Serikali inaendelea
na utekelezaji wa miradi mingi ya kuimarisha miundombinu katika sekta
mbalimbali ikiwemo mradi ya umeme (JN HPP-Julius Nyerere Hydropower project)
kwa gharama ya shilingi trilioni 6.5, Ujenzi wa Reli ya Kisasa SGR kwa gharama
ya shilingi trilioni 7 na miradi mingine ambayo itaweka mazingira wezeshi kwa
wananchi kufanya biashara na uwekezaji.
Mnamo Desemba 8,
2019, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli alizindua
ujenzi wa mradi mwingine mkubwa wa ujenzi wa meli kubwa ya abiria na mizigo ya
MV. Mwanza, ukarabati wa meli za MV. Victoria na MV. Butiama pamoja na ujenzi
wa chelezo katika lango la biashara na uchumi kanda za ziwa ambao utekelezaji
wake unaendelea vizuri na utakapokamilika utakuwa umegharimu zaidi ya shilingi
bilioni 153.7.
Meneja wa mradi
huo, Mhandisi Abel Gwanafyo ameeleza kuwa, meli kubwa ya “MV Mwanza, Hapa Kazi Tu” itakayogharimu shilingi bilioni 89.76
ambayo ujenzi wake unatekelezwa na kampuni ya ujenzi ya GAS ENTEC
wakishirikiana na KANG NAM kutoka Korea Kusini pamoja na SUMA JKT kutoka
Tanzania, itakuja kuwa mbadala ya Meli ya MV Bukoba ambayo ilizama miaka 23
ilipita.
Katika kampeni za uchaguzi mkuu wa 2015, Rais
wa Awamu ya Tano, Dkt John Pombe Magufuli aliwaahidi wananchi wa kanda ya ziwa
kuwa atajenga meli kubwa kuwaenzi waliokufa kwenye ajali hiyo lakini pia
kuimarisha usafirishaji katika ukanda huo wa Tanzania kwani kuna fursa nyingi
za biashara.
“Ni miaka 23,
tangu kuzama meli ya MV. Bukoba mwaka 1996, miaka mingi imepita, lakini pia
kuharibika kwa meli ya mizigo kumekuwa na tatizo kubwa kwa sekta ya usafarishaji
kwa wananchi wanaioshi kuzunguka ziwa Victoria na hivyo kuathiri shughuli za
uchumi na uzalishaji Kanda ya Ziwa”, Rais Dkt. John Magufuli.
Mradi huo mkubwa
utakwenda sambamba na miradi mingine ya ukarabati wa meli ya Mv Victoria
utaogharimu shilingi bilioni 22.71, Mv Butiama bilioni 4.9, ambazo ujenzi wake
unatekelezwa na kampuni ya ujenzi ya KTMI kutoka Korea Kusini huku ujenzi wa
chelezo utakaogharimu shilingi bilioni 36.4, unatekelezwa na kampuni ya Stx
Engine ikishirikiana na SAE Kyong kutoka Korea Kusini.
MV Mwanza Hapa Kazi Tu, itakuwa na urefu wa mita 92, na uwezo wa kubeba abiria 1,200, mizigo
tani 400, magari makubwa 3 na magari madogo 20, huku Mv Victoria ikibeba abiria
1,200, mizigo tani 200 na Mv Butiama abiria 200, tani 100, na kuwezesha zaidi
ya abiria 2,600 na tani 700 za mizigo kwa wakati mmoja hivyo kusadia kupunguza
adha ya usafiri na usafirishaji kwa abiria na mizigo katika ukanda huo wa ziwa.
“Ni wazi kuwa
utekelezaji wa miradi hii utakaogharimu shilingi bilioni 153.7 utasaidia sana
kutatua tatizo la usafiri na usafirishaji kwa wananchi wanaoishi kando ya ziwa
Victoria, siyo tu hapa nchini bali hata kwa jirani zetu Kenya na Uganda kwa
hiyo ni miradi ambayo ina manufaa kwa uchumi wetu”, amesema Rais Magufuli.
Aidha kukamilika
kwa mradi huu kutaondoa kwa kiasi kikubwa tatizo la usafiri kwa abiria katika
ukanda huo wa ziwa ikiwa ni pamoja na usafirishaji wa mizigo na mazao
mbalimbali ya biashara na kuzalisha ajira kwani meli hii itahitaji wafanyakazi
wa aina mbalimbali. Kwa upande wa nchi jirani za Kenya na Uganda , hii pia
itakuwa fursa kwao kusafirisha mazao ya biashara na chakula kupitia ziwa
Victoria badala ya kutegemea usafiri wa aina moja wa barabara au wa anga.
