Matokeo chanyA+ online




Monday, March 16, 2020

WAZIRI KALEMANI AKERWA NGUZO ZA UMEME KUTOSIMIKWA

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (katikati), akimwagiza Mkandarasi kutoka Kampuni ya Namis Corporate Ltd), anayetekeleza mradi wa Umeme wa Peri-Urban katika Mtaa wa Bombambili, wilayani Ilala, mkoani Dar es Salaam, kuhakikisha anawaunganishia umeme wananchi wote waliolipia ifikapo mwisho wa mwezi huu (Machi, 2020). Alitoa maagizo hayo Machi 12 mwaka huu, akiwa katika ziara ya kazi.

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani ameonesha kukerwa na tabia ya wakandarasi wanaorundika nguzo za umeme katika maeneo mbalimbali kwa muda mrefu pasipo kuzisimika ili kuwaunganishia umeme wananchi.
Hali hiyo ilidhihirika Machi 12 mwaka huu aliposhuhudia rundo la nguzo zikiwa chini katika mtaa wa Viwege, Kata ya Majohe, wilayani Ilala, Mkoa wa Dar es Salaam, akiwa katika ziara ya kazi.
Kufuatia hali hiyo, Dkt Kalemani alimwagiza Mkandarasi anayetekeleza mradi wa umeme pembezoni mwa miji (Peri-Urban) katika eneo hilo (kampuni ya Namis Corporate Ltd) kuziondoa nguzo hizo mara moja na kuzisimika kisha kuwaunganishia umeme wananchi husika.
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (mwenye miwani-kulia), akimwagiza Mkandarasi kutoka Kampuni ya Namis Corporate Ltd), anayetekeleza mradi wa Umeme wa Peri-Urban katika Mtaa wa Viwege, Kata ya Majohe, wilayani Ilala, mkoani Dar es Salaam, kuziondoa nguzo zilizorundikwa chini na kuzisimika mara moja kisha awaunganishie wananchi husika umeme. Alitoa maagizo hayo Machi 12 mwaka huu akiwa katika ziara ya kazi.
“Asipotekeleza agizo langu kufikia kesho asubuhi, nawaomba Diwani na Mwenyekiti wa Mtaa mnipigie simu na kunijulisha ili nimchukulie hatua mara moja,” alisisitiza Waziri.
Aidha, alisema agizo hilo liwafikie wakandarasi wote wanaotekeleza miradi mbalimbali ya umeme nchini kote kwamba hawatakiwi kurundika nguzo chini pasipo sababu ya msingi, wakati wananchi wakiendelea kulalamika kutounganishiwa huduma hiyo kwa wakati.
Sambamba na agizo hilo, Waziri pia alimwagiza Mkandarasi huyo kuhakikisha anawaunganishia umeme wananchi wote waliolipia huduma hiyo katika maeneo anakotekeleza mradi yakihusisha Kivule Bombambili, Viwege, Majohe na Dondwe kabla ya mwisho wa mwezi huu wa Machi, 2020 vinginevyo hatua kali za kimkataba zitachukuliwa dhidi yake.
 

Mafundi wakifunga Mashine Umba (Transfoma) katika eneo la Dondwe, wilayani Mkuranga, Mkoa wa Pwani, wakati Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani na Ujumbe wake, walipotembelea eneo hilo kujionea maendeleo ya kazi husika, Machi 12 mwaka huu.

“Nawaahidi mimi mwenyewe nitarudi hapa ifikapo mwisho wa mwezi ili kujiridhisha endapo maagizo yangu yametekelezwa. Ikitokea nikashindwa kuja mimi, nitamtuma mwakilishi aje kukagua na kuniletea mrejesho.”
Akiwa katika ziara hiyo ya siku moja, Waziri alikataa kuwasha umeme katika Mtaa wa Bombambili kutokana na idadi ndogo ya wateja waliounganishwa na kueleza kuwa atarudi kufanya kazi hiyo baada ya mkandarasi kutekeleza maagizo yake ya kuwaunganishia umeme wateja wote watakaokuwa wamelipia ndani ya kipindi cha mwezi mmoja.
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (mwenye miwani-mbele), akikagua utekelezaji wa Mradi wa Umeme wa Peri-Urban katika Mtaa wa Bombambili, wilayani Ilala, Mkoa wa Dar es Salaam, akiwa katika ziara ya kazi, Machi 12 mwaka huu.


Veronica Simba – Dar es Salaam
Kufuatia utekelezaji duni wa mradi husika katika maeneo hayo, Waziri aliagiza Fundi Mchundo kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), anayesimamia mradi huo katika maeneo husika, kuondolewa katika nafasi hiyo na ateuliwe mwingine mara moja.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Diwani wa Kata ya Tengerea, Shabani Manda, alimshukuru Waziri kwa kufanya ziara hiyo pamoja na maagizo aliyoyatoa akisema anaamini wananchi wa maeneo hayo watanufaika na huduma hiyo ya umeme kwa kuanzisha biashara mbalimbali zitakazowasaidia kuwainua kiuchumi.

Katika ziara hiyo, Waziri alifuatana na viongozi na wataalamu mbalimbali kutoka wizarani, TANESCO na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), akiwemo Kamishna Msaidizi wa Umeme, Mhandisi Innocent Luoga.

No comments:

Post a Comment