Rais Magufuli amesema miaka 4 ya tangu Serikali ya Awamu ya
Tano iingie madarakani Tanzania imepiga hatua kubwa katika kutekeleza Dira ya
Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025, Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka
2015 – 2020, mipango ya kimataifa na kikanda na Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa
Miaka 5 (2016/17 – 2020/21)
iliyolenga kujenga uchumi wa viwanda utakaochochea mageuzi ya kiuchumi na
maendeleo ya watu.
Rais
Dkt. John Magufuli amesema hayo tarehe 21 Januari, 2020 katika hafla ya kuukaribisha
Mwaka Mpya aliyowaandalia Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa (Sherry Party)
na kufanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Rais ametaja
baada ya mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kulinda na kudumisha amani na usalama wa nchi,
kuimarisha Muungano ambao Aprili 2020 utatimiza miaka 56, ukuaji mzuri wa
uchumi wa wastani wa asilimia 7, kudhibiti mfumuko wa bei hadi kufikia asilimia
3.5 na kuongeza akiba ya fedha za kigeni kutoka Dola za Marekani Bilioni 4.123
hadi kufikia Dola za Marekani 5.579 zinazotosheleza kuagiza bidhaa na huduma
kwa kipindi kisichopungua miezi 6.3.
Kiongozi wa Mabalozi (Dean of Diplomatic Corps) Mhe. Ahamada El Badaoui Mohamed Fakih akizungumza |
Mafanikio
mengine ya kiuchumi ni kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato kutoka wastani wa
shilingi Bilioni 850 kwa mwezi hadi kufikia shilingi Trilioni 1.5 (ambapo Desemba 2019 ilifikia shilingi
Trilioni 1.9), kuvutia uwekezaji wenye thamani ya
shilingi Trilioni 30 uliozalisha ajira laki 1, kuogeza biashara ya nje kutoka
shilingi Trilioni 11.5 hadi kufikia shilingi Trilioni 16.6, kuongeza uzalishaji
wa mazao ya biashara kutoka tani 796,512 hadi kufikia tani 1,141,774 (ongezeko la asilimia 43.3)
na kujenga viwanda vipya 4,877.
Aidha,
katika kipindi hicho mauzo ya dhahabu nje ya nchi yameongezeka kutoka Dola za
Marekani Bilioni 1.469 hadi kufikia Bilioni 1.743, mapato ya Serikali kutokana
na madini yameongezeka kutoka shilingi Bilioni 168 hadi kufikia shilingi
Bilioni 346, idadi ya watalii imeongezeka kutoka watalii Milioni 1.1 hadi
kufikia Milioni 1.5 na mapato yatokanayo na utalii yameongezeka kutoka Dola za
Marekani Bilioni 1.9 hadi kufikia Bilioni 2.488.
Rais Magufuli ameongeza kuwa katika kipindi hicho Serikali imetekeleza miradi
mikubwa ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa (standard gauge railway)
kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma utakaogharimu zaidi ya shilingi Trilioni 7,
ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere litakalozalisha megawati 2,115 za umeme utakaogharimu
shilingi Trilioni 6.5, ujenzi wa kilometa 2,500 za barabara za lami na nyingine
2,400 zikiendelea kujengwa, kilometa 7,087 la barabara za lami zikiwa katika
maandalizi ya kuanza kujenzi na kukamilisha ujenzi wa madaraja makubwa 8.
Miradi
mingine ni kufufua reli ya Dar es Salaam – Tanga – Moshi iliyokuwa haitoi
huduma tangu miaka zaidi ya 20 iliyopita, kupanua bandari za Dar es Salaam,
Mtwara na Tanga, kukarabati meli 7 katika maziwa makuu, kukamilisha ujenzi wa
jengo la 3 la abiria katika uwanja wa ndege wa Julius Nyerere Jijini Dar es
Salaam (Terminal III),
kujenga viwanja vya ndege 11, kununua rada 4, na kufufua Shirika la Ndege
Tanzania (ATCL) baada ya kununua ndege mpya 11.
