Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Hamisi Kigwangalla akipanda mlima Kilimanjaro akiwa ameambatana na kunndi la wasanii na wadau mbalimbbali kwa lengo la kuutangaza mlima Kilimanjaro hivi karibuni. |
Waziri wa Malisili na
Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla amesema ataongoza kampeni ya kuvitangaza vivutio vya
utalii vilivyopo katika ukanda wa kusini na ukanda wa Kaskazini magharibi
kwenye hifadhi mpya za Taifa zilizotangazwa hivi karibuni.
Amesema kampeni hiyo itawahusisha
wasanii na watu maarufu wenye ushawishi katika jamii na inalenga kuhamasisha
utalii wa ndani na kutangaza vivutio vya utalii vilivyo katika hifadhi za Taifa
za Ruaha,Mikumi, Nyerere na Burigi – Chato.
Dkt.Kigwangalla
ameyasema hayo alipokuwa akizugumza na Menejimenti ya Shirika la hifadhi za
Taifa nchini (TANAPA) na wakuu wa Kanda wa shirika hilo jijini Arusha.
Amesema hatua hiyo ya
kuwatumia wasanii na watu maarufu wenye ushawishi katika jamii inalenga kuogeza
hamasa kwa watanzania wavijue na kuvitembelea vivutio vya utalii vilivyopo
katika hifadhi hizo hivyo kuogeza idadi ya watalii wa ndani.
Dkt.Kigwangalla
amesema wasanii hao na watu maarufu wana wafuasi wengi wanaofuatilia kazi zao
na matukio wanayofanya katika jamii kupitia vyombo vya habari na mitandao ya
kijamii hivyo ni vyema wakatumika kutangaza utalii katika maeneo hayo.
Amesema hatua kazi
hii ya kuhamasisha utalii wa ndani ni vyema wadau na watumishi walio kweye
sekta husika wakawa wa kwanza kuvijua vivutio vya utalii vilivyopo katika
maeneo mbalimbali ili iwe rahisi kuvielezea na kuvitagaza.
“Tukitaka kutagaza
soko la utalii wa ndani lazima sisi wenyewe tuanze kwanza kuyajua maeneo ya vivutio
tuliyonayo ili iwe rahisi kuwafikia watu wengine, tuna marafiki zetu ndani na
nje ya Tanzania inakua rahisi kwetu kuwaalika na kuwakaribisha kwenye vivutio
hivyo kwa kuwa sisi wenyewe tunavijua” Amesisitiza Dkt.Kigwangalla.
Amesema mkakati wa
sasa ni wa kusambaza uelewa kuhusu vivutio vilivyopo ndani ya nchi ili
kuwahamasisha watanzania wengi zaidi kutembelea vivutio hivyo akibainisha
kwamba mkakati huo utakuwa na matokeo ya haraka na gharama nafuu ya kuhamasisha
utalii wa ndani katika maeneo mengine ya nchi tofauti na ilivyo sasa ambapo
watu wengi wanayafahamu maeneo machache na hasa yaliyo mikoa ya Kaskazini.
“Nilipoamua
kuutangaza mlima Kilimanjaro na mimi mwenyewe kushiriki kupanda
mlima kila mtu alishuhudia nini kilichotokea, kila mtu alikua akiuzungumzia
mlima na hii inaongeza umaarufu wa mlima ndani ya nchi huu ni mkakati
tunaotakiwa kuutumia katika maeneo mengine” Amesema.
Dkt. Kigwangalla ameiagiza
TANAPA iendelee kukusanya takwimu za makundi mbalimbali ya watalii wa ndani wanafanya
utalii katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo watazania wanaoshiriki mbio za
marathon.
Katika hatua nyingine
Waziri wa Maliasili na Utalii ameiagiza TANAPA kuifanyia kazi na kuikamilisha
miradi ya ujenzi wa magati na ununuzi wa vivuko na Boti zitakazokuwa zikitumika
kusafirisha watalii katika ukanda wa Pwani wa Bahari ya Hindi kwenye eneo la
Hifadhi ya Taifa ya Saadani.
Amesema gati hizo
zitajengwa Dar es salaam, Saadani, Pangani, Pangani na Tanga ili kuwezesha boti
hizo kusimama katika maeneo hayo yenye vivutio vya utalii na kushusha watalii wanaotaka
kutembelea maeneo hayo.
“Hili ni eneo muhimu
sana kwetu na rahisi kuuza huduma zetu za utalii wa ndani ya maji kutokana na
uwepo wa visiwa na idadi ya watu wanaokwenda kuvitembelea, Ni lazima tujipange
kuzitumia fursa hizi kwa kuwa na boti nzuri zitakazowawezesha watu kufanya
utalii, mikutano, harusi na sherehe mbalimbali ndai ya maji na hii itakua ni
Biashara kubwa kwetu na njia moja nzuri ya kulitumia vizuri eneo la bahari
tulilo nalo” Amesisitiza Dkt. Kigwangalla.
Amesema ili
kuitangaza hifadhi ya Taifa ya Saadani ni lazima kuiunganisha na utalii wa
fukwe ili kuwavutia watalii wengi zaidi na kuongeza kuwa hifadhi hiyo kutokana
na maeneo mazuri yaliyopo,sehemu za kulala na ukaribu wake na Bagamoyo na Dar
es salaam.
Dkt. Kigwangalla
amefafanua kuwa uanzishaji safari za boti za siku kutokea Dar es Salaam kwenda
Bagamoyo na kurudi Dar es salaam utawawezesha watalii kwenda kati katika maeneo
hayo kwa haraka na ni rahisi kuuza huduma hiyo kwa wageni watakaokuwa
wanakwenda kufanya utalii mwisho wa wiki na kuiwezesha Serikali kupata faida ya
kiuchumi kutokana na uwepo wa huduma hizo.
Na.Aron Msigwa – WMU
Na.Aron Msigwa – WMU
No comments:
Post a Comment