Tume ya Madini imetangaza zabuni kwa ajili ya ununuzi wa
maeneo 10 yenye leseni hodhi za
madini na yenye ukubwa wa kilomita za mraba
381.89 yaliyopo katika maeneo ya Ngara – Kagera, Kahama- Shinyanga, Chunya-
Mbeya, Bariadi na Busega – Simiyu, Morogoro, Nachingwea – Lindi ambayo awali
leseni hodhi zake zilikuwa zimerudishwa Serikalini.
Uamuzi huo umetangazwa
tarehe 19 Desemba, 2019 na Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula
kupitia mkutano wake na waandishi wa habari
uliofanyika jijini Dodoma na
kuhudhuriwa na Kamishna wa Tume ya Madini, Dkt. Athanas Macheyeki, Katibu
Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya pamoja na watendaji wengine
wa Tume ya Madini.
Profesa Kilula alifafanua
kuwa, awali mwaka 2017 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha
marekebisho ya Sheria ya Madini Sura Namba 123 na kanuni zake ambapo pamoja na mambo mengine, zilizokuwa
leseni hodhi za madini ( retention
licence) zilirudishwa Serikalini .
Alisema baada ya marekebisho
hayo maeneo yote 10 yenye ukubwa wa
kilomita za mraba 381.89 yalirudishwa Serikalini na kuongeza kuwa, wachimbaji
wa madini wengi wamekuwa wakiulizia maeneo hayo mara kwa mara lengo likiwa ni
kuomba leseni za uchimbaji madini.
Aliendelea kusema kuwa,
baada ya uchambuzi wa kina kufanyika, Serikali kupitia Tume ya Madini, maeneo yote 10 yaliyokuwa na
leseni hodhi yatatolewa kwa zabuni na kukaribisha kampuni za uchimbaji wa
madini na watu binafsi wenye uwezo wa
fedha na utaalam katika miradi ya uchimbaji wa madini na wenye nia ya kuendeleza miradi ya madini
ya nickel, dhahabu na rare earth elements kuomba zabuni hizo.
Aliongeza kuwa, mwekezaji
atakayeonesha nia ya kuwekeza katika maeneo hayo atakuwa na jukumu la kufanya kazi na kuwaendeleza wachimbaji
wadogo wa madini.
Katibu Mtendaji wa Tume ya
Madini, Profesa Shukrani Manya (kushoto)
akifafanua jambo katika mkutano huo.
|
Wakati huo huo, Katibu
Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya akielezea hatua
zinazochukuliwa kwa wamiliki wa leseni
wasioendeleza maeneo yao, aliwataka wamiliki na waombaji wote wa leseni za utafutaji na uchimbaji wa madini wenye mapungufu kurekebisha mapungufu hayo ndani ya
siku 30 kuanzia sasa.
Alifafanua mapungufu hayo
kuwa ni pamoja na leseni ambazo hazifanyiwi kazi, leseni ambazo hazijalipiwa
ada ya pango la mwaka, maombi ambayo hayajalipiwa ada ya maombi na maombi
yaliyokosa viambatisho muhimu kwa mujibu wa sheria.
Profesa Manya alitaja
mapungufu mengine kuwa ni pamoja na waombaji waliokidhi vigezo vya kupewa leseni
lakini hawajalipa ada ya maandalizi na wamiliki ambao leseni zao zimeshatolewa
lakini hazijachukuliwa.
Alifafanua kuwa mpaka sasa
leseni zaidi ya 134 za utafutaji na uchimbaji wa kati wa madini hazijachukuliwa
na zaidi ya maombi 450 ya leseni za utafutaji yana mapungufu.
Akielezea hatua
zitakazochukuliwa kwa kampuni au watu binafsi walioaminiwa na Serikali na
kupewa leseni lakini wameshindwa kutekeleza masharti ya leseni kwa mujibu wa
Sheria ya Madini, alisema leseni ambazo
hazijalipiwa ada ya pango kwa mwaka, leseni ambazo hazifanyiwi kazi na leseni
ambazo zimekwishatolewa lakini hazijachukuliwa zitaandikiwa hati ya makosa na
yasiporekebishwa zitafutwa kwa mujibu wa sheria.
Aidha alisema kuwa, maombi
yote ya leseni za utafutaji na uchimbaji wa kati yenye mapungufu yataondolewa
kwenye mfumo wa utoaji wa leseni ili waombaji wengine wenye sifa pamoja na
wachimbaji wadogo waweze kuomba maeneo hayo.
Aliendelea kusema kuwa,
maombi ambayo yamekidhi vigezo vya kupewa leseni lakini hayajalipiwa ada ya kuandalia
leseni yataondolewa kwenye mfumo ili waombaji wengine wenye sifa waweze kuomba
maeneo hayo.
Alisisitiza kuwa tangazo la
zabuni husika linapatikana katika tovuti ya Wizara ya Madini ambayo ni (www.madini.go.tz) Tume ya Madini (www.tumemadini.go.tz) magazeti ya Habari
Leo na Daily News ya tarehe 20 Desemba, 2019 pamoja na blogs na mitandao ya
kijamii.
No comments:
Post a Comment