Mkuu wa mkoa wa Rukwa
Mh. Joachim Wangabo amewataka viongozi wa vitongoji, vijiji pamoja na watendaji
wao wa kata za Korongwe na Kabwe kuhakikisha wanawahamasisha wananchi katika
maeneo yao kuwa mstari wa mbele katika kuilinda nchi kutokana na ugonjwa wa
Corona kwa kuzuia uingiaji holela wa wageni wanaoweza kuuleta ugonjwa huo
kutoka nchi za jirani.
Mh Wangabo amesema
kuwa hadi sasa mkoa wa Rukwa umewaweka Karantini watu 49 ambapo kati ya hao watanzania
36 na wageni 13 ambao walipita katika bandari na mipaka rasmi ya mkoa huo na
kusisitiza kuwa katika utekelezaji wa kuwaweka watu Karantini hauangalii uraia
wa mtu wala hadhi yake, na kuongeza kuwa inachokijali serikali ni usalama wa wananchi
wake dhidi ya ugonjwa hatari wa Corona.
Hivyo amewataka
viongozi hao kuwaelimisha wananchi kuwakataa wageni wasiotumia mipaka na
bandari rasmi kuingia katika nchi kwani kutofanya hivyo kutailetea nchi maafa
makubwa na hivyo na hivyo kuwataka viongozi na wananchi kuacha matumizi ya
bandari bubu zilizopo katika vijiji vya mwambao wa ziwa Tanganyika.
“Waende wakapite
katika maeneo ambayo ni rasmi, waje hapa kwenye bandari ya Kabwe, wapite hapo
na taratibu nyingine za kiafya zitafanyika, lakini sio kwenye bandari bubu
huku, bandari bubu ni marufuku kutumika, ndani ya wilaya hii ya Nkasi kuna
bandari bubu 46, Nkasi peke yake na katika kata zenu mbili hizi, ya Korongwe na
Kabwe kuna bandari bubu 13, ndio maana nikasema viongozi ninyi wa kata mbili
hizi mje hapa, ili muone umuhimu wa kuzuia watu kiholela holeal kuja kwenye
bandari hizi bubu,” Alisisitiza.
Mkuu wa mkoa wa Rukwa mh. Joachim Wangabo akizungumza na viongozi mbalimbali wa vijiji na vitongoji vinavyopaka na mwambao wa ziwa Tanganyika katika kata za Korongwe na Kabwe Wilayani Nkasi |
Wangabo ameyasema
hayo wakati wa kikao na wenyeviti wa vitongoji na vijiji vyenye bandari bubu
pamoja na watendaji wa kata Kabwe na Korongwe zinazobeba vijiji hivyo katika
kikao kilicholenga kutoa elimu ya ugonjwa wa Corona kwa viongozi hao pamoja na
kutoa maelekezo ya serikali dhidi ya mapambano ya ugonjwa huo.
Kwa upande wake
Kamanda wa Jeshi la Uhamiaji Mkoa wa Rukwa Kamishna Msaidizi Elizeus Mushongi
alitahadharisha matumizi mabaya ya madaraka ya viongozi hao ambao huwapokea
wageni hao na kuwaruhusu kuingia katika nchi bila ya kufuata utaratibu wa
serikali na kuongeza kuwa matumizi ya bandari bubu ni haram una hivyo
atakayekamatwa anahalalisha matumizi ya bandari hizo hatua kali zitachukuliwa
dhidi yake.
“Wageni kutoka nje ya
nchi, iwe Kongo, iwe Burundi, iwe Zambia, mnawapokea kule na nyinyi ndio
mnakuwa maafisa uhamiaji, mnakuwa maafisa forodha, kila kitu mnamaliza wenyewe
kule, sasa kama mtampokea mtu anaumwa ule ugonjwa, ninyi ndio mtakaoanza
kuupokea ule ugonjwa kabla ya wote na bila ya kujua mtaenda kuambukiza familia
na familia kama dokta alivyosema, niwaombe sana msipokee watu kutoka nje ya
nchi kama hawajapita katika vituo vilivyoainishwa kisheria,” Alisema.
Aidha wakati akitoa salamu
zake kwa mkuu wa mkoa, Diwani wa Viti Maalum Mh. Christina Simbakavu alisema
kuwa kuna baadhi ya watu wenye ndugu zao nchi ya jirani ya Kongo huwa na
kawaida ya kuingia katika vijiji hivyo nyakati za usiku na ndugu zao huwapokea katika
utaratibu ambao unaweza kuhatarisha maisha yao.
“Kuna boti zinazoingia
usiku kama alivyotamka mjumbe wa Kijiji cha Kalila, zile boti zinaingia lakini
wenyeji wenye ndugu zao kutoka nchi jirani ya kongo wanawapokea katika
mazingira ambayo sio Rafiki sana na hawatoi taarifa, na hili nalo linafukuta
lakini hatujapata uhakika uliowazi, tunajaribu kuongea na wananchi kuwa
tusipokee wageni wa aina yoyote na nawaomba viongozi wangu tuhamasishe utumiaji
wa maji na sabuni kunawa na katika nyumba zetu tuweke vifaa hivyo,” alisema.
Naye Diwani wa Kata
ya Korongwe Mh. Venus Bamilitwaye wakati akitoa neno la shukurani ka mkuu wa
mkoa wa rukwa aliwasisitiza viongozi wa kata hizo kuhakikisha wanashirikiana na
wananchi katika kulinda bandari bubu pamoja na kuzuia uingiaji wa kiholela wa
wageni jambo ambalo ni hatari kwa afya ya wananchi wa mkoa wa Rukwa na Tanzania.
No comments:
Post a Comment