Mratibu wa Mradi
katika kiwanda cha nyama na machinjio cha Tan Choice Dkt. Juma Mtei
akitoa maelezo kuhusu mashine za kuchinjia mifugo kwa Waziri wa Nchi
Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki alipotembelea
kuona namna kiwanda kilivyojipanga kuanza shughuli za uzalishaji wake
katika Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani.
Kiwanda cha
kuchakata nyama na machinjio ya mifugo cha Tan Choice kinatarajiwa
kuzalisha ajira 500 za kudumu katika fani mbalimbali nchini mara baada
ya kuanza kazi rasmi mapema Machi, 2020.
Hayo yamesemwa na
Msemaji wa kiwanda hicho Bw. Albert Kilalah wakati akiwasilisha taarifa
ya kiwanda kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia
masuala ya Uwekezaji nchini Mhe. Angellah Kairuki alipotembelea na
kukagua maendeleo ya ujenzi wa kiwanda pamoja na kusikiliza na kutatua
changamoto zilizowasilishwa za kiwanda hicho.
Waziri wa Nchi
Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki akihutubia wakati
wa mkutano wake na watendaji wa kiwanda cha kuchakata nyama cha Tan
Choice (hawapo pichani) alipotembelea kiwandani hapo Januari 17, 2020
Wilaya ya Kibaha mkoa wa Pwani.
Waziri Kairuki
alifanya ziara hiyo (Ijumaa tarehe 17 Januari, 2020) ambapo alipata
fursa za kukagua maeneo ya kiwanda hicho chenye uwezo wa kuchakata nyama
bora (organic meet) na kusema amevutiwa na kupongeza jitihada za
uwekezaji huo mkubwa.
“Nimefarijika
kuwa hadi sasa mmeweza kutoa ajira zaidi ya 300 na ni matarajio yenu
kutoa ajira 500 kiwanda kitakapoanza kazi mapema mwaka huu na
tutaendelea kuwaunga mkono ili kuwafikia wananchi kwa utoaji wa bidhaa
bora zenye uhakika,”alisema Waziri Kairuki.
Mkurugenzi Mkuu
wa kiwanda cha Tan Choice, Rashid Abdul akisema neno la ufunguzi wa
mkutano wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah
Kairuki alipotembelea kiwandnai hapo.
Waziri alieleza
kuwa huo ni uwekezaji mkubwa wenye tija ambapo hadi sasa umegharimu
zaidi ya Tshs bilioni 25, hivyo ni kiwanda cha mfano kwa nchi za Afrika
ya Kati na kuahidi kutoa ushirikiano ili kufikia malengo ya kiwanda
hicho.
Aidha Msemaji wa
Mradi huo alieleza uwepo wa kiwanda hicho ulizingatia mahitaji ya nyama
bora na mazingira rafiki ya uwekezaji yaliyopo nchini kwa kuzingatia
umuhimu wa wawekezaji na wafanyabiashara.
Msemaji wa
kiwanda cha kuchakata nyama cha Tan Choice Bw. Albert Kilalah akikabidhi
taarifa ya kiwanda hicho kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu
(Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki wakati wa ziara yake ya kikazi
kiwandani hapo.
“Bodi ya Tan
Choice ilivutiwa uwekezaji kwenye sekta ya nyama kutokana na uwepo wa
mazingira rafiki ya uwekezaji nchini chini ya Serikali ya Awamu ya Tano
na uwepo wa mifugo itayowezesha uendeshaji wa miradi huu na kukidhi soko
la ndani na nje ya nchi,” alisema Bw. Albert Kilalah
Alieleza kiwanda
hicho ni fursa kwa wafugaji na wafanyabiashara wa mifugo nchini ambapo
zaidi ya watu 10000 watanufaika kiuchumi kwa kuzingatia uhakika wa soko
la nyama na mazao yatokanayo na mifugo.
Sehemu ya
washiriki wa mkutano wakimsikiliza hotuba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki (hayupopichani) wakati wa
ziara yake katika kiwanda cha TAN CHOICE.
Alifafanua,
Kiwanda hicho kitakuwa cha pili kwa ukumbwa kwa nchi za Africa Mashariki
kikifuatiwa na kiwanda cha Ethiopia ambacho kina uwezo wa kuchinja
ng’ombe 3,000, kondoo na mbuzi 6,000 kuzalisha zaidi ya tani 300 kwa
siku.
“Kiwanda
kitakapokamilika kitakuwa kikubwa na bora cha aina yake katika ukanda wa
Afrika Mashariki na Kati na kitakuwa na uwezo wa kuchinja ng’ombe
1,000 na mbuzi na kondoo 4,500 kwa siku nyama na mazao mengine
yatakayozaliswa na kiwanda yatazingatia ubora na usalama,”alisema
Kilalah.
Mkuu wa Mkoa wa
Pwani Mhe. Evarist Ndikilo akizungumza jambo kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki alipomtembelea ofisi
kwake wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kutembelea maeneo ya
uwekezaji ikiwemo viwanda vilivyopo katika mkoa huo.
Alisema kuwa, Tan
Choice inatarajia kuuza nyama soko la nchi za Uarabuni Mashariki ya
Kati ikiwemo Falme za Kiarabu (UAE) na Saudi Arabia pamoja na masoko
yatakayo jitokeza ikiwemo China, Malaysia, Vietnam na Indonesia pamoja
kutumia fursa ya soko huru la kibiashara litakaloazishwa barani Afrika
na kuuza nyama hiyo.
Waziri wa Nchi
Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki akiwa katika
picha ya pamoja na Viongozi wa Serikalini pamoja na watendaji wa kiwanda
cha kuchakata nyama na machinjio ya TAN CHOICE mara baada ya kumaliza
ziara yake kiwandani hapo Januari 17, 2020.Kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya
ya Kibaha Mhe. Asupter Mshama na kushoto kwake ni Mkurugenzi Mkuu
kiwanda hicho Bw. Rashid Abdul.
Akihitimisha
taarifa hiyo aliomba Serikali kuendelea kuboresha barabara kutoka eneo
la kiwanda hadi Kongowe iboreshwe kwa viwango vya lami ili kurahisisha
usafirishaji wa mifugo kiwandani na pamoja na nyama zitakazozalishwa
kwenda uwanja wa ndege, bandarini na masoko ya ndani.
Aidha aliomba kuwe na uboreshwaji wa minada ili kuwe na uhakika wa upatikanaji wa wanyama wengi na wenye uhakika.
Mratibu wa Mradi
katika kiwanda cha Tan Choice Dkt. Juma Mtei akitoa maelezo ya kiwanda
cha kuchakata nyama cha Tan Choice kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki wakati wa ziara yake ya kikazi
kiwandani hapo,Januari 17, 2020.
Naye Mkuu wa
Wilaya ya Kibaha, Mhe. Asupter Mshama alishukuru wawekezaji katika
Wilaya yake, na kuwatoa shaka juu ya utatuzi wa changamoto walizonazo na
kuendelea kuunga mkono jitihada zao kwa kuhakikisha huduma muhimu
ikiwemo, nishati ya umeme, maji, barabara na mawasilino vinazingatiwa
ili kuwa na manufaa ya uzalishaji wa kiwanda.
No comments:
Post a Comment