Matokeo chanyA+ online




Wednesday, February 26, 2020

TANESCO WATAKIWA KUHAMIA KWENYE MAJENGO YAO

Taswira ya jengo la Ofisi za Shirika la Umeme Tanzania, Wilaya ya Chato linalojengwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA). Taswira hii ilichukuliwa Februari 25, 2020 wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani).
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani ametoa maagizo kwa uongozi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kuhakikisha wanahamisha Ofisi zao zilizo katika majengo ya kupanga na kuhamia katika majengo yao yanayojengwa sehemu mbalimbali nchini.

Dkt Kalemani alitoa maagizo hayo Februari 25 mwaka huu baada ya kutembelea eneo zinapojengwa ofisi za TANESCO wilayani Chato, Mkoa wa Geita ambapo alisisitiza kuwa, mwisho wa kutekeleza agizo hilo ni Aprili 31, 2020.
 

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (wa pili-kushoto), akitoa maelekezo kwa Wakandarasi wanaosimamia ujenzi wa Jengo la Ofisi za Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Wilaya ya Chato, alipotembelea kujionea maendeleo yake, Februari 25 mwaka huu.
Alisema lengo la kujenga Ofisi hizo ni kusogeza huduma kwa wateja ili waweze kuhudumiwa kwa wakati pamoja na kuwapunguzia kero ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma.

“Mheshimiwa Rais ametuelekeza tusogeze huduma kwa wananchi. Nasi kama Wizara, tumejipanga vizuri kupitia TANESCO kutekeleza maagizo hayo.”

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (wa tatu-kulia), akijadiliana jambo na Msimamizi wa Ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), wilayani Chato, Mhandisi Gladys Jefta kutoka Wakala wa Majengo Tanzania (wa tatu-kushoto). Waziri alizuru eneo hilo kujionea maendeleo ya ujenzi huo, Februari 25 mwaka huu.
Akielezea zaidi kuhusu manufaa ya ujenzi husika hususan kwa wilaya ya Chato, Dkt Kalemani alisema kabla ya ujenzi, wananchi walikuwa wanalazimika kufuata huduma Geita na Biharamulo.

Alisema, jengo hilo litakapokamilika, litahudumia wananchi wa Chato na maeneo  jirani hususani yanaopakana nayo, ambayo ni pamoja na Biharamulo, Ngara na Bukombe.
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (aliyeinua mikono-kulia), akitoa maelekezo kwa wakandarasi wanaosimamia ujenzi wa Jengo la Ofisi za Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), alipotembelea eneo hilo, Februari 25 mwaka huu.
Kuhusu Mkandarasi anayejenga jengo hilo, Waziri alieleza kuwa ni Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), ambapo baada ya kufanya ziara hiyo alimwelekeza kufanya kazi usiku na mchana pamoja na kuongeza idadi ya vibarua ili akamilishe kazi husika ifikapo Aprili mwaka huu badala ya Juni kama ilivyo kwenye mkataba.

Akizungumzia uamuzi wa serikali kuitaka TANESCO kuondoka kwenye majengo ya kupanga, Waziri alisema utasaidia kuokoa fedha nyingi za shirika zilizokuwa zikitumika kulipia kodi lakini pia itawezesha shirika kumiliki mali zake ambazo zinaweza kutumika hata katika mikopo kwa ajili ya uendeshaji wake.


Mafundi wakiendelea na kazi ya ujenzi wa Jengo la Ofisi za Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), wilayani Chato, wakati Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani) alipotembelea eneo hilo kujionea maendeleo yake Februari 25, mwaka huu.
  
Veronica Simba – Chato

Ujenzi wa majengo mbalimbali ya Ofisi za TANESCO unaendelea nchini kote hususan katika maeneo ambayo shirika hilo lilikuwa limepanga katika majengo ya watu binafsi.

Imeelezwa kuwa idadi ya majengo hayo ya TANESCO yanayoendelea kujengwa inafikia 42 nchi nzima.
 

No comments:

Post a Comment