Na
Mwandishi Wetu, MAELEZO
Azimio namba 64/292 la mwaka 2010
la Umoja wa Mataifa linatamka kuwa huduma ya maji na usafi wa mazingira ni haki
ya msingi ya binadamu na pia ni hitaji muhimu kwa maisha ya viumbe hai na
shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Uwepo wa rasilimali za maji
za kutosha, miundombinu ya usambazaji
maji na usafi wa mazingira, na uwezo wa kiuchumi wa kuwekeza na kuendesha
huduma za maji ni masuala ya msingi na muhimu katika kufikia lengo hilo.
Katika kutekeleza Sera ya 9 Maji
ya Taifa ya mwaka 2002, Wizara ya Maji ina jukumu la kuhakiki ubora na usalama
wa maji katika vyanzo vya maji na mitandao ya kusambaza maji kwa lengo la kulinda
afya za wananchi na mazingira.
Malengo ya Serikali ni kuboresha
hali ya upatikanaji wa huduma ya maji katika Miji Mikuu ya Mikoa kufikia
asilimia 95; na Miji Mikuu ya Wilaya, Miji Midogo na Miradi ya Kitaifa kufikia
asilimia 90 ifikapo mwaka 2020. Kwa upande wa huduma ya uondoaji wa majitaka,
lengo la Serikali ni kuongeza huduma hiyo kufikia asilimia 30 ifikapo mwaka
2020.
Hadi mwezi Aprili 2019, hali ya
upatikanaji wa huduma ya maji katika maeneo yanayohudumiwa na Mamlaka za
Majisafi na Usafi wa Mazingira katika Miji Mikuu ya Mikoa ni asilimia 80 na kwa
Miji Mikuu ya Wilaya, Miji Midogo na Miradi ya Kitaifa upatikanaji wa huduma
hiyo ni asilimia 64.
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa
Mazingira Lindi (LUWASA) inatekeleza Mpango
wa Uboreshaji wa Huduma ya Maji katika Mji wa Lindi (Mradi wa Maji Ng’apa)
unaolenga kutoa huduma ya majisafi kwa wakazi wote waishio eneo la Manispaa ya
Lindi na kuondoa changamoto iliyopo ya wananchi hao hulazimika kufuata
maji umbali mrefu kupitia Virula(Vioski).
Akizungumza
katika mahojiano maalum na Maafisa Habari wa Idara ya Habari (MAELEZO)
waliofanya ziara ya kutembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali
Mkoani Lindi karibuni, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa
Mazingira Lindi (LUWASA), Mhandisi Juma Sudi anasema anasema mradi huo
umekamilika kwa asilimia 92 na hali ya upatikanaji wa huduma ya maji katika Mji
wa Lindi ni asilimia 75 kwa sasa.
Mhandisi
Sudi anasema mradi huo ulioanza miaka miwili ulioanza mwaka 2013 na kutarajiwa
kukamilika mwaka 2015, una jumla ya visima saba vinavyozalisha maji wastani wa
mita za ujazo 7500 kwa siku, huku mahitaji halisi ya huduma ya maji katika
Manispaa ya Lindi ni wastani wa mita za ujazo 5000.
Alisema
mwezi Februari mwaka huu, Serikali ilitoa kiasi cha Tsh. Bilioni 32 kwa ajili
ya kukamilisha hatua mbalimbali zilizosalia katika mradi wa maji wa Ng’apa na
mkandarasi mpya wa mradi huo kampuni ya Shanx Corporation Company Ltd Ltd
tayari ameanza kazi hiyo ambayo inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Mwezi Julai
mwaka huu.
‘’Serikali
imeweka fedha nyingi sana katika mradi huu,ni uwekezaji mkubwa unaleta maji
katika maeneo yote ya Mji, tunamshukuru sana Rais Dkt, John Magufuli kwa kutoa
fedha hizi amefanya maamuzi magumu, sisi LUWASA tumejipanga kuhakikisha
tunapeleka huduma ya maji katika maeneo yote ya mjini’’ alisema Mhandisi Sudi.
Aidha
Mhandisi Sudi anasema kuwa katika kuhakikisha kuwa tatizo la huduma ya maji katika
Mji wa Lindi linatatuliwa kwa haraka, Serikali kupitia Wizara ya Maji imetoa
kiasi cha Tsh Bilioni 2.9 kwa ajili ya kujenga mtandao wa mabomba katika Mji wa
Lindi ili kuhakikisha kuwa wakazi wote wanapata huduma ya maji wakiwa majumbani
kwao.
