Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (katikati), akizungumza na wananchi wa kijiji cha Musasa, kilichopo wilayani Chato, alipofika kuwasha rasmi umeme, Novemba 23, 2019. |
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard
Kalemani amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli
haina mzaha katika kutekeleza ahadi ilizotoa kwa wananchi na kwamba itafikisha
umeme katika vijiji vyote nchini ifikapo mwisho wa Desemba mwaka huu kama
ilivyoahidi.
Aliyasema hayo kwa nyakati
tofauti, Novemba 23, 2019 wakati akizungumza na wananchi wa vijiji vya Musasa
na Mutundu, vilivyopo wilayani Chato, Mkoa wa Geita.
“Nafahamu kiu ya umeme
mliyonayo wananchi. Tafadhali muiamini Serikali yenu. Umeme utawafikieni nyote
kama tulivyoahidi.”
Akitoa mfano kuthibitisha
namna serikali inavyochapa kazi ili kutimiza ahadi zake, hususan katika
kuwapelekea umeme wananchi; Waziri Kalemani alisema kwa Wilaya ya Chato yenye
jumla ya vijiji 115, tayari vijiji 101 vimeunganishwa kutoka vijiji 9 tu
vilivyokuwa na nishati hiyo mwaka 2015.
Alisema kuwa dhamira ya
serikali ni kuhakikisha vijiji vyote vya Tanzania Bara vikiwemo vya Chato
vinakuwa na umeme ifikapo mwisho wa mwezi Desemba mwaka huu.
Aidha, Waziri Kalemani
aliwasha umeme katika Zahanati ya Kijiji cha Mutundu, Ofisi ya Serikali ya Mtaa
wa Musasa pamoja na Mradi wa Maji katika eneo hilo huku akisisitiza maelekezo
ya serikali kuwa kipaumbele cha umeme vijijini ni kwa Taasisi za Umma ili
kuziwezesha kutoa huduma bora kwa wananchi.
Aliwataka wananchi kulinda
miundombinu ya umeme katika maeneo yao kwani kuihujumu kwa namna yoyote ni
kinyume cha sheria na ni hatari kwa maisha yao.
Vilevile, aliendelea
kusisitiza wananchi waliofikiwa na miundombinu ya umeme katika maeneo yao,
kulipia gharama za kuunganishiwa nishati hiyo na waachane na kasumba
iliyozoeleka na wengi kuwa wanasubiri nguzo kwani hilo siyo jukumu la
mwananchi.
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (katikati), akizungumza na wananchi wa kijiji cha Musasa, kilichopo wilayani Chato, alipofika kuwasha rasmi umeme, Novemba 23, 2019. |
Kwa upande wao, viongozi wa
vijiji husika akiwemo Diwani wa Kata ya Butengolumasa, Jeremia Mswanzali,
walitoa pongezi nyingi kwa Rais Magufuli na Waziri Kalemani kwa jitihada
wanazofanya kuwapelekea wananchi wanyonge maendeleo hususan umeme vijijini.Veronica Simba - Geita
No comments:
Post a Comment