Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA
Tume ya Kurekebisha
Sheria Tanzania imekabidhi Taarifa ya Mapitio ya Sheria Zinazosimammia Utatuzi wa
Migogoro ya Ardhi nchini kwa Waziri wa Katiba ba Sheria Dkt Balozi Augustine Mahiga.
Taarifa hiyo
imekabidhiwa kufuatia Tume ya Kurekebisha Sheria kufanya utafiti baada ya kupokea
maelekezo ya Wizara ya Katiba na Sheria yakitaka kupitia Mfumo wa Utatuzi wa
Migogoro ya Ardhi Tanzania.
Makabidhiano hayo
yamefanyika leo tarehe 20 Aprili 2020 katika ofisi za Wizara ya Katiba na
Sheria zilizopo Mji wa Serikali eneo la Mtumba jijini Dodoma ambapo Mwenyekiti
wa Tume ya Kurekebisha Sheria Jaji Mstaafu Januari Msofe alimkabidhi Waziri wa
Katiba na Sheria Dkt Balozi Augustine
Mahiga.
Akielezea Utafiti wa
Mapitio ya Sheria hiyo wakati wa makabidhaino ya Taarifa hiyo, Jaji Mstaafu
Msofe alisema, katika kukamilisha mapitio ya sheria hiyo Tume ilikusanya maoni
ya wadau mbalimbali kwenye mikoa ya Shinyanga, Mwanza, Tanga, Kilimanjaro,
Arusha, Dodoma, Iringa , Mbeya , Songwe na Dar es Salaaam.
‘’Baada ya Tume kukusanya
maoni ya wadau wakiwemo Majaji, Mawakili, Wasajili wa Mabaraza ya Ardhi,
Wenyeviti wa Mabaraza na Wajumbe wa Kata na Wazee wa Mabaraza Tume imebaini changamoto mbalimbali zilizosababisha kutofikiwa malengo
yaliyokusudiwa ambayo ni mfumo wa
utatuzi wa migogoro ya ardhi wa haraka ,
haki na unaofikika kwa urahisi’’ alisema
Jaji Mstaafu Msofe.
Alizitaja baadhi ya
changamoto kuwa ni pamoja na Mamlaka za Kipekee za Mahakama za Ardhi ambazo
utafiti wake ulionesha lengo kutofikiwa kutokana na kukosekana rasilimali
fedha, watu na vitendea kazi sambamba na idadi ndogo ya mabaraza ya ardhi na
nyumba ya wilaya.
Aidha, Mwenyekiti wa
Tume, ameeleza Uhuru wa Mahakama za Ardhi kuwa ni changamoto yenye kasoro kutokana
na baadhi ya mahakama hizo kuwa chini ya mhimili wa serikali na kutolea mfano wa Mabaraza ya Ardhi ya Vijiji, Kata na Wilaya.
Hata hivyo, Jaji
Mstaafu Msofe amezitaja changamoto nyingine kuwa ni kufikika kwa mabaraza ya
kata na ya wilaya, Ada zitolewazo na mahakama za ardhi, lugha inayotumika kwenye
mahakama za ardhi, vigezo vya wajumbe wa baraza la ardhi la kijiji na kata, Uharaka katika kusikiliza
na kuamua mashauri, Wazee wa Baraza katika mabaraza ya nyumba ya wilaya,
miongozo katika utatuzi migogoro, utozaji ushuru wa hati za madai ya gharama na
muongozo wa mwenendo wa maadili ya wajumbe wa mabaraza ya ardhi ya kijiji na
mabaraza ya kata.
Kwa upande wake waziri
wa Katiba na Sheria Dkt Balozi Augustine Mahiga aliipongeza Tume ya Kurekebisha
sheria kwa kutekeleza kazi ya utafiti kuhusiana na sheria ya utatuzi wa
migogoro ya ardhi na kubainisha kuwa kazi hiyo ni moja ya masuala mengi ambayo Tume
inatakiwa kuyafanyia kazi huku Tume hiyo ikiwa na mzigo mkubwa wa kazi mbalimbali
za mapitio ya sheria.
‘’Kama kuna sehemu
ambayo Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania inahitaji msaada basi ni katika eneo
la Mapitio mbalimbali ya sheria ambazo nyingi zimepitwa na wakati na zinahitaji
kupitiwa upya’’ alisema Dkt. Balozi Mahiga.
Naye
Katibu Mkuu wa
Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania Casmir Kyuki alisema kati ya ripoti
ambazo
tume imezifanyia kazi , Ripoti ya Utafiti Kuhusiana na Mapitio ya Sheria
Zinazosimamia Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi imefanyika kwa haraka na
kasi kubwa kufuatia mhimu
wa sheria yenyewe sambamba na kutekeleza matakwa ya sheria kama
inavyoelekeza.
Utafiti uliofanywa na Tume ni utekelezaji wa majukumu yake kama yalivyoanishwa katika kifungu
cha 4 (1), (2) na (4) cha Tume ya Kurekebisha Sheria kinachotamka kuwa jukumu
kubwa la Tume ni kufanya Mapitio, Utafiti na Kutathmini maeneo yote ya sheria
zote za Tanzania Bara na kutoa mapendekezo serikalini ya namna ya kuboresha
sheria hizo ili ziakisi mabadiliko yanayotokea.
No comments:
Post a Comment