Matokeo chanyA+ online




Thursday, July 18, 2019

RAIS MAGUFULI AAGIZA WIZARA YA SHERIA KUPITIA MAGEREZA, AAGIZA KUNUNULIWA NDEGE 3 MPYA NA AAGIZA ASKARI POLISI WAREJESHWE KAZINI



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwapungia mkono wananchi wa Kongwa mara baada ya kuwasili wakati akitokea Chamwino mkoani Dodoma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na viongozi wa kidini wakati akiondoka katika eneo la Makaburi ya Ukoo wa Ndugai katika eneo hilo la Kongwa mara baada ya kuweka shada la maua.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na wananchi wa Kongwa mkoani Dodoma mara baada ya kuwasili wakati akitokea Chamwino mkoani Dodoma.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa anazungumza na Spika wa Bunge ambaye pia ni Mbunge wa Kongwa Job Yustino Ndugai wakati akitoka kuweka shada la maua katika kaburi la Baba mzazi wa Spika Mzee Yustino Ndugai katika eneo la Malalo ya ukoo wa Ndugai.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza katika eneo la Makaburi ya Ukoo wa Ndugai mara baada ya sala fupi iliyofanyika katika eneo hilo
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na wananchi wa Kongwa mkoani Dodoma mara baada ya kuwasili wakati akitokea Chamwino mkoani Dodoma.

Sehemu ya Wananchi wa Kongwa wakisikiliza kwa makini hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli wakati alipokuwa akiwahutubia.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na wananchi wa Kongwa mkoani Dodoma mara baada ya kuwasili wakati akitokea Chamwino mkoani Dodoma.
Sehemu ya Wananchi wa Kongwa wakishangilia wakati wa hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli wakati alipokuwa akiwahutubia.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiweka shada la maua katika kaburi  la Baba mzazi wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai katika eneo la Makaburi ya Ukoo wa Ndugai yaliyopo Chimotolo Kongwa mkoani Dodoma. PICHA NA IKULU

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameiagiza Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na vyombo vyote vya ulinzi na usalama vinavyohusika na masuala ya Mahakama kupita katika Magereza yote nchini ili kuchambua na kuwaondoa Mahabusu ambao hawastahili ama hawalazimiki kuwa Magerezani.
Mhe. Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo wakati akizungumza na wananchi wa Kongwa katika Mkutano wa hadhara uliofanyika Mjini hapo muda mfupi baada kutembelea eneo la maziko ya ukoo wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Yustino Ndugai (ambaye ni Mbunge wa Kongwa) na kuweka shada la maua katika kaburi la Baba yake Mzazi, Marehemu Yustino Ndugai.

Mhe. Rais Magufuli amechukua hatua hiyo ikiwa ni siku 2 tangu atembelee Gereza Kuu la Butimba Mkoani Mwanza na kujionea hali halisi ambapo amekuta Gereza hilo lenye uwezo wa kuchukua wafungwa na mahabusu 900 lina jumla ya wafungwa na mahabusu 1,925 wakiwemo mahabusu wenye makosa madogo yanayoweza kupata dhamana.

Amempongeza Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) Bw. Biswalo Mganga kwa kuchukua hatua mara moja ambapo ndani ya siku 2 amepitia Magereza ya Butimba, Bariadi, Mugumu, Tarime, Bunda na Kahama na kuwaachia Mahabusu zaidi ya 325 wakiwemo Askari Polisi waliokamatwa kwa kuhusika na utoroshaji wa dhahabu Mkoani Mwanza, na ameagiza Askari hao warejeshwe kazini.

“Siwezi kutawala nchi ya machozi, machozi haya yataniumiza, siwezi kutawala nchi ya watu wanaosikitika wapo kwenye unyonge na unyonge wao ni wa kuonewa” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.

