Selikali imezipiga marufuku taasisi zote za Umma nchini
kujenga mifumo ya fedha ya kieletroniki bila ridhaa ya Wizara ya Fedha na Mipango na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA).
Agizo hilo limetolewa Jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa Wizara ya
Fedha na Mipango, Bw. Doto James, wakati akizundua Mfumo wa Malipo ya Serikali
kwa njia ya Kielektroniki (GePG) toleo la simu za mkononi (GePG App), hafla iliyowakutanisha
Wizara ya Fedha na Mipango na Idara, Wakala, Taasisi, Bodi, Mashirika ya Umma
yaliyo katika Kanda ya Kati.
“Baadhi
ya faida za Matumizi ya Mfumo huo ni kuongezeka
kwa uwazi na udhibiti katika ukusanyaji wa fedha za umma, kupata taarifa sahihi
na kwa wakati zinazohusu makusanyo na kuwa na viwango na utaratibu unaofanana
katika ukusanyaji wa fedha za umma kwa taasisi zote za umma”, alisema Bw. James.
Alisema faida nyingine ni pamoja na kuchochea ubunifu katika
ukusanyaji wa pesa za Serikali na sekta ya fedha kwa ujumla kwa kuweka
mazingira rafiki na ya usawa kwa wakusanyaji, kutoa huduma bora na rahisi ya
malipo ya fedha za umma hivyo kuchochea ongezeko la makusanyo na kufika haraka
katika akaunti kuu za makusanyo za taasisi.
“Kwa kutofanya usuluhishi wa miamala kwa wakati kunaweza
kusababisha upotevu wa fedha nyingi za Umma na pia kuwa na taarifa za fedha
zisizo sahihi, hivyo nawaagiza nyote kuhakikisha mnafanya usuluhishi wa miamala
inayopitia Mfumo wa GePG kwa usahihi na kwa wakati, na kufanyia kazi kwa wakati
changamoto mbalimbali zitokanazo na matokeo ya usuluhishi wa Miamala husika”,
alisisitiza Bw. James.
Aidha alimpongeza
Mkurugenzi wa Mifumo ya Usimamizi wa Fedha wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw.
John Sausi pamoja na timu yake ya wataalam wabobezi kwa kutengeneza Mfumo wa
Kieletroniki wa Kukusanya Mapato ya Serikali (GePG) sambamba na toleo la simu
za mkononi (GePG App) ambao umerahisisha ukusanyaji wa mapato ya Serikali
pamoja na kuwawezesha wadau kupata huduma kwa wakati.
Aliahidi kuwa Wizara yake itaendelea kuiwezesha Idara hiyo ili
iweze kutekeleza majukumu yake ya kubuni mifumo kama hiyo kwa faida ya Serikali
na wananchi kwa ujumla.
Aidha, Bw. James ambaye pia ndiye Mlipaji Mkuu wa Serikali,
alisema kuwa Wizara kupitia Idara ya Mifumo ya Usimamizi wa Fedha inaandaa
mfumo mwingine utakaotumika kwa ajili ya matumizi ya Serikali ujulikanao kwa
kifupi kama MUCE.
“Mfumo huu umeshaanza kufanyiwa majaribio kwenye taasisi chache
za umma na baadae utasambazwa kwenye taasisi zote na kwamba Mfumo huu utakuwa
mwarobaini wa matumizi yasiyo sahihi ya fedha za Umma”, aliongeza Bw. James.
Alisema Mfumo huo utakuwa suluhisho la matumizi yasiyofaa ya
umma na kuongeza kuwa watendaji wengi Serikalini hawataufurahia mfumo huo lakini
hilo haliihusu Serikali. Watajua wenyewe! Alisema huku washiriki wakiangua
kicheko ukumbini.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mifumo ya Fedha, wa Wizara ya
Fedha na Mipango, Bw. John Sausi, alisema kuwa kabla ya kuwa na Mfumo wa Malipo
kwa njia ya Kielektroniki (GePG) ilikua inafanyika miamala 10 kwa siku na baada
ya mfumo huo inafanyika miamala milioni moja kwa siku.
Alisema kuwa miongoni mwa mafanikio ni kuongezeka kwa Taasisi
zinazotumia Mfumo wa GePG, kutoka
taasisi 300 muda mfupi uliopita hadi
kufikia taasisi 620 hivi sasa.
Bw. Sausi alisema kuwa Mfumo wa GePG kwa njia ya mtandao wa simu
za mkononi uliozinduliwa utasaidia watumiaji kupata huduma mbalimbali kama vile
kununua umeme, kulipia Ankara mbalimbali zikiwemo za makosa ya usalama barabarani,
maji na nyingine nyingi ndani ya sekunde 30.
Ametoa wito kwa wananchi wanaotumia simu janja (android au IPA
App) kupakua application hiyo kupitia play store au App Store na kutafuta neno
GePG Tanzania tayari kwa matumizi yao ambayo amesema wananchi watafurahia
huduma hiyo.
Naye Mwakilishi wa Benki katika Mkutano huo, Bi Domina Tarimo na
Mwakilishi wa kampuni za Simu, Bw. Alafat Ibrahim, walisema kuwa Mfumo wa GePG
umezisaidia kwa kiasi kikubwa kurahisisha kazi zao, na kuboresha huduma kwa
wateja wao na wameipongeza Wizara ya Fedha na Mipango na Serikali kwa ujumla
kwa jitihada zake za kuhakikisha kuna mifumo imara ya fedha inayoongeza uwazi
na uwajibikaji.
No comments:
Post a Comment