Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli
akiwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Waziri wa Nishati wa Misri Dkt.
Mohamed Shaker wakivuta utepe kuashiria uwekaji wa Jiwe la Msingi mradi
wa Ujenzi wa Kuzalisha umeme Megawati 2115 katika eneo la mto Rufiji
katikati ya Morogoro na Pwani.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli
akimpongeza Waziri wa Nishati wa Misri Dkt. Mohamed Shaker mara baada ya
kuweka Jiwe la Msingi mradi wa Ujenzi wa Kuzalisha umeme Megawati 2115
katika eneo la mto Rufiji katikati ya Morogoro na Pwani.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli
akifurahia pamoja na viongozi wengine mara baada ya tukio hilo la
uwekaji wa Jiwe la Msingi.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli
akiwa na Mkewe Mama Janeth Magufuli, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Waziri
wa Nishati wa Misri Dkt. Mohamed Shaker, Waziri wa Nishati Medard
Kalemani pamoja na viongozi wengine akisikiliza namna mradi wa Kuzalisha
umeme Megawati 2115 katika eneo la mto Rufiji utakavyokuwa ukifanya
kazi mara baada ya kukamilika.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli
akiangalia michoro ya ujenzi huo mkubwa wa kufua umeme.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli
akizungumza na wananchi kabla ya kuweka jiwe la msingi mradi wa
Kuzalisha umeme Megawati 2115 katika eneo la mto Rufiji.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli
akizungumza na Waziri wa Nishati wa Misri Dkt. Mohamed Shaker wakati
wakielekea kwenda kuweka jiwe hilo la msingi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe
Magufuli akikata utepe kuashiria uzinduzi wa mitambo itakayotumika
katika mradi huo mkubwa wa kufua umeme.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli
akiangalia eneo la bonde katika mto Rufiji mara baada ya kuweka jiwe la
msingi la mradi huo wa umeme.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli
akiwasalimia wananchi mara baada ya kuwasili katika eneo la Mradi.
Eneo la mto Rufiji ambalo litatumika katika ujenzi huo wa kufua umeme kama linavyoonekana. PICHA NA IKULU.
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 26 Julai, 2019
ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme katika mto Rufiji
Mkoani Pwani ambao utakamilika Juni 2022 na kuzalisha megawati 2,115.
Sherehe za uwekaji
wa jiwe la msingi la mradi huo zimefanyika kando ya eneo litakapojengwa bwawa
la maji na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri Mkuu Mhe. Kassim
Majaliwa Majaliwa, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.
Dkt. Tulia Ackson, Waziri wa Nishati wa Misri Mhe. Dkt. Mohamed Shaker,
Mawaziri na Naibu Mawaziri wa Tanzania, Wabunge, Viongozi Wakuu wa Vyombo vya
Ulinzi na Usalama, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya, Viongozi wa Dini, Viongozi
wa vyama vya siasa na viongozi wa taasisi mbalimbali za Serikali.
Ujenzi wa mradi
huo utagharimu shilingi za Kitanzania Trilioni 6.5 na bwawa litakalojengwa
litakuwa la kwanza kwa ukubwa Afrika Mashariki na la nne kwa ukubwa Barani
Afrika, na Mhe. Rais Magufuli amependekeza bwana hilo liitwe Bwawa la Nyerere
ikiwa ni kutambua na kuenzi maono ya Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage
Nyerere aliyetaka kujenga bwawa hilo wakati wa uongozi wake.
Katika hotuba
yake, Mhe. Rais Magufuli ameipongeza Wizara ya Nishati kwa kusimamia
utekelezaji mradi huo na ameeleza kuwa Serikali imechukua hatua za kujenga
bwawa hilo ili kuongeza uzalishaji wa umeme nchini kutoka megawati 1,601 zinazozalishwa
hivi sasa, hadi kufikia megawati 10,000 ifikapo mwaka 2025.
Mhe. Rais Magufuli
amesema pamoja na kutekeleza mradi huo, Serikali itajenga mradi wa kuzalisha
umeme katika mto Ruhudji utakaozalisha megawati 359, mradi wa Lumakali megawati
222, mradi wa kakono megawati 87, Rusumo megawati 80 na mingine itakayotumia
nishati ya gesi, makaa ya mawe, jua, jotoardhi, upepo na urani.
Amewataka
wakandarasi wanaojenga mradi (Arab Contractors na Elsewedy Electric za Misri)
kukamilisha mradi huo kabla ya Juni 2022 hasa ikizingatiwa hakuna tatizo la
fedha ili Watanzania waanze kunufaika mapema.
