Matokeo chanyA+ online




Friday, July 26, 2019

HIFADHI MPYA YA MWL.NYERERE KUKUZA UTALII SELOUS.



Rais Dkt. John Pombe Magufuli ameitaka wizara ya Maliasili na Utalii kutenganisha eneo la uwindaji Selou (Hunting block) kwa kutengeneza Hifadhi ya Taifa ambayo itaitwa Hifadhi ya taifa ya Mwalimu Julius Nyerere.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa mradi wa kufua umeme wa mto Rufiji mkoani Pwani utakaozalisha megawatt 2,115, Rais Magufuli amesema kuwa eneo la uwindaji la Selou ni eneo ambalo limezunguka mradi huo mkubwa wa umeme na lina urefu wa kilomita za mraba elfu 57.

“Eneo la Selou ni eneo kubwa ambalo linachukua takribani kilomita 50, hivyo ni lazima Wizara itenge eneo ambalo litatengenezwa na kuwa Hifadhi kuweza kukidhi mahitaji ya utalii na kukisaidia kizazi kijacho kuendelea kuenzi mambo ambayo ameyafanya baba wa Taifa,” amesema Rais Magufuli.

Amesema maeneo ya uwindaji wa wanyama yanafikia 47 katika mbuga ya wanayama Selou hivyo Wizara ya Maliasili lazima itenge eneo la hifadhi na la uwindaji, ili kuimarisha utalii na kuvutia watalii wengi katika mbuga hiyo

Rais Magufuli alisisitiza kuwepo kwa utaratibu kwa Wizara ya Maliasili na Utalii kuangalia maeneno ambayo yanavitalu wa uwindaji ili kuhakikisha kuwa Serikali inafaidika na maeneno hayo, pia aliagiza barabara ya kutoka Fuga kilomita 60 kwenda mahari ambapo mradi unajengwa ianze kutengenezwa kwa rami ili kufungua sekta ya utalii katika Mbuga ya wanayama Selous.

Aidha, Rais Magufuli amesema kuwa mradi wa kufua umeme wa mto Rufiji ni mradi ambao unaweza kudumu kwa muda wa miaka 60 ambapo utasaidia kuzalisha umeme wa kutosha na kusaidia Tanzania kuweza kutekeleza malengo ya milenia ya maendeleo endelevu.

Amesema mradi wa mto Rufiji utasaidia kuchochea maendeleo katika sekta ya viwanda ambapo wewekezaji wataweza kupata umeme wa uhakika na kwa bei nafuu na wenye kuaminika ili kuweza kuzarisha bidhaa zenye ubora.

“Mradi huu wa umeme wa mto Rufiji unaweza kudumu kwa muda wa miaka 60 na kusaidia watanzania kupata umeme wa uhakika na wenye gharama nafuu ambao utasaidia wawekezaji kupata huduma ya umeme kwa uhakika bila mgao ili kuweza kuzarisha bidhaa zenye ubora na kuweza ushindano kwenye masoko mbalimbali ya kimataifa,” amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli alisisitiza kuwa katika utekelezaji wa mradi huo, mkandarasi anatakiwa kutumia wafanyakazi walioko karibu kwa kazi ambazo siyo za kitaalamu, akasisitiza ajira zitolewe kwa wenyeji wa maeneo ya mradi kwa mikoa ya Morogoro na Pwani, na amewataka wananchi kuchangamkia fursa kwa miezi hiyo 36 ya ujenzi.

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa alisema kuwa Ndoto ya Rais Magufuli ya kuenzi mambo makubwa ya Baba wa Taifa, Mwl.Julias Nyerere ikiwemo utekelezaji wa ujenzi wa bwawa la kufua umeme katika maporomoko ya maji ya mto Rufiji.

