibiti uhalifu wa mipakani
hasa kwenye udhibiti wa uingizwaji wa bidhaa haramu ikiwepo dawa za kulevya.
Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini
(DPP) Biswalo Maganga alisema mkakati wa kutaifisha mali za wahalifu umekuja
kufuatia kuona vifungo gerezani kwa wahalifu hao havitazinufaisha nchi hizo na
badala yake kuchukua mali zao ili kukomesha kabisa suala hilo.
Aidha alisema tayari
wataalamu kadhaa wa upelelezi wa kufuatilia mali na kuzitaifisha wameshapata
mafunzo na kwamba zoezi hilo linaendelea ili kuhakikisha linafanyika kikamilifu
na kwa usiri mkubwa.
ARINSA ni umoja wa urejeshaji
wa mali zinazohusiana na uhalifu wenye Nchi
wanachama 16 zilizopo Barani Afrika ambao kwa pamoja wanakusudia
kukabiliana na uhalifu hususan kwenye mipaka ya nchi hizo.
No comments:
Post a Comment