Na Amiri kilagalila, Njombe
Serikali mkoa wa Njombe imezindua soko la uuzaji wa madini ya dhahabu
na vito kwa nia ya kudhibiti wimbi la utoroshaji wa madini uliokuwa
unafanywa na wachimbaji waliokuwa wakikwepa kulipa mapato ya serikali.
Akizungumza katika uzinduzi huo mkuu wa mkoa wa Njombe Christopher
Ole Sendeka amesema kuwepo kwa soko hilo la madini itasaidia wachimbaji
hao kutumia fursa na njia zilizosahihi kulipa mapato kwa serikali.
“Kuanzisha soko la madini katika mkoa wetu inakuwa ni fursa ya
serikali katika kukusanya mapato yake yanayotokana na madini, lakini pia
eneo letu hili la soko la madini litakalokuwa pia eneo linalotoa elimu
ya uchimbaji wa madini kwa njia ya kisasa na kueleza kuwaunganisha
wananchi na wawekezaji wengine wenye nia ya kuwekeza mkoani
Njombe"alisema Ole Sendeka.
Ole Sendeka alisema mkoa wa Njombe unayo rasilimali nyingi ya madini
mbalimbali ikiwemo aina tofauti ya vito, hivyo ni vyema wachimbaji wa
madini wakaendelea kuhamasisha wawekezaji mbalimbali wakaja mkoani hapa
kuwekeza kwa maslahi mapana ya taifa.
“Nampongeza sana Rais Dkt. Magufuli kwa kuhakikisha kwamba rasilimali
na utajiri wa nchi yetu unatumika kwa manufaa na maslahi mapana ya
nchi yetu, sasa namna bora ya kumuunga mkono Rais ni kuhakikisha madini
yetu yanazalishwa bila kujali madini ya kiwandani madini ya vito
yanapitwa katika mfumo na yanauzwa katika utaratibu rasmi uliowekwa na
serikali”alisema Ole Sendeka.
Kwa upande wake,kamishina wa madini mkoa wa Njombe, Wilfred Machumu
alisema mkoa wa Njombe changamoto iliyopo kwa sasa ni utoroshaji wa
madini kwenye baadhi ya maeneo yaliyopo mkoani humo hali inayosababisha
kuikosesha mapato serikali.
“Utoroshaji wa madini upo mkubwa sana katika mkoa wa Njombe,hasa
maeneo ya Uwemba,Lola Lupembe na Mfumbi Makete, yale maeneo ndiyo
yanayotusumbua sana na hayo ndiyo takwimu zinaonyesha kuwa ndiko kwenye
utoroshaji mkubwa sana,tumepanga kuongeza nguvu katika kuyafatilia
maeneo hayo kuhakikisha hakuna jambo hilo"alisema Machumu.
Baadhi ya wachimbaji wa madini akiwemo Abusalum Sanga walimweleza Ole
Sendeka kuwa mkoani Njombe rasilimali ya madini ni nyingi isipokuwa
changamoto iliyopo ni kukosekana kwa vifaa vya kusaidia uchimbaji wa
madini ya aina mbalimbali kwenye mkoa wa Njombe ikiwemo madini aina ya
shaba ambayo walisema iko kwenye ubora wa juu tofauti na maeneo mengine
hapa nchini.
“Tatizo linalotukwami sisi wachimbaji hapa Njombe ni kukosekana kwa
mashine ambazo zingekuwa mkombozi mkubwa na tungekuwa mbali sana kwenye
uchimbaji wa madini hapa mkoani, dhahabu iliyopo kata ya Ibumi ni nzuri
na safi lakini kikwazo ni vifaa vya kuchimbia vinatuangusha"alisema
Sanga.
Kwa upande wa mwenyekiti chama cha wachimbaji madini mkoa wa Njombe
Alfred Luvanda alisema soko hilo litajenga imani ya uwekezaji sekta ya
madini kwa wakazi wa mkoa huo kinyume na hapo awali.
No comments:
Post a Comment