|
Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi
akizungumza jambo wakati alipotembelea kituo cha watu waliopata
maambukizi ya virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Corona (COVID – 19)
cha Amana jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuona namna ambavyo
madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo watakavyoweza kutoa huduma kwa
wagonjwa hao. |
Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) itawahudumia wagonjwa wenye matatizo ya
moyo yanayohitaji matibabu ya kibingwa walioko katika kituo cha watu
waliopata maambukizi ya virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Corona (COVID
– 19) cha Amana jijini Dar es Salaam.
Hayo
yamesemwa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Prof. Mohamed
Janabi alipotembelea kituo hicho kwa ajili ya kuona ni namna gani
wataalamu wa JKCI watavyoweza kutoa huduma kwa wagonjwa wa moyo kituoni
hapo.
Prof.
Janabi alisema licha ya Taasisi hiyo kwenda katika kituo hicho kutoa
huduma ya matibabu ya kibingwa ya moyo pia itatoa mafunzo kwa vikundi
vya watu wachache kwa wafanyakazi wa Hospitali hiyo ambayo yatawasaidia
katika utendaji wao wa kazi wa kila siku hasa katika kipindi hiki cha
janga la Corona.
|
Msimamizi
wa kituo cha watu waliopata maambukizi ya virusi vinavyosababisha
ugonjwa wa Corona (COVID – 19) Dkt. Stanley Binagi akielezea jinsi
wanavyowahudumia wagonjwa hao wakati wataalamu kutoka Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete JKCI na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) walipotembelea
kituo hicho leo ili kuona namna ambavyo watatoa huduma za kibingwa kwa
wagonjwa hao.
|
Wataalamu
kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete JKCI na Hospitali ya Taifa
Muhimbili (MNH) wakiwa katika picha ya pamoja mara walipomaliza kikao
chao na uongozi wa kituo cha watu waliopata maambukizi ya virusi
vinavyosababisha ugonjwa wa Corona (COVID – 19) cha Amana jijini Dar es
Salaam. Wataalamu hao walitembelea kituo hicho kwa ajili ya kuona
namna ambavyo watatoa huduma za kibingwa kwa wagonjwa wanaotibiwa katika
kituo hicho. Picha na JKCI
“Mimi
pamoja na wataalamu wangu tumekuja hapa ili kuona ni jinsi gani
tunaweza kushirikiana kwa pamoja katika kutoa huduma za matibabu ya moyo
kwa wagonjwa. Kwani wagonjwa wa Corona ambao wana matatizo ya moyo
wanahitaji kupata huduma za matibabu walizokuwa wanazipata kabla
hawajapata maambukizi”,.
“Pia
tutatoa mafunzo katika makundi ya watu wachache kwa wataalamu wa afya
ya jinsi ya kutoa huduma kwa wagonjwa hasa wenye matatizo ya moyo”,
alisema Prof. Janabi.
Kwa
upande wake Dkt. Stanley Binagi ambaye ni msimamizi wa kituo hicho
alisema baadhi ya wagonjwa waliopo katika kituo cha Amana wanasumbuliwa
na magonjwa mengine ikiwepo moyo, figo na kisukari yanayohitaji
matibabu ya kibingwa .
“Ninawashukuru
Wataalamu kutoka JKCI na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambao
mmefika katika kituo hiki na kuona jinsi gani mnaweza kushirikiana na
sisi katika kutoa huduma za matibabu ya kibingwa kwa wagonjwa wa COVID
-19”.
“Kupatikana
kwa huduma za matibabu kutoka kwa wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kutasaidia kwa kiasi
kikubwa kuokoa maisha ya wagonjwa hawa”, alisema Dkt. Binagi.
| |
|
No comments:
Post a Comment