“Mhe. Rais, ndoto yako leo imeanza kupata mafanikio, ndoto yako ni kupeleka umeme hadi kule kijijini kwa wananchi wa kawaida na umetoa agizo kuwa kila nyumba ya mtanzania iwe ya bati, nyasi au tembe lazima iwake umeme, kwa hiyo umeme huu ambao ujenzi wake umezinduliwa leo ni kukamilisha azma yako bila kujali maisha ya watanzania”, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Waziri Mkuu alisema kuwa kampuni zinazojenga mradi huo mkubwa wa kufua umeme Tanzania, Els weldey na Arab Contructors, zinafanya kazi nzuri kwa hiyo zitatekeleza mradi huo kwa weledi mkubwa, kama zinavyofanya kule Misri.

Naye Waziri wa Nishati amesema mradi huo unabainisha mambo mawili ya kumuenzi Rais wa kwanza Tanzania, hayati Julius Nyerere, ambayo Rais Magufuli anatekeleza likiwemo kuhamisha makao makuu ya nchi kwenda Dododma, ambayo tayari yanatekelezwa, likiwemo la ujenzi wa Bwawa la Rufiji.

“Naomba niwakumbushe watanzania Mhe. Rais ametengeneza mambo makubwa mawili ya ndoto ya baba wa Taifa ikiwemo kuhamisha makao makuu ya nchi kwenda Dododma na utekelezaji wa mradi mahususi wa bwawa la kufua umeme, mradi mkubwa wa kwanza Tanzania, Afrika Mashariki na wa nne barani Afrika, huku ukiingia kwenye mabwawa 70 makubwa duniani yakuzarisha umeme,” Waziri Kalemani.

Aidha Waziri Kalemani amesema kuwa mradi huu utekelezaji wake utachukua miezi 42 ambapo hadi sasa miezi sita imeshapita na kubaki miezi 36 kukamilisha ujenzi wa mradi huo ambao unategemewa kukamilika Juni 13, 2022.

Waziri Kalemani aliongeza kuwa katika ujenzi wa mradi huo kazi kubwa ya mkandarasi ni pamoja na ujenzi wa bwawa kubwa litakaloweza kuhifadhi maji ya mita za ujazo billioni 33.2, ujenzi wa Power house itakayokuwa na mashine tisa zenye kuzalisha megawati 235 kwa kila mashine na kazi ya mwisho ni kujenga substation yenye kilovolt 400, ambapo ni umeme mkubwa utakaotumika kwenye uchumi wa viwanda.

Umeme huo utasafirishwa kutoka Rufiji kwenda Chalinze umbali wa kilomita 127 kwa dola za kimarekani 188 Chalinze mpaka Dar es Salaam na Dodoma na ndio umeme utakao tumika kuendesha Treni ya kisasa (SGR), lengo la Serikali ni kufikisha megawati 10,000 ifikapo mwaka 2025 kwahiyo mradi huu mkubwa ni kichocheo kikubwa sana kuelekea uzarishaji wa hizo megawati.

Kwa upande wake Waziri wa nishati na umeme kutoka Misri Dkt. Mohamed Shaker amesema kuwa utekelezaji wa mradi huo unaimarisha mahusiano ya Tanzania na Misri katika sekta mbalimbali, ikiwemo ya nishati.

“Ujenzi wa mradi huu mkubwa ni moja ya hatua kubwa katika mahusiano ya nchi mbili ambayo itahamasisha zaidi utekelezaji wa miradi mingine ya undugu kati ya Tanzania na Misri, hususani kwenye nyanja ya umeme, nipende kusisistiza kwamba mradi huu wa umeme Rufiji unaungwa mkono na Rais wa Misri, Abdel Fattah El-Sisi” Waziri Shaker.

Nchi ya Misri itaendelea kushirikiana na Tanzania katika utoaji wa mafunzo ya teknolojia ya kuzalisha umeme, kwani ina vituo 22 vya kutolea mafunzo hayo na imetoa nafasi 50 kwa wataalamu kutoka Tanzania kwenda kujifunza masuala ya ufuaji na uzalishaji umeme.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiangalia eneo la bonde katika mto Rufiji mara baada ya kuweka jiwe la msingi la mradi huo wa umeme.

No comments:

Post a Comment