Sekta ya Uchukuzi inatoa mchango
mkubwa katika shughuli za maendeleo ya uchumi na pia ni mwezeshaji mkubwa wa
sekta za uzalishaji, biashara na usambazaji wa bidhaa na huduma katika soko la kitaifa
na kimataifa.
Usafirishaji wa bidhaa na huduma katika
masoko, hutegemea zaidi mfumo wa uchukuzi wenye tija na ufanisi kwa ajili ya
uhimizaji na uwezeshaji wa biashara na hivyo kupunguza gharama za uendeshaji pamoja
na kuokoa muda.
Kivuko cha M.V Kitunda kikiendelea kutoa huduma za usafiri wa abiria, mizigo na magari katika Manispaa ya Lindi kama kilivyokutwa na kamera ya Idara ya Habari MAELEZO hivi karibuni. Picha na MAELEZO |
Mkoa wa Lindi ni miongoni mwa
Mikoa iliyopo pembezoni mwa nchi, ambapo katika miaka ya hivi karibuni umekuwa
na kasi kubwa ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi kutokana na juhudi
zilizofanywa na Serikali katika kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na
Makazi ya mwaka 2012, Mkoa wa Lindi una jumla ya wakazi 864,652, huku nusu ya
wakazi hao wakiishi katika maeneo ya pembezoni kuzunguka bahari ya Hindi na
wananchi hao kulazimika kutembea umbali mrefu kutafuta huduma za kijamii
kutokana na maeneo hayo kukosa usafiri
wa uhakika.
Kivuko cha M.V Kitunda kikiendelea kutoa huduma za usafiri wa abiria, mizigo na magari katika Manispaa ya Lindi kama kilivyokutwa na kamera ya Idara ya Habari MAELEZO hivi karibuni. Picha na MAELEZO |
Miongoni mwa maeneo yaliyokuwa
yakikabiliwa na changamoto kubwa ya usafiri ni Kijiji cha Kitunda kilichopo
Manispaa ya Lindi ambao awali wananchi wake walikuwa wakitumia vyombo visivyo
salama vya usafiri ikiwemo mitumbwi, ngalawa na majahazi kwa ajili ya kuingia
na kutoka eneo la Manispaa ya Lindi kutafuta huduma za kijamii.
Katika kukabiliana na changamoto
hiyo, Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ilitekeleza
ahadi iliyotolewa na Rais Dkt. John Magufuli aliyoitoa kwa wananchi wa Manispaa
ya Lindi wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani wa
mwaka 2015, ilijenga kivuko cha M.V Kitunda kinachotoa huduma ya usafiri wa
abiria, magari na mizigo.
Kivuko cha M.V Kitunda kikiendelea kutoa huduma za usafiri wa abiria, mizigo na magari katika Manispaa ya Lindi kama kilivyokutwa na kamera ya Idara ya Habari MAELEZO hivi karibuni. Picha na MAELEZO |
Akizungumza katika mahojiano
maalum na MAELEZO, Meneja wa Wakala wa Huduma za Ufundi na Umeme (TEMESA) Mkoa
wa Lindi, Mhandisi Locky Sabigoro anasema kivuko hicho kilianza kazi rasmi
mwezi Machi 2018, ambapo Serikali ilifanya maboresho ya miundombinu mbalimbali yenye
thamani ya Tsh Bilioni 2.2.
Aidha Sabigoro anasema kati ya
fedha hizo, kiasi cha Tsh Bilioni 1.9 zimetumika kwa ajili ya kujenga
miundombinu ya barabara ya kuingilia katika eneo la Kivuko na Tsh Milioni 333
zimetumika kwa ajili ya kujenga maegesho na barabara na kuongeza kuwa Serikali
imetumia kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya kuhakikisha kuwa wananchi
wanapata huduma ya uhakika ya kivuko.
Mhandisi Sabigoro anasema kivuko
cha M.V Kitunda kina uwezo wa kubeba abiria 100 na mizigo yenye uzito wa tani
50 pamoja na magari sita kwa wakati mmoja na inatumia muda wa dakika 10 hadi 12
tofauti na wakati wa nyuma ambapo walikuwa wanatumia zaidi ya saa 1 kwa ajili
ya kuvuka kuelekea upande wa pili.
Kivuko cha M.V Kitunda kikiendelea kutoa huduma za usafiri wa abiria, mizigo na magari katika Manispaa ya Lindi kama kilivyokutwa na kamera ya Idara ya Habari MAELEZO hivi karibuni. Picha na MAELEZO |
‘’Kivuko hiki cha M.V Kitunda
kina uwezo wa kubeba abiria 1800 kwa siku lakini kwa idadi ya wakazi waliopo
katika eneo la Kitunda-Manispaa ya Lindi unakuta kivuko kinabeba abiria 500-600
kwa siku, tumeongea na Serikali ya Mkoa kuona namna bora ya kujenga vivutio vya
uwekezaji’’ alisema Mhandisi Sabigoro.