‘’Mwanzo
kabisa wananchi wa Manispaa ya Lindi walikuwa wakipata huduma ya maji kutoka
katika chanzo cha kitunda ambacho kipo ng’ambo ya bahari ambao ulikuwa
ukizalisha wastani wa mita za ujazo 2000 kwa siku na hata hivyo hakuweza
kukidhi mahitaji, hivyo kukamilika kwa mradi huu wa Ng’apa utakuwa mkombozi kwa
wananchi wa Manispaa ya Lindi’’ alisema Mhandisi Sudi.
Anaongeza
kuwa moja ya kazi inayofanywa na mkandarasi mpya kwa sasa ni pamoja na
kuhakikisha anakamilisha kuweka mfumo katika mtambo ili kusukuma maji katika
visima vyote vilivyopo umbali wa kilometa 13 kutoka katika chanzo cha Ng’apa
pamoja na kukamilisha kazi ndogondogo zilizosalia katika mradi huo.
Kwa
upande wake Bi Amina Ally Mkazi wa Kilimahewa Manispaa ya Lindi, aliipongeza
Serikali ya Awamu ya Tano kwani kwa sasa wameokoka na matatizo ya ukosefu wa
huduma ya maji katika maeneo yao kwani hapo awali walikuwa wakitembea umbali
mrefu kwa ajili ya kutafuta maji.
‘’Tunaishukuru
Serikali kwani imetutua ndoo kichwani sisi akina Mama, kwa sasa Maji yanapatikana
katika maeneo yetu hatufuatani tena na akina Baba kwa ajili ya kutupeleka
kuchota maji, ambayo yaliyokuwa yakipatikana maeneo ya porini, ambako kulikuwa
na vitisho mbalimbali kwa sisi akina mama’’ anasema Amina.
Anaongeza
kuwa kwa sasa afya zao zimeimarika kwani hawabebi mizigo mizito kichwani ya
ndoo walizokuwa wakisafiri nazo kwa umbali mrefu, kwani Serikali imerahisisha
kwa kiasi kikubwa kwa kufunga mtandao wa mabomba ambayo yamerahisisha huduma ya
upatikanaji wa maji kwa wananchi wa Kilimahewa, ambao jiografia yakekwa kiasi
imetawaliwa na milima mingi.
Aidha
anasema kuwa hali ya upatikanaji wa huduma ya maji katika eneo lao imekuwa
nzuri kwani virula (vioski) vilivyofungwa katika sehemu ya eneo la Kilimahewa
vipo karibu na makazi ya wananchi na maji hayo ni safi na salama kwa matumizi
mbalimbali ya nyumbani.
Naye
Bi. Zubeda Hamadi, Mkazi wa Kilimahewa anasema akina Mama wa eneo la Kilimahewa
wanaipongeza Serikali ya Awamu kwa mageuzi makubwa inayoendelea kuyafanya
katika utoaji wa huduma za kijamii ikiwemo maji, ambapo huko nyuma walikuwa
wakitembea umbali mrefu kutafuta maji, ambayo hayakuwa yakikidhi mahitaji ya
nyumbani.
‘’Linapokuja
suala la maji, sisi akina Mama tumekuwa tukipata shida sana na kutaabika,
lakini tunamshukuru Rais Magufuli na Serikali kwa ujumla kutuletea maji sasa
hivi maji yanatoka kwa wakati, yapo safi na salama kwa matumizi’’ alisema Bi.
Zubeda.
Bi. Elizabeth
Amosi mkazi wa mapoteni Manispaa ya Lindi, anasema akina mama na familia nyingi
sasa zina furaha, huduma ya maji imeokoa ndoa za familia nyingi kwani wanaume
wengi walikuwa wakigombana na wake zao kutokana na kuchukua muda mrefu wa
kwenda na kurudi majumbani wakati wa zoezi la kutafuta maji.
‘’Waume
zetu walikuwa na wivu sana ni jambo gumu sana kumwambia mume umetumia masaa 2-3
kwa ajili ya kwenda kutafuta maji katika umbali wa karibu kilometa 2-3 kutoka
katika majumba yetu, hayo ndio yalikuwa maisha yetu, lakini kwa sasa shida na
matatizo hayo yamekwisha’’ alisema Bi. Elizabeth.
Usimamizi
madhubuti wa rasilimali za maji unahitaji ushirikiano wa wananchi na wadau
mbalimbali ambao ndio watumia maji na wasimamizi wa kwanza wa rasilimali hizo
ikiwa ni mkakati na jitihada za kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji nchini.
No comments:
Post a Comment