Matokeo chanyA+ online




Tuesday, January 14, 2020

RAIS DKT. MAGUFULI APOKEA HATI ZA UTAMBULISHO TOKA KWA MABALOZI WA ALGERIA, UJERUMANI NA QATAR

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akipokea Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Algeria nchini Mhe. Ahmed Djellal kwenye hafla liyofanyika Ikulu jijini Dar es salaam Jumanne Januari 14, 2020


Rais Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 14 Januari, 2020 amepokea hati za utambulisho za Mabalozi 3 walioteuliwa kuziwakilisha nchi za Ujerumani, Qatar na Algeria hapa nchini.
Mabalozi waliowasilisha hati hizo ni Mhe. Regine Hess – Balozi wa Jamhuri ya Ujerumani hapa nchini, Mhe. Hussein Bin Ahmed Mohamed Ibrahim Al-Homaid – Balozi wa Taifa la Qatar hapa nchini na Mhe. Ahmed Djellal – Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Algeria hapa nchini.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akipokea Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani nchini Mhe. Regina Hess kwenye hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es salaam  Jumanne Januari 14, 2020

Akizungumza na Mabalozi hao, Mhe. Rais Magufuli amewakaribisha hapa nchini na kuwahakikishia kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inayo dhamira ya dhati ya kuukuza na kuuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano mzuri na wa kihistoria uliopo kati ya Tanzania na nchi hizo.
Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa Mabalozi hao kuwahamasisha wafanyabiashara na wawekezaji mbalimbali kutoka nchini mwao kuja kuwekeza hapa nchini katika sekta mbalimbali hasa kilimo, mafuta, gesi, viwanda na madini kwa kuwa Tanzania imejaaliwa kuwa na rasilimali za kutosha katika sekta hizo ambazo zinahitaji ushirikiano wa pamoja katika uwekezaji.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akipokea Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule Taifa la Qatar nchini Mhe. Hussein Bin Ahmed Mohamed Ibrahim Al-Homaid katika hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es salaam  Jumanne Januari 14, 2020

Amewaomba Mabalozi hao kufikisha shukrani zake kwa viongozi wa nchi zao na kuwakaribisha kutembelea Tanzania kwa ziara rasmi ama kutembelea vivutio vingi vya utalii vilivyopo.
Kwa upande wao, Mabalozi hao wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kukubali kuwapokea na katika kipindi cha uwakilishi wao wameahidi kufanya juhudi za kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano hasa katika masuala ya kiuchumi ambayo Serikali ya Awamu ya Tano inayapa kipaumbele.

No comments:

Post a Comment