Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) katika kipindi cha miaka minne ya Uongozi wa Serikali ya Awamu
ya Tano, imefanikiwa kukusanya kiasi cha Tsh Trilioni 58.3/- ikilinganishwa
makusanyo ya Tsh trilioni 34.97/- katika kipindi cha miaka minne iliyopita.
Hayo yamebainishwa
leo (Jumatatu Novemba 25, 2019) Jijini Dar es Salaam na Naibu Kamishina Mkuu wa
TRA, Msafiri Mbibo wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa vyombo vya
habari kuhusu mafanikio ya taasisi hiyo katika kipindi cha miaka minne ya
Uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano.
Mbibo alisema mwaka
2015/16, makusanyo ya mapato ya Mamlaka hiyo yalifikia Tsh trilioni 12.5/-,
mwaka 2016/17 makusanyo yaliongezeka na kufikia Tsh Trilioni 14.4/-, mwaka
2017/18 makusanyo yaliongezeka pia hadi kufikia Tsh trilioni 15.5/- na mwaka
2018/19 makusanyo yaliongezeka zaidi na kufikia Tsh trilioni 15.9 na kufanya
makusanyo yote ya jumla kufikia Tsh triloini 58.3/-.
‘Kwa miaka hii minne
ya Serikali ya Awamu ya Tano, TRA imekuwa ikikusanya wastani wa Tsh trilioni
1.3 kwa mwezi ikilinganishwa na wastani wa Tsh Bilioni 850/- kabla ya Awamu ya
Tano haijaingia madarakani, sambamba na ongezeko hilo, kuanzia Julai hadi
Oktoba 2019/2020 wastani wa makusanyo umepanda hadi kufikia Tsh trilioni 1.45/-
kwa mwezi’’ alisema Mbimbo.
Aliongeza kuwa
mafanikio hayo yametokana na msukumo wa Serikali ya Awamu ya Tano wa kuendelea
kuboresha mikakati ya kuimarisha ukusanyaji wa mapato, kuibua vyanzo vya kodi
pamoja na utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Tano wa TRA wa ukusanyaji wa kodi
wenye dhamira ya kuongeza makusanyo ya kodi za ndani kwa kukuza ulipaji kodi wa
hiari.
Akifafanua zaidi
Mbibo aliongeza kuwa sababu nyingine za kuongezeka kwa makusanyo hayo ni
kuimarika kwa matumizi ya Mashine za Kielekroniki za Kutolea Risiti (EFD)
badala ya stakabadhi zinazoandikwa kwa mkono, pamoja na kuboresha mifumo ya
makusanyo inayoendana na mazingira ya sasa ya ukuaji wa sayansi na teknolojia.
Akizungumza kuhusu Mfumo
wa Stempu za Kodi za Kielektoniki (ETS), Mbibo alisema mfumo huo ulioanza
kutumika kuanzia Januari mwaka huu, umeiwezeha TRA kukusanya Tsh Bilioni 77.8/-
uliotokana na ushuru wa bidhaa, kodi ya ongezeko la thamani na Kodi ya mapato
yaliyokana na bidhaa za vileo, vinwaji baridi, maji, juisi na CD/DVD.
‘’Kutokana na
utekelezaji wa mfumo huu kwenye eneo la pombe kali na mvinyo tu, TRA imekusanya
ushuru wa bidhaa wa kiasi cha Tsh Bilioni 77.8/- kwa kipindi cha mwezi Februari
hadi Oktoba 2019 sawa na ongezeko la Tsh Bilioni 19.6/- au ukuaji wa asilimia
34 ukilinganisha na kiasi cha Tsh Bilioni 58.2 kilichokusanywa kipindi kama
hicho mwaka jana’’ alisema Mbibo.
Akibainisha mafanikio
mengine, Mbibo alisema kufuatia mabadiliko ya Sheria ya Kodi na Mapato ya yaliyofanywa
kupitia Sheria ya Fedha ya mwaka 2019, Serikali imeweza kupunguza kiwango cha
kodi kwa wafanyabiashara wadogo kutoka Tsh 150,000/- hadi kufikia Tsh 100,000/-
kwa wale wenye mzunguko wa mauzo yanayozidi Tsh Milioni 4 kwa mwaka.
‘Kwa wafanyabiashara
wadogo wenye mauzo kati ya Tsh Milioni 7- 12/- viwango vya kodi vimepunguzwa
hadi kufikia Tsh 250,000/- kutoka Tsh 318,000/- wakati wafanyabiashara wenye
mauzo kati ya Tsh Milioni 11- Milioni 14/- vinwango vya kodi vimepunguzwa hadi
kufikia Tsh 450,000/- kutoka Tsh 546,000/-‘’ alisema Mbibo.
Mbibo alisema
mafanikio mengine ya TRA ni kutangaza msamaha maalum wa riba na adhabu kwenye
malimbiko ya madeni ya kodi kwa asilimia 100 tofauti na asilimia 50
ilivyokuwepo, ambapo lengo la msamaha huo ulitangazwa Julai mwaka 2018 ni
kuwapa fursa walipakodi kulipa kodi ya msingi mara moja au kwa awamu ndani ya mwaka wa fedha 2018/19.
Anaongeza kuwa
kutokana na hatua hiyo, jumla ya walipakodi 9,406 waliomba msamaha na
waliokidhi vigezo na kukubakliwa ni walipakodi 8687, ambapo jumla ya Tsh
Bilioni 328.4 za riba na adhabu zilisamehewa wakati jumla ya Tsh Bilioni 458.58
zinaendelea kukusanywa kama kodi ya msingi.
‘’Mpaka sasa, Mamlaka
imeshakusanya Tsh. Bilioni 120.01 kutokana na kodi ya msingi inayotakiwa
kulipwa na walipakodi waliosamehewa riba na adhabu, pia Serikali iliongeza muda
uliowekwa awali wa Juni 30, 2019 kuwa Desemba 31, 2019’’ alisema Mbibo.
No comments:
Post a Comment