Mhe. Rais Magufuli amewapongeza wananchi wa Kongwa kwa kuchapa kazi na kushirikiana vizuri na Mbunge wao katika maendeleo, na amemuelezea Mhe. Ndugai kuwa ni kiongozi mwenye mchango mkubwa kwa Taifa kutokana na kuliongoza Bunge kupitisha bajeti na Sheria mbalimbali zilizoiwezesha Serikali kutetea rasimali za Taifa, kuongeza ukusanyaji wa mapato na kutekeleza miradi mbalimbali mikubwa na yenye manufaa kwa Watanzania wote.
Ameitaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge Railway – SGR), kujenga mradi wa uzalishaji wa megawati 2,115 za umeme katika mto Rufiji, miradi ya maji, ujenzi wa barabara, ujenzi wa hospitali na vituo vya afya, kutoa elimu ya msingi na sekondari bila malipo, kutoa shilingi Bilioni 473 za mikopo ya elimu ya juu na kuongeza bajeti ya dawa kutoka shilingi Bilioni 31 (2015/16) hadi shilingi Bilioni 270 hivi sasa.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amesema kutokana na mafanikio ya kuongeza ukusanyaji wa mapato kutoka shilingi Bilioni 850 (2015/16) hadi kufikia shilingi Trilioni 1 na Bilioni 300 kwa mwezi hivi sasa, Serikali imeweza kufufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kwa kununua ndege mpya 8 zikiwemo 6 zilizowasili nchini na kuanza kutoa huduma ndani na nje ya nchi, na kwamba tayari ameshatoa maelekezo ya kununuliwa kwa ndege zingine 3 (Airbus 2 na Bombardier 1) ili kupanua huduma za usafiri wa anga na kukuza utalii.
Ametoa wito kwa wananchi wa Kongwa kuendelea kuchapa kazi na kudumisha amani, na amewapongeza viongozi wa Mkoa wa Dodoma na Mkoa wa Manyara kwa kukomesha migogoro ya wakulima na wafugaji iliyokuwa ikisababisha mauaji.

Akizungumza katika Mkutano huo, Mhe. Ndugai amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa hatua yake ya kuhamishia Serikali katika Makao Makuu ya Nchi Mkoani Dodoma pamoja na kutekeleza miradi mikubwa ikiwemo ujenzi wa Hospitali ya Uhuru, Uwanja wa Ndege Msalato, barabara za lami za Jiji la Dodoma kilometa 110, kutoa shilingi Bilioni 1.5 kwa ajili ya mradi wa maji wa Kongwa, kujenga Hospitali ya Wilaya ya Kongwa, vituo vya afya vya Ugogoni na Mlali na kujenga chuo cha ufundi.

Mhe. Ndugai amemuomba Mhe. Rais Magufuli kusaidia kujenga barabara ya lami ya Mbande – Kongwa- Mpwapwa hadi kuungana na Barabara Kuu ya Iringa – Dodoma, na kwa ombi lake la kusaidiwa ujenzi wa Shule ya Msingi Sagala iliyoezuliwa na Upepo, Mhe. Rais Magufuli amechangia shilingi Milioni 5 na ameendesha harambee iliyofanikisha kupatikana shilingi Milioni 6.5, mifuko 528 ya saruji na mabati 252.

Kuhusu maombi ya kupelekewa Kikosi cha Jeshi katika Wilaya ya Kongwa ambayo ina historia ya kuwa na kambi ya wapigania uhuru wa nchi nyingi za Afrika, Mhe. Rais Magufuli ameahidi kufanyia kazi maombi hayo. 

Akiwa njiani kutoka Kongwa kwenda Ikulu ya Chamwino, Mhe. Rais Magufuli amesimama kuwasalimu wananchi wa Mbande Mnadani na Mbande Njiapanda ambao wamemshukuru kwa kupatiwa vitambulisho vya wajasiriamali vinavyowawezesha kufanya biashara bila bughudha, na amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge kumega eneo lililo chini ya Tume ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC) kando ya Mbande Njiapanda kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Mabasi, Kituo cha Polisi na Kituo kidogo cha afya, na kuhakikisha eneo la Mbande Mnadani linapatiwa maji na vyoo. Pia amechangia shilingi Milioni 5 kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho cha Polisi.
  
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chamwino
18 Julai, 2019

No comments:

Post a Comment