Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mwenyekiti wa Kamati ya Maafisa
Waandamizi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Balozi Kanali
Wilbert Ibuge amefungua kikao cha Maafisa Waandamizi chenye jukumu la kundaa
ajenda za mkutano wa Baraza la Mawaziri utakaofanyika tarehe 18, Machi mwaka
huu Jijini Dar es Salaam,Tanzania, ambacho kimefanyika kutokana na maendeleo ya
teknolojia ya Habari na Mawasiliano TEHAMA –ICT kwa nchi za SADC.
Akizungumza katika mkutano huo
ambao unafanyika kwa Video Coferencing,
Balozi Ibuge amesema kuwa kikao hicho kitajadili ajenda mbalimbali zikiwemo
Taarifa ya Maandalizi ya Dira ya SADC ya mwaka 2050, Mpango Mkakati wa
Maendeleo wa SADC 2020-2030, Maadhimisho ya miaka 40 ya SADC tangu kuanzishwa
kwake mwaka 1980, Utekelezaji wa maazimio ya vikao vilivyopita, Hali ya
michango na kifedha kwa ujumla ya SADC na Kupokea taarifa ya ukaguzi wa
shughuli mbalimbali za Sekretariati ya SADC.
"Kikao hicho ambacho
kinafanyika kwa njia ya Video
Conferencing kufuatia ushauri uliotolewa na Mawaziri wa Afya wa Nchi za
SADC walipofanya Mkutano wa dharura kufuatia mlipuko wa Ugonjwa wa Virusi vya
Corona (Covid-19), uliofanyika Jijini Dar es Salaam Machi 9 2020, na tutakuwa
na ajenda chache, nawasihi tuendelee kufuatilia na kutekeleza yale yote ambayo
tumeyaazimia", amesema Balozi Ibuge.
Pamoja na hayo Balozi Ibuge amebainisha
kuwa kuna uwezekano wa Maafisa Waandamizi wa Nchi hizo za ukanda wa Kusini Mwa
Afrika (SADC), kukutana mwezi Juni 2020
iwapo hali ya sasa ya mlipuko wa ugonjwa wa Corona (Covid-19, itakuwa
imebadilika ili kujadili kwa kina ajenda zilizosalia na zingine
zitakazopendekezwa.
Mkutano huo ambao umeendeshwa kwa
mara ya kwanza kwa kutumia njia ya Mtandao yaani Video conferencing kwa nchi za
SADC, umethibitisha kukua kwa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)-ICT
na itaendelea kuimarishwa zaidi kwa Nchi hizi ili kuepuka kuwepo kwa taharuki
ya milipuko mbalimbali au adha ambazo zitasababisha kuahirishwa kwa mikutano
hiyo.
Aidha, amewataka wananchi wanachama
kuendelea kuchukua tahadhari kujikinga na ugonjwa wa Corona ili kuepusha
kusambaa katika nchi wanachama.
“Naomba nitumie fursa hii
kuwaomba na kuwasihi nchi wanachama kuendelea kujinga na maambukizi ya Covid-19
na kushikamana kwa umoja wetu kupunguza kasi ya maambukizi na hatimaye kuondoa
kabisa katika sura ya dunia”, Alisema Balozi Ibuge.





No comments:
Post a Comment