Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekutana na
kufanya mazungumzo na Rais wa Misri Abdel Fattah Al- Sisi, ambapo
wametumia fursa hiyo kuzungumzia masuala mbalimbali ikiwemo namna ya
kuimarisha ushirikiano baina ya nchi za Tanzania na Misri.
Mbali na kuzungumzia masuala hayo ya
kuimarisha ushirikiano katika nyanja mbalimbali zikiwemo za kisiasa,
kiuchumi na kijamii, pia Waziri Mkuu amemfikishia Rais wa Misri salamu
kutoka kwa Rais wa Tanzania Dkt. John Magufuli.
Mazungumzo
baina ya Waziri Mkuu na Rais wa Misri yamefanyika leo (Jumatano, Juni
10, 2019) Ikulu jiji Cairo, ikiwa ni katika siku ya tatu na ya mwisho ya
ziara yake ya kikazi nchini Misri. Katika ziara hiyo ameambatana na
Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga.
Waziri Mkuu amemaliza ziara yake ya
kikazi nchini Misri ambapo katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Cairo
ameagwa na Waziri wa Kilimo na Uhaulishaji wa Ardhi wa Misri, Dkt. Ezz
Eldien Abo Setit.
Akiwa ziarani nchini Misri, Waziri Mkuu
alikutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Misri, Dkt. Mostafa
Madbouly katika siku yake ya kwanza ya ziara yake, ambapo aliwakaribisha
wawekezaji na wafanyabiashara kutoka Misri waje kuwekeza nchini.
Pia, Waziri Mkuu alitembelea miradi
mbalimbali ya maendeleo nchini humo ambayo ni pamoja na mradi wa ujenzi
wa makao makuu mapya ya nchi hiyo, mradi wa awamu ya pili ya upanuzi wa
mfereji wa Suez Canal na kiwanda kikubwa cha ngozi.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, JULAI 10, 2019.
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, JULAI 10, 2019.
No comments:
Post a Comment