Akifafanua zaidi Sabigoro anasema
Serikali ya Mkoa tayari imeanza maandalizi ya kujenga miundombinu ya huduma za
kijamii ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya, ujenzi wa shule na vyuo vya elimu ya juu katika Eneo
la Kitunda ili kuongeza kasi ya ukuaji wa kijiji cha Kitunda na kurahakisha
kasi ya ukuaji wa maendeleo ya Mkoa wa Lindi.
Mhandisi Sabigoro anasema hapo
awali hali ya mawasiliano ya usafiri baina ya wananchi wa Kitunda na Manispaa
ya Lindi haikuwa nzuri kwani wakazi wa maeneo hayo walilazimika kutumia
mitumbwi na maboti kwa ajili ya
kuvuka upande wa pili kwa ajili ya
kupata huduma muhimu za kijamii, ambazo nyingi zinapatikana eneo la Manispaa ya
Lindi.
Anaongeza kuwa kwa sasa wananchi
wanafurahia huduma ya kivuko cha MV Kitunda kutokana na kutumia muda mfupi
kuvuka katika eneo hilo, hivyo TEMESA Mkoa wa Lindi imejipanga kuhakikisha kuwa
inalinda miundombinu ya kivuko hicho ili kuleta maendeleo endelevu kwa ustawi
wa wananchi wa Manispaa ya Lindi.
‘’Mhe. Rais aliona namna watu
walivyokuwa wakihangaika hususani akina mama, walikuwa wakidhalilika sana na
wakati ule magari yalikuwa yanazunguka upande wa pili wa eneo la mnazimmoja na
kusafiri umbali wa kilometa 70 kuingia eneo la Kitunda, lakini kwa sasa hali ni
tofauti usafiri umekuwa rahisi na kutoa unafuu mkubwa kwa wananchi’’ alisema
Mhandisi Sabigoro.
Wananchi mbalimbali wa Manispaa
ya Lindi wamempongeza Rais Dkt. John Magufuli na serikali ya awamu ya tano kwa
kuendelea kutimiza ahadi ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo hapa
nchini ikiwemo ujenzi wa kivuko cha M.V Kitunda ambao utasaidia kuondoa changamoto
ya usafiri kwa wananchi kati ya Manispaa ya Lindi na kijiji cha Kitunda.
Bi. Subira Hamisi Mkazi wa
Manispaa ya Lindi anasema kabla ya kivuko cha M.V Kitunda hali ya usafiri baina
ya kijiji cha Kitunda na Manispaa ulikuwa mgumu, na vyombo vya usafiri vilivyotumika
havikuwa na utaratibu maalum, lakini kwa sasa hali ni tofauti wanasafiri muda
wote na kivuko kinachotumika kina usalama wa uhakika.
Tunapoingeza Serikali kwa kuondoa
changamoto ya usafiri kwetu sisi wakazi wa Manispaa ya Lindi, kwa hapo awali
ndugu zetu hususani akina mama walikuwa wanapata matatizo mbalimbali pindi
walipokuwa wanatumia mitumbwi na maboti ambayo hayakuwa na uhakika wa
kupatikana kwake pale ilipokuwa ikihitajika’’ alisema Subira.
Naye Bw. Mohamed Nguse Mkazi wa
Kijiji cha Kitunda anasema Kivuko cha M.V Kitunda kimesaidia kuondoa changamoto
ya usafiri kwa wananchi kati ya Kijiji cha Kitunda na Manispaa ya Lindi na
kuinua kipato cha wananchi wa maeneo hayo, kiuchumi na kijamii kwa kuwa
Serikali imeanza ujenzi wa vivutio vya uwekezaji vinavyoharakisha ukuaji wa Mji
huo na Mkoa wa Lindi kwa ujumla.
Aliongeza kuwa ili kuhakikisha
kuwa kivuko hicho kinaendelea kutoa huduma bora, aliwaomba wananchi wote kuhakikisha
kuwa kivuko hicho kinatunzwa vizuri huku huku wakizingatia usalama wa abiria na
mali zao, huku akiishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kutoa fedha zote
zilizotengwa kwa ajili ya kutekeleza ujenzi wa kivuko hicho.
Kwa upande wake Bi Saidika Nanjemela
wa Kijiji cha Kitunda, Manispaa ya Lindi alisema kivuko cha M.V Kitunda ni
mkombozi wa uhakika wa usafiri kwa wananchi wote wa Manispaa ya Lindi kwa kuwa
utatoa fursa ya kuweza kushiriki katika shughuli za uzalishaji ikiwemo kilimo
ambao ndiyo msingi wa maisha ya wananchi wengi wa vijijini.
Uwepo wa kivuko cha M.V Kitunda
katika Manispaa ya Lindi, fursa kwa
wananchi kuweza kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali ikiwemo kilimo ili
kujiongezea kipato na kujikwamua na umaskini kupitia fursa mbalimbali
zinazotolewa na Serikali.
Ni wajibu wa wananchi na wadau
mbalimbali wa maendeleo kujitokeza na kuunga mkono juhudi hizo ili kuweza kutoa
hamasa kwa serikali kuongeza juhudi katika kubuni mikakati, mipango na sera
mbalimbali zitakazosaidia kuharakisha kasi ya ukuaji wa uchumi nchini.
No comments:
Post a Comment