Matokeo chanyA+ online




Friday, April 24, 2020

RAIA WA NIGERIA NA WATANZANIA WAWILI WALIOKAMATWA NA KILO 268.50 ZA DAWA ZA KULEVYA AINA YA HEROIN WAMEFIKISHWA LEO KATIKA MAHAKAMA YA HAKIMU MKAZI KISUTU

Washtakiwa, David Chukwu raia wa Nigeria, Isso Lupembe, wa Mbezi Luis na Allistair Mbele  wakitolewa katika chumba cha mahabusu cha mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu tayari kwa kupelekwa mahabusu katika gereza la Segerea baada ya kesi ya kusafirisha dawa za kulevya inayowakabili kuahirishwa.

Raia wa Nigeria, David Chukwu 38 Mkazi wa Masaki na wenzake wawili raia wa Tanzania waliokamatwa na Dawa za kulevya aina ya Heroin kilogramu 268.50, wamefikishwa leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na shtaka la kusafirisha dawa za
kulevya na kutakatisha zaidi ya sh. Milioni 150.

Mbali na Chukwu washtakiwa wengine ni Isso Lupembe 49 mkazi wa Mbezi Luis na Allistair Mbele 38 anayeishi Mbezi Kibanda cha Mkaa. Katika hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani hapo na mawakili wa serikali waandamizi, Veronika Matikila, na Wankyo Simon pamoja na wakili wa serikali Batlida Mushi mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Geoffrey Issaya washtakiwa katika kosa la kwanza wanashtakiwa kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya.
Washtakiwa David Chukwu (38), raia wa Nigeria, (kushoto)  Isso Lupembe (49) (wa kwanza kulia) mkazi wa Mbezi Luis na Allistair Mbele (38) (wa katikati) wakiwa katika ukumbi wa wazi wa mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakisubiri kusomewa mashtaka dhidi ya yao ya kusafirisha kilogramu 268.50 za dawa za kulevya aina ya Heroine na kutakatisha  USD 61,500 pamoja na Sh.milioni 17.8
Akisoma hati ya mashtaka, wakili Batlida amedai kuwa, Aprili 4, mwaka 2020 huko katika eneo la Mbezi Kibanda cha Mkaa ndani ya Wilaya ya Ubungo Jijini Dar es Salaam,
washtakiwa walikutwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya Heroine zenye uzito wa kilogramu 268.50.

Aidha katika shtaka la pili lililosomwa na wakili mwandamizi Wankyo imedaiwa kuwa, kati ya Januari 2016 na Aprili 15 2020 katika maeneo tofauti ya jiji la Dar es Salaam, washtakiwa hao walijihusisha katika miamala iliyohusisha fedha USD 61,500 na fedha za kitanzania Sh. 17,835, 500 huku wakijua kuwa fedha hizo ni zao la kosa tangulizi la kusafirishi dawa za kulevya. 


Hata hivyo, washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu kitu
 chochote mahakamani hapo na wamerudishwa rumande kwa kuwa mashtaka yanayowakabili hayana dhamana. 

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi katika kesi hiyo bado haujakamilika na kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 8 mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.

Aidha upande wa mashtaka umesema kutoka na uwepo wa ugonjwa hatari wa homa ya mapafu (CORONA) wameshawapima washtakiwa wote watatu na wako salama na hivyo wanaweza kwenda mahabusu.

No comments:

Post a Comment