Nchi
za Bara la Afrika Tanzania ikiwemo zimesema wakati umefika sasa kwa
Nchi zilizoendelea kuisaidia Afrika kujitegemea na kuliwezesha kutumia
rasilimali zake yenyewe kwa maendeleo ya watu wake badala ya kulifanya
Bara hilo kama eneo la kupata malighafi ya kuhudumia viwanda za nchi
zilizoendelea.
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,Prof. Palamagamba
John Kabudi ameyasema hayo baada ya kushiriki Mkutano wa Mawaziri wa
Maandalizi ya Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya
Afrika (TICAD 7) uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa
Pacifico jijini Yokohama, Japan.
Ameongeza
kuwa mkutano huo pamoja na mambo mengine umesisitiza umuhimu ya uwepo
wa miundombinu ambayo inaunganisha Nchi za Kiafrika ili kuliwezesha bara
la Afrika kuwa na miundo mbinu ya usafirishaji imara na zenye kuleta
tija kwa wote.
Aidha
Prof. Kabudi ameongeza kuwa ni mkutano huo pia umeazimia kuzitaka nchi
zilizoendelea kuongeza fedha zaidi kwa ajili ya kutoa huduma za kijamii
hususani katika nyanja za afya hususani katika kupambana na
malaria,kifua kikuu na ukimwi sambamba na Afrika kuwajibika kuchukiua
hatua zote za kuhakikisha uwepo wa utawala bora,usalama na Amani.
Akifungungua
mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan, Mhe. Kono Taro
amezipongeza nchi za Afrika kwa kupiga hatua katika maendeleo kupitia
ushirikiano na Japan na kwamba nchi yake itaendelea kuunga mkono
jitihada zinazofanywa na nchi hizo ili kuziwezesha kufikia malengo
ikiwemo mapinduzi ya viwanda.
Mhe.
Taro amesema kuwa, ushirikiano kati ya Afrika na Japan kupitia mpango
wa TICAD umeendelea kuimarika tangu kuanzishwa kwa mpango huo mwaka 1993
na kwamba ni matarajio yake Mktano wa Saba utakuwa wa tija zaidi kwa
pande hizo mbili.
“Nawakaribisha
Mawaziri wenzangu Yokohama ambapo maandalizi ya mkutano wa saba wa
kimataifa wa Tokyo kuhusu maendeleo ya Afrika yanaendelea. Jukumu letu
ni kupitia na kupitisha rasimu ya Azimio la Yokohama na Mpango kazi wake
ili hatimaye litunufaishe sote pale litakapopitishwa na Wakuu wa nchi”
alisema Mhe. Taro.
Naye
Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa
Mkutano huo, Mhe. Sameh Shoukry ameipongeza Japan kwa kuendelea kuandaa
mikutano hiyo ambayo ina nia ya kuifikisha Afrika katika mapinduzi ya
viwanda na kuondokana na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa ajira
kwa vijana na nyingine nyingi.
Kwa
upande wake, Naibu Mwenyekiti wa Kamishenii ya Umoja wa Afrika ambao ni
miongoni mwa waandaaji wenza wa Mkutano wa Saba wa TICAD, Bw. Kwesi
Quartey amesema kuwa, mkutano huo unafanyika wakati Umoja wa Afrika
unaendelea kutekeleza agenda 2063. Agenda hiyo pamoja na mambo mengine
inalenga kuziwezesha nchi za Afrika kufikia maendeleo ya hali ya juu
kwenye sekta mbalimbali zikiwemo afya, elimu, teknolojia na
miundombinu.
Kadhalika
Mkurugenzi wa Kituo cha Huduma za Kanda ya Afrika kutoka Shirika la
Maendeleo la Umoja wa Afrika, Bw. Lamin Manneh alisema kuwa ushirikiano
kati ya Afrika na Japan kupitia TICAD umekuwa na mchango mkubwa kwenye
maendeleo ya Bara la Afrika.
Mkutano
wa Saba pamoja na mambo mengine unatoa fursa ya kupanga mikakati ya
ushirikiano na agenda za kimaendeleo zitakazotelezwa kati ya Japan na
Afrika kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo kuanzia mwaka 2019 hadi 2021.
Agenda
za mkutano wa mwaka huu zinalenga kujadili mageuzi ya kiuchumi na
kuboresha mazingira ya uwekezaji kwa kukuza sekta na uvumbuzi. Pia
kuimarisha usalama na ustahimilivu endelevu kwenye jamii pamoja na
kuendeleza jitihada za kuimarisha amani na usalama barani Afrika. Agenda
za Mkutano wa Saba zinaenda sambamba na agenda 2063 ya Umoja wa Afrika,
Agenda 2030 ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa na maazimio
mengine ya kimataifa kama Mkataba wa Paris kuhusu Mabadiliko ya Hali ya
Hewa.
Mkutano
huu ambao umewashirikisha Mawaziri kutoka nchi za Afrika, na wadau
mbalimbali wa maendeleo unafanyika ikiwa ni maandalizi ya Mkutano wa
Wakuu wa Nchi na Serikali utakaofanyika kuanzia tarehe 28 hadi 30 Agosti
2019.
No comments:
Post a Comment