Waziri wa Nishati,
Mhe. Dkt Medard Kalemani amesema tayari wakandarasi wanaojenga mradi huo
wamelipwa asilimia 15 ya fedha zote za mradi huo ambayo ni sawa na shilingi
Trilioni 1.007 na kwamba ujenzi utahusisha bwawa la maji lenye uwezo wa
kukusanya mita za ujazo Bilioni 33.2, Jengo la mitambo ya kuzalisha umeme
litakalokuwa na mitambo 9, kituo cha umeme na njia ya kusafirishia umeme yenye
urefu wa kilometa 135 hadi kufika Chalinze.
Naibu Spika wa
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson amesema
Wabunge wanampongeza Mhe. Rais Magufuli kwa utekelezaji wa mradi huo na
wanaamini kuwa umeme utakaozalishwa utawasaidia Watanzania na pia kufanikisha
miradi mikubwa inayotekelezwa katika awamu hii ikiwemo ujenzi wa reli na ujenzi
wa viwanda.
Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amesema kuanza
kwa ujenzi wa mradi huo ni mafanikio makubwa ya Mhe. Rais Magufuli ambaye amedhamiria
kuhakikisha kila nyumba ya Mtanzania inapatiwa umeme.
Waziri wa Nishati
wa Misri amewasilisha salamu za Rais wa Misri, Mhe. Abdel Fattah El- Sisi
ambaye ameahidi kufuatilia ujenzi wa mradi huo unaofanywa na kampuni za Misri
na pia ameahidi kuwa nchi hiyo itaendelea kushirikiana na Tanzania katika nyanja
mbalimbali ikiwemo kutoa udhamini wa masomo ya nishati jadidifu kwa wanafunzi
50 ambao watasaidia juhudi za kuongeza uzalishaji wa umeme hapa nchini.
Aidha, Mhe. Rais
Magufuli amewataka Watanzania kujivunia mafanikio haya makubwa ya kuongeza
uzalishaji wa umeme nchini na kutoyumbishwa na wanaopinga utekelezaji wa mradi
huo kwa kigezo cha uharibifu wa mazingira kwani mradi huo utasaidia zaidi
kutunza mazingira kwa watu kutumia umeme badala ya kuni na mkaa zinazotokana na
ukataji wa miti, na pia utasaidia kuwepo uvuvi, kilimo cha umwagiliaji na
kuinua utalii kutokana na Wanyama wengi kupata maji ya uhakika.
“Kwenye hili pori la Selous
kuna hoteli za kitalii za gharama kubwa, kuna vitalu vya utalii 47 na kuna
uwindaji unaendelea, sasa haiwezekani sisi tukitaka kujenga bwawa la kuzalisha
umeme tuambiwe tunaharibu mazingira wakati eneo tunalotumia ni chini ya
asilimia 3 ya pori la Selous.
Mradi huu umekumbana na
upinzani mkali wa ndani na nje ya nchi, lakini kwa kuwa sisi ni Taifa huru na
sio masikini kama watu wanavyodhani, tumeamua kutekeleza mradi huu”
amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Magufuli
ameagiza kumegwa kwa sehemu ya Pori la Akiba la Selous ili iwe Hifadhi ya Taifa
na amependekeza iitwe Hifadhi ya Nyerere na sehemu yenye vitalu vya uwindaji
iendelee, lengo likiwa kuimarisha zaidi uhifadhi wa maliasili katika eneo hilo
na kupata manufaa zaidi.
Ameagiza barabara
ya kuunganisha eneo la mradi huo mpaka Fuga ianze kujengwa kwa kiwango cha lami
hatua kwa hatua ili kurahisisha mawasiliano ya eneo hilo.Pamoja na kutaka
wananchi wa Morogoro na Pwani wapewe kipaumbele katika ajira wakati wa mradi
huo, Mhe. Rais Magufuli ameagiza mradi huo kukatiwa bima ya Taifa, utoaji wa
vibali vya kazi kwa wafanyakazi wa kutoka nje ya nchi ufanyike haraka na vyombo
vya ulinzi na usalama vya Morogoro na Pwani vishirikiane kuulinda.
Pia amewataka
viongozi na wananchi wa Mikoa yote yenye vyanzo vya maji vinavyomwaga maji yake
katika mto Rufiji kuhakikisha wanavitunza vyanzo hivyo ili viendelee kuchangia
maji mengi katika mto Rufiji.
Gerson
Msigwa
Mkurugenzi
wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Rufiji
26 Julai,
2019
No comments:
Post a Comment