Matokeo chanyA+ online




Friday, December 20, 2019

KONGAMANO LA TATU LA SIKU MBILI LA KIMATAIFA LA KISWAHILI LAFUNGULIWA ZANZIBAR

Balozi Seif akiangalia baadhi ya Vitabu vya Kiswahili na kuridhika na kazi kubwa ilivyofanywa na Magwiji wa Lugha ya Kiswahili kutoka pembe mbali mbali za Dunia.
Mzee Mwinjuma Kirobo kutoka Kikundi cha Wajasiriamali cha Tulikotoka kutoka Bweleo akimpatia maelezo Balozi Seif jinsi Kikundi hicho kinavyoendelea na uratibu wa kuhifadhi vitu vya Aslimu vilivyokuwa vikitumiwa na Waswahili wa enzi zilizopita.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akilifungua Kongamano la Tatu la Siku Mbili la Kimataifa la Kiswahili kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein hapo katika Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil Kikwajuni.

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa ZanzibarMabaraza, Taasisi pamoja na Wataalamu wanaoshughulikia Kiswahili wana wajibu wa kusimama kidete kuhakikisha kuwa Lugha ya Kiswahili inaendelezwa na kutumiwa katika usahihi wake kulingana na Utamaduni wa Waswahili kwa vile Lugha ni kipengele muhimu cha Utamaduni wa Jamii.
Washirika hao lazima waone fahari ya mafanikio ya Lugha ya Kiswahili kwamba sasa imekuwa sio Lugha ya Waswahili wazawa wachache peke yao bali imeshaenea kuwa Lugha ya Kimataifa yenye utambulisho wa kujivunia kama nembo ya Afrika.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein alitanabahisha hayo wakati akilifungua Kongamano la Tatu la Siku Mbili la Kimataifa la Kiswahili katika Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo katika Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil Kikwajuni.
Alisema hiyo ni hatua muhimu ya kupanda hadhi kwa Lugha ya Kiswahili jambo ambalo halitotokea kwa sadfa, bali litatokana  na dhamira ya dhati ya Watu wenye mapenzi na Lugha hii adhimu na wanaoishughulikia.
Mwenyekiti wa Baraza la Kiswahili Zanzibar {BAKIZA} Dr. Muhammed Seif Khatib akitoa salamu za kuwakaribisha Waswahili kutoka pembe zote za Dunia waliohudhuria Kongamano la Tatu la Kimataifa la Kiswahili hapo Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil.  
Waziri wa Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo Balozi Ali Aman Karume akimkaribisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kulifungua Kongamano hilo la Siku mbili la Kiswahili. 
Balozi Seif  pamoja na Viongozi wengine wa Kitaifa na Baraza la Kiswahili wakiwaonyesha Washiriki wa Kongamano wa Tatu la Kimataifa la Kiswahili nakala ya Kitabu akichokizindua kilichotungwa na Gwiji wa Kiswahili wa uandishi wa Vitabu Duniani Mzee Haji Gora Haji na kupewa jina la Shuwari.


Alisema Lugha ya Kiswahili kama zilivyo Lugha nyengine Duniani ina Utamaduni wake uliopevuka na kuimarika pamoja kusheheni masuala mbali mbali ya Mila, Desturi na Silka za Waswahili mambo ambayo ni rasilmali kubwa inayohitajika kuenziwa.
Dr. Shein alisema kutokana na mahitaji makubwa ya Lugha ya Kiswahili kukidhi kama daraja la mawasiliano katika shughuli mbali mbali za Kitaifa na Kimataifa, Lugha hii sasa imekuwa ni bidhaa inayouzika katika soko la Kimataifa kwa vile tayari hutumika kupitishia maafira tofauti.
Alieleza kwamba Wataalamu na watumiaji wa Lugha ya Kiswahili wanayo nafasi ya kuzitumia njia za kisasa za Teknolojia ya Mawasiliano, ili kuchangamkia fursa zilizopo za soko la Lugha hiyo kwa upande wa Fasihi na Isimu katika Mataifa mbali mbali Duniani kwa lengo la kujiongezea kipato.
Alifahamisha kwamba hadhi ya Lugha ya Kiswahili hivi sasa ni bidhaa muhimu katika kukuza Maendeleo ya Kiuchumi na Kiutamaduni Ulimwenguni. Hivyo inachopaswa kuzingatiwa kwa sasa ni jinsi gani itakavyopangwa Mikakati ya kuzitumia fursa zinazotokana na Kiswahili.
Balozi Seif na viongozi wengine wa Serikali wakikagua Vitabu mbali mbali vilivyoandikwa kwa Lugha ya Kiswahili na Waandishi Mahiri waliobobea kwenye Maonyesho ya Kongamano la Kimataifa la Kiswahili. 
Na Othman Khamis/Rashida Abdi wa OMPR, ZNZ

Rais wa Zanzibar alieleza kwa lengo la kuzidi kupiga hatua za kuiendeleza Lugha ya Kiswahili na kuweza kuzitumia fursa tofauti zinazozidi kujitokeza za kunufaika na Lugha hii adhimu, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekiagiza Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar {SUZA} kifanye maandalizi ya kuanzisha Skuli ya Tafsiri na Ukalimali.
Alisema hatua hiyo itawezesha kuandaliwa mapema Wataalamu waliobobea  wa fani za tafsiri na ukalimali wanaohitajika kwa wingi katika maendeleo mbali mbali ya Mawasiliano ikiwemo katika Mikutano ya Kimataifa ambako Lugha ya Kiswahili tayari inatambulika hivi sasa.
Dr. Shein alielezea matumaini yake kwamba jambo hilo kwa Zanzibar ni stahiki yake na linawezekana kutokana na uzoefu uliopo wa kuwasomesha Wageni Lugha ya Kiswahili kwa kipindi kirefu katika iliyokuwa Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni Zanzibar {TAKILUKI}.
“ Serikali pamoja na kuongeza vifaa na vivutio vyengine maalum vya kuwafanya wageni imeshakiagiza Chuo Kikuu cha SUZA kuiimarisha Skuli hiyo ya Kiswahili na Lugha za Kigeni kuwa Kitivo Kikuu cha kuifanya Zanzibar kuwa Center of Exicellence wanaotaka kujifunza lugha washawishike kujiunga”. Alisisitiza Dr. Shein.
Alisema kama lilivyowezekana suala la kuanzisha Shahada ya Uzamivu na Uzamili za Kiswahili jambo hili litawezekana kwa vile Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kukata pua, kuunga wajihi katika kulifanikisha suala hilo kama ilivyowahi kufanya katika kufanikisha masuala mengine yenye maslahi kwa Taifa.

No comments:

Post a Comment