Katika uzinduzi wa ujenzi wa mradi huo ambao
utafungua ukanda wa kibiashara na kusaidia kukuza pato la taifa, Rais Magufuli
alieleza dhamira kubwa ya Serikali ya Awamu ya Tano kuwa ni kufanya mabadiliko
makubwa kwa kuleta miradi wezeshi kwa wananchi bila kutegemea misaada yenye masharti
lukuki na ufadhili.
Sekta hii ya
usafirishaji kwa njia ya maji ni muhimu sana na Serikali kupitia Mamlaka ya
Bandari Tanzani (TPA), pamoja na Shirika la Huduma za Meli imekuwa na usimamizi
madhubuti ili kukuza na kuimarisha sekta
hiyo ambayo ni nyenzo kubwa katika uchumi.
Kampuni ya Huduma
za meli iliyoanzishwa na Baba wa Taifa, Mwl. Julius Nyerere kwa sasa inafanya
kazi kubwa baada ya Rais Magufuli kuingia madarakani na kuelekeza nguvu katika
kuimarisha bandari nchini. Hapo awali ziwa Victoria lilikuwa meli 14 ikiwemo
meli ya utalii, lakini meli hiyo iliacha kufanya kazi kutokana na uongozi
mbovu, ikiwa ni pamoja na vitendo vya wizi na ubadhilifu wa mali za umma na hatimaye meli zote 14 ziliisha na kubaki
moja tu.
“Nawapongeza
Kampuni ya Huduma za Meli kwa kuboresha utendaji kazi katika kampuni hii, kwani
miaka ya nyuma hata mishahara mlikuwa hamuwezi kulipa wafanyakazi wenu, lakini
kwa sasa utendaji kazi uko vizuri na umeimarika ambapo mpaka sasa meli nne zipo
na zinafanya kazi. Meli hizo ni Mv Clarius, Mv Umoja, Mv Sangara na Mv Wimbi,
kwa hiyo ujenzi wa meli mpya na ukarabati wa meli hizi mbili utasaidia kukuza
huduma zenu”, alisema,Rais Magufuli.
Mamlaka ya
Bandari imekuwa ikiendelea na upanuzi na ujenzi wa bandari mbalimbali nchini
zikiwemo bandari ya Dar es Salaam, Mtwara, Tanga, Mwanza na bandari zake ndogondogo
za Kemendo, Bukoba, Kwemukwikwi na Nyamirembe kwa upande wa kanda ya ziwa.
Mhandisi,Gwanafyo ameeleza kuwa ujenzi wa meli
mpya “Mv Mwanza Hapa Kazi Tu” umefikia
asilimia 52 tofauti na mwezi Desemba 2019 ambapo ulikuwa asilimi 50, huku
ukarabati wa Mv Victoria ukiwa asilimia 75 badala ya 65, Mv Butiama asilimi 70
badala ya 60 huku ujenzi wa chelezo ukiwa ni asilimia 80 badala 68 za mwezi
Desemba 2019.
Miradi hiyo
imeweza kutoa fursa nyingi kwa wananchi wa mkoa wa Mwanza ikiwemo fursa za
biashara na ajira kwani mpaka sasa kuna ajira zaidi ya 1,000 na bado
zinaongezeka kwa kadri siku zinavyoongezeka.
Ujenzi wa meli
hii kubwa ni utekelezaji wa ahadi na kutimiza maono ya Baba wa Taifa Mwl.Julius
Nyerere aliyetaka kuwepo na meli kubwa katika ukanda huo wa kiuchumi wa
Tanzania, ambapo mwaka 1979, alisimamia kuundwa kwa meli ya MV Bukoba ambayo ilizama mwaka 1996 na kuleta ugumu wa usafiri
na usafirishaji katika ziwa Victoria ambalo ni tegemeo kwa wananchi wa kanda
hiyo pamoja na nchi jirani. Uamuzi wa Rais Magufuli wa kujenga meli hiyo kubwa ‘Mv Mwanza, Hapa Kazi Tu’ na kukarabati
meli nyingine unaonyesha jinsi alivyodhamiria kuyaishi na kuyatekeleza maono ya
Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere kwa vitendo.
Na.Paschal Dotto-MAELEZO
No comments:
Post a Comment