Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi Dkt Mabula amewataka vijana kujifunza maisha ya baba wa Taifa Mwalimu
Julius kwa vitendo ili matendo ya kiongozi huyo wa kwanza wa Tanzania yaendelee
kukumbukwa. 
Akiwa katika Maadhimisho ya miaka 20 ya kumbukumbu
ya Mwl.  Nyerere katika kanisa Katoliki la Bikira Maria jimbo la Musoma
Parokia ya Butiama mkoani Mara leo tarehe 14 Oktoba 2019 Dkt Mabula alisema, ni
vyema vijana wa watanzania wakatumia hazina ya wazee kama Mwl Nyerere Julius
Nyerere kuwa chachu ya kuishi kwa vitendo. 
"Niwaombe vijana kutumia hazina ya wazee
wetu na kuwa chachu ya kuishi kwa vitendo" alisema Dkt Mabula. 
Dkt Mabula ambaye alikuwa Mkuu wa kwanza wa
wilaya ya Butiama mkoani Mara  alihitimisha salamu zake za miaka 20 ya
kifo cha Mwalimu Nyerere wilayani Butiama kwa kuwataka wananchi kuishi pia kwa
kumcha Mungu kwa kuwa wakati wa uhai wake baba wa taifa aliishi kwa kumcha
Mungu.  
Naibu
 Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (Wa 
tatu kulia) pamoja na viongozi wengine wakiwa nje ya Kanisa Katoliki 
Parokia ya Butiama mara baada ya Misa ya kumuombea Baba wa Taifa Mwalimu
 Nyerere katika Maadhimisho ya Miaka 20 ya kifo chake katika kijiji cha 
Mwitongo Butiama mkoa wa Mara leo tarehe 14 Oktoba 2019. Wa kwanza 
kushoto ni Waziri Mkuu Mstaafu Joseph Sinde Warioba na wa pili kushoto 
ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Phillip Mangula. Kulia ni 
Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Sospeter Muhongo na wa pili kushoto 
ni Mkuu wa Mkoa wa Mara Adam Malima.
Kwa upande wake Waziri Mkuu Mstaafu Joseph
Sinde Warioba alimueleza Mwl Nyerere kuwa alikuwa ni mtu wa maisha ya Mungu
aliyejitahidi kujenga umoja na mshikamano kwa nchi yake na Bara la Afrika kwa
ujumla. 
  Naibu
 Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (Wa 
pili kushoto) pamoja na viongozi wengine wakiwa mbele ya kaburi la 
hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere Maadhimisho ya Miaka 20 ya kifo 
chake katika kijiji cha Mwitongo Butiama mkoa wa Mara leo tarehe 14 
Oktoba 2019. Kulia ni Waziri Mkuu Mstaafu Joseph Sinde Warioba na wa 
pili kulia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Phillip Mangula.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi
(CCM) Phillip Mangula alimuelezea Mwl Nyerere kama mtu aliyepigania haki na
aliyesisitiza kuwa binadamu wote ni ndugu na Afrika ni moja. 
Maadhimisho ya miaka 20 ya kumbukumbu ya Mwl
Nyerere katika kanisa katoliki Parokia ya Butiama mkoani Mara 
yalihudhuriwa pia na  Mkuu wa mkoa wa Mara Adam Malima, Mjumbe wa Kamati
Kuu ya CCM  Steven Wasira, Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Sospeter
Muhongo,  Chief Wanzagi,  Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa
(NHC) Dkt Maulid Banyani na Mkurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania 
Masanja Kadogosa. Na Munir
Shemweta, WANMM BUTIAMA
No comments:
Post a Comment