Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe amewasilisha Itifaki ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Mitandao ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (EAC
Protocol on ICT Networks) kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu ili
waweze kuipitia na kuridhia kabla ya kuiwasilisha kwenye Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania
Baada ya Kamwelwe
kuwasilisha Itifaki hiyo mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu
chini ya Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Selemani Kakoso, Kamati ilipokea Itifaki
hiyo na kualika wadau wa Sekta ya Mawasiliano ili waweze kufika mbele ya Kamati
hiyo na kutoa maoni yao
Kamwelwe
aliwaeleza wajumbe wa Kamati hiyo kuwa madhumuni ya Itifaki hiyo ni kuendeleza
uunganishaji wa miundombinu ya TEHAMA mipakani; kuwezesha matumizi ya pamoja ya
miundombinu ya TEHAMA, ikiwa pamoja na masafa na namba; kuwezesha matumizi ya
huduma za mitandao ya TEHAMA bila upendeleo; kuendeleza matumizi ya huduma za
mitandao ya TEHAMA Serikalini na kwenye sekta binafsi ikijumuisha Serikali
Mtandao, Biashara Mtandao, mfumo wa “Geospatial Information System (GIS)” na
utangazaji; kuwianisha sera, sheria na programu za TEHAMA zitakazowezesha
kufikiwa kwa malengo ya itifaki; kutoa elimu bora na mafunzo yanayohitajika kwa
ajili ya uongozi wa kimkakati, usimamizi, utafiti na ujuzi katika eneo la
mitandao ya TEHAMA ndani ya Jumuiya; kuendeleza mashirikiano baina ya sekta ya
umma na binafsi; kuwezesha upatikanaji wa mawasiliano kwa wote hususan
kuunganisha visiwa na nchi zisizopakana na bahari; na kuhakikisha usalama na
ubora wa huduma za mawasiliano na kuwezesha matumizi salama ya mtandao.
Aliongeza
kuwa kwa upande wa Tanzania, nchi yetu imejiimarisha kwa kuweka miundombinu
muhimu ya TEHAMA ambayo ni pamoja na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ambao
umejengwa na kufika katika Mikoa 26 ya Tanzania Bara pamoja na Zanzibar na kufikisha
kwenye maeneo tisa ya mipaka na nchi jirani ikiwemo Kenya, Rwanda, Burundi na
Uganda ambapo kuna watoa huduma za mawasiliano wa nchi hizo wanaotumia Mkongo
wa Taifa. Pia, nchi za Rwanda, Uganda, Zambia na Malawi zinategemea uwepo wa
miundombinu ya TEHAMA ya Tanzania kuwasiliana kimataifa. Vilevile, watoa huduma
wa nchini Kenya wanatumia Mkongo wa Taifa wa Tanzania kupitisha mawasiliano
yake kwenda nchi nyingine. Miundombinu mingine iliyopo ni Kituo cha Taifa cha
Kuhifadhi Data, Vituo sita vya maunganisho ya watoa huduma za intaneti
(Internet Exchange Point – IXPs), miundombinu ya utangazaji pamoja na Mfumo wa
Kuratibu na Kusimamia Mawasiliano (Telecommunication Traffic Monitoring
System-TTMS).
Pia, Serikali inaendalea kukamilisha Mkakati wa Taifa wa Mtandao
wa Kasi (National Broadband Strategy).
Wakitoa
maoni yao kuhusu Itifaki hiyo mbele ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Miundombinu, wadau mbali mbali wakiwemo Kampuni ya Simu ya Airtel, Shirika la
Mawasiliano Tanzania (TTCL), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Kituo
cha Taifa cha Kuhifadhi Data (NIDC) wameridhia Itifaki hiyo na kuomba Bunge
kupitia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu iliridhie na kupitisha Itifaki
hiyo
Meneja
wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, Adin Mgendi alisema kuwa, “Itifaki hii
imekuja wakati muafaka, Tanzania imekuwa mdau wa Jumuiya ya Afrika Mashariki,
imejenga miundombinu na kuwezesha nchi za jirani zisizopakana na bahari kupata
mawasiliano. Itifaki hii itatuweka mahali pazuri na tutashirikiana vema, kwa
sasa tunaingia makubaliano baina ya nchi mbili na kupeleka mawasiliano, ila
tukitofautiana hakuna pa kwenda, ila kupitia itifaki hii tutaendelea kufungua
masoko EAC na nchi za SADC ambapo hadi sasa tumeunga Malawi na tunaendelea
Msumbiji,”.
Naye
Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi na Utekelezaji wa TCRA, Dkt. Phillip Filikunjombe
alisema kuwa Itifaki hii ikipitishwa, nchi wanachama wa EAC tutakuwa na fursa
ya kukaa pamoja na kuja na sheria zinazofanana na zinazoendana na matakwa ya
nchi yetu katika kudhibiti uhalifu mtandaoni
Filikunjombe
alifafanua kuwa Tanzania tumefunga mtambo wa TTMS ambapo Itifaki hii
inazungumzia mifumo ya kudhibiti usalama wa mtandao kwa kuwa Tanzania sio
kisiwa na uhalifu mtandao hauna mipaka, tutahakikisha nchi za wenzetu wanakuwa
na mifumo yenye viwango vinavyohitajika kudhibiti usalama kwa kuwa hawana mfumo
kama TTMS hivyo tutahakikisha nao wanafunga mifumo ya kudhibiti uhalifu wa
mtandao na usalama
Mwakilishi
wa Airtel, Delfina Martin alisema kuwa kampuni yao imeridhia Itifaki hii na
itapunguza gharama za mawasiliano kwa wateja wao wanaowasiliana kutoka nchi
moja kwenda nchi nyingine kwa kuwa hadi sasa Airtel wapo nchi 16 za Afrika na wana makubaliano ya moja
kwa moja ya kutumia miundombinu na huduma za mawasiliano
Baada
ya kupokea maoni ya wadau, Kakoso amesema kuwa Kamati yake imeridhia Itifaki
hiyo na itawasilisha taarifa yake Bungeni na kuunga mkono Serikali kupitia
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ili Itifaki hiyo iweze kuridhiwa kupitishwa
na Bunge
No comments:
Post a Comment