Kwa
upande wa huduma za kijamii amesema mbali na kujenga Bwawa la Mwalimu Nyerere,
Serikali imejenga njia ya umeme ya Iringa – Shinyanga, Makambako – Songea na
Lindi – Mtwara, kupeleka umeme vijijini ambapo idadi ya vijiji vilivyofikiwa na
umeme imeongezeka kutoka 2,018 hadi kufikia 8,587, kujenga vituo vya afya 352 na
Hospitali za Wilaya 69, kuajiri watumishi wa afya 8,000 na kuongeza bajeti ya
dawa na vifaa tiba kutoka shilingi Bilioni 31 hadi kufikia shilingi Bilioni 270
kwa mwaka.
Amebainisha
kuwa Serikali inatoa elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari ambapo
imeshatumia shilingi Trilioni 1, mikopo ya elimu ya juu imeongezeka kutoka
shilingi Bilioni 341 hadi kufikia shilingi Bilioni 450, imetekeleza miradi ya
maji yenye thamani ya shilingi Trilioni 3 na hivyo kuongeza upatikanaji wa maji
kutoka wastani wa asilimia 56 hadi kufikia asilimia 71, kuongeza mapambano
dhidi ya rushwa na Serikali kuhamia Dodoma.
Mhe.
Rais Magufuli amesema kwa kuongozwa na sera ya diplomasia ya uchumi, Tanzania
imeendeleza na kukuza zaidi uhusiano wake na nchi mbalimbali duniani ambapo
pamoja na kufanya ziara katika nchi mbalimbali, Balozi mpya 7 zimefunguliwa na
kushiriki katika shughuli na mipango mbalimbali ya kimataifa ikiwemo ulinzi wa
amani ambapo kwa sasa askari 2,297 wa Tanzania wapo katika ulinzi wa amani
katika nchi mbalimbali.
Baadhi ya Mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini, Waakilishi wa Mashirika ya kimataifa katika Sherehe za Mwaka mpya 2020 kwa Mabalozi hao (Diplomatic Sherry Party) |
Ameahidi
kuwa katika mwaka 2020 Serikali imejipanga kuendelea kutekeleza Mpango wa
Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, kudumisha amani na usalama, kukuza zaidi
uchumi, kuimarisha akiba ya fedha za kigeni, kuongeza ukusanyaji wa mapato,
kukuza sekta kuu za uzalishaji yaani kilimo, viwanda, ujenzi, madini na utalii
pamoja na kuboresha mazingira ya kufanyia biashara ambapo amewaomba Mabalozi
hao kuwashawishi wafanyabiashara wa nchi zao kuja kuwekeza nchini Tanzania.
Pia,
amewahakikishia kuwa katika mwaka 2020 ambapo Tanzania inafanya Uchaguzi Mkuu,
Serikali imejipanga kuhakikisha unafanyika kwa misingi ya kidemokrasia na
katika mazingira ya amani, uhuru na haki, na amezikaribisha nchi na taasisi
mbalimbali kuja kuangalia jinsi Tanzania ilivyokomaa kidemokrasia pindi wakati
ukifika.
Ameahidi
kuwa Tanzania, itaendelea kukuza ujirani mwema, kushirikiana na nchi mbalimbali
na kutekeleza majukumu ya kimataifa ikiwemo kuwahudumia wakimbizi na
kuwarejesha makwao kwa hiari, lakini ameeleza kusikitishwa na hujuma na
propaganda zinafanyika kwa lengo la kukwamisha zoezi hilo.
Akizungumza
kwa niaba ya Mabalozi hao, Kiongozi wa Mabalozi (Dean
of Diplomatic Corps) Mhe. Ahamada El Badaoui Mohamed
Fakih amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa uongozi mzuri aliouonesha katika kipindi
cha miaka minne ambapo miradi mikubwa ya maendeleo imetekelezwa, kukua kwa
uchumi, ustawi wa watu na ameahidi kuwa Mabalozi wataendelea kutoa ushirikiano
wowote utakaohitajika.
Tuna mshukuru Mungu,katuwezesha kupata Kiongozi wa nchi aliye Imara,Shupavu na Mchapa kazi hodari katika Serikali ya Awamu ya Tano.Rais Magufuli Ni Mzalendo wa kweli anayo nia thabiti kuitumikia nchi yetu Tanzania. Amen
ReplyDelete