Waziri
wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa (katikati) akipata ufafanuzi
kuhusu matumizi ya mashine ya Cherehani katika utengenezaji wa Barakoa
kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Uchapishaji cha Five
stars, Ashik Abbas Karim (kushoto), Aprili 20, 2020 alipokua katika
ziara ya Jijini Dar es Salaam ya kutembelea Viwanda vinavyozalisha
Barakoa na Vitakasa Mikono.
Waziri
wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa (katikati) akisikiliza kwa
makini maelezo ya eneo la uzalishaji kutoka kwa Msimamizi wa Mradi wa
Uzalishaji Vitakasa mikono kutoka Kampuni ya Total, Umesh Ankoleker
(kulia) Aprili 20, 2020 alipokua katika ziara ya Jijini Dar es
Salaam ya kutembelea Viwanda vinavyozalisha Barakoa na Vitakasa Mikono.
Waziri
wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa (kulia) akipata ufafanuzi
kuhusu mtambo wa kutengeneza Barakoa kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa
Kiwanda cha Uchapishaji cha Five stars, Ashik Abbas Karim (kushoto),
Aprili 20, 2020 alipokua katika ziara ya Jijini Dar es Salaam ya
kutembelea Viwanda vinavyozalisha Barakoa na Vitakasa Mikono.
WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa amebainisha kwamba
Serikali imejipanga kuzalisha zaidi ya Barakoa Milioni tatu na nusu kwa
mwezi ili kukidhi mahitaji ya Watanzania wote.
Hayo ameyasema Aprili 20, 2020 alipokua katika ziara ya Jijini
Dar es Salaam ya kutembelea Viwanda vinavyozalisha Barakoa (face mask)
na Vitakasa mikono (Hand sanitizer) ambapo kwa siku ya leo ziara hiyo
imefanyika katika Kiwanda cha Uzalishaji cha Prestine, Kiwanda cha
Uchapishaji cha Five stars na Kiwanda cha Uzalishaji Mafuta na
Vilainishi cha Total.
Waziri Bashungwa ameeleza kwamba Uzalishaji wa Barakoa za kutosha kwa
sasa ni muhimu sana na Serikali inahakikisha kwamba Viwanda hivi
vinapata malighafi ya kutosha ili viendelee kuzalisha vizuri.
“Kiwanda cha Prestine sasa hivi kinatengeneza Barakoa elfu thelathini
kwa siku (30,000) lakini baada ya vifaa kuingia kitazalisha elfu
hamsini kwa siku (50,000) na Kiwanda cha Five Star kitazalisha barakoa
laki moja kwa siku (100,000) hivyo kwa ujumla Viwanda hivi vitazalisha
barakoa zisizopungua milioni tatu na nusu kwa mwezi mmoja (3,500,000)
hii ni hatua muhimu sana.”alisema Waziri Bashungwa.
Akizungumza kuhusiana na ziara yake katika Kiwanda cha Total Waziri
Bashungwa ameeleza kwamba Uongozi umekubali kushirikiana na Serikali
katika kuzalisha vitakasa mikono na tayari maandalizi ya awali
yamefanyika ikiwa ni pamoja na kuangalia sehemu ambayo itatumika kwa
ajili ya uzalishaji.
“Baada ya kuangalia Kiwanda na eneo maalumu ambalo wamelitenga kwa
ajili ya uzalishaji wa vitakasa mikono, na kwa uwezo wa kiwanda hiki kwa
siku kitakua na uwezo wa kutengeneza lita elfu sita (6000) ikiwa ni
sehemu ya jitihada za serikali kudhibiti ugonjwa huu.” Aliongeza Waziri
Bashungwa.
Katika hatua ya mwisho Waziri Bashungwa ametoa wito kwa watanzania
“Natoa wito kwa wazalishaji wengine kujitokeza na Serikali tutawapa
ushirikiano wa kipekee, Pia Tuendelea kuzingatia melekezo na kanuni za
kujikinga na Maambukizi ya virusi vya Corona (COVID -19).”
No comments:
Post a Comment