Na. Farida Ramadhani na Peter Haule, WFM, Dodoma
Serikali imesema kuwa imetenga Sh. bilioni 600 kwa
ajili ya kulipa madeni yaliyohakikiwa ya Watumishi wa umma kwa mwaka wa fedha
2019/2020 ikiwa ni moja ya mkakati wa kuleta nidhamu na uwajibikaji katika
matumizi ya fedha za umma.
Hayo yameelezwa jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha
na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, alipokuwa akijibu swali la msingi la
Mbunge wa Bumbwini, Mhe. Muhammed Amour Muhammed, aliyetaka kujua ni lini
Serikali italipa madeni ya Watumishi wa umma kutokana na madeni hayo kuongezeka.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji |
Dkt. Kijaji alisema kuwa Serikali imetenga jumla ya
Sh. bilioni 600 ambazo zimeidhinishwa na Bunge ili kugharamia malipo ya madeni
mbalimbali ikijumuisha madeni ya Watumishi kwa mwaka wa fedha 2019/2020.
“Hadi kufikia mwezi Machi, 2020 jumla ya shilingi
bilioni 364.7 zimelipwa kama madai ya Watumishi, Wazabuni na Wakandarasi ambapo
kati ya hizo kiasi cha shilingi bilioni 97.6 zimelipwa kama madeni ya Watumishi
pekee”, alieleza Dkt. Kijaji.
Alisema kuwa katika kipindi cha kuanzia mwaka wa fedha
2015/2016 hadi 2019/2020 jumla ya Sh. bilioni 375.7 zilitolewa kugharamia
madeni mbalimbali, kati ya fedha hizo Sh. bilioni 113.8 zilitumika kulipa
madeni ya mshahara na Sh. bilioni 261.9 madeni yasiyo ya mshahara.
Dkt. Kijaji alibainisha kuwa, kutokana na changamoto
ya uwepo wa madeni hewa Serikali ilizuia ulipaji wa madeni kabla ya kuhakikiwa
lengo likiwa ni kuleta nidhamu ya matumizi ya fedha za umma.
Aidha kutokana na takwimu hizo, Serikali inajisikia
fahari na inahitaji kupongezwa kutokana na juhudi mbalimbali inazochukua katika
kuhakikisha madeni yote ya Watumishi yanalipwa kwa wakati ikithibitika yana
uhalali.
No comments:
Post a Comment