Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Singida, Adili Elinipenda, akizungumza na waandishi wa habari.
Na Godwin Myovela, Singida.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCB) Mkoa wa Singida imemburuza mahakamani Dkt. Abdul Sewando wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida (Mandewa) akituhumiwa kwa kosa la kuomba na kupokea rushwa kutoka kwa mgonjwa kinyume na kifungu cha 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya Mwaka 2007.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jana kwenye ofisi za PCCB, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Singida, Adili Elinipenda, alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa Mei 5, 2020 majira ya saa 9 na nusu alasiri baada ya kuwekewa mtego na kujiridhisha uwepo wa tuhuma hizo.
Alisena mtuhumiwa alikamatwa na maafisa wa TAKUKURU baada ya kumaliza kumsafisha mgonjwa akiwa eneo la Hopitali hiyo ya Rufaa ya Mkoa wa Singida (Mandewa)
Elinipenda alisema awali uchunguzi wa TAKUKURU mkoani hapo ulibaini, Mei 6, 2020 mtuhumiwa alipokea kiasi cha sh.60, 000 kutoka kwa mgonjwa ambaye jina lake limehifadhiwa ili ampe huduma ya kumsafisha baada ya kumfanyia vipimo vya ' Ultra Sound.'
Alisema uchunguzi wao pia ulibaini kuwa mtuhumiwa alielekeza atumiwe fedha hizo kwa njia ya mtandao ambapo alizipokea kwa njia ya Mpesa kupitia simu yake.
Elinipenda alisema TAKUKURU Mkoa wa Singida inatoa rai kwa watumishi wa idara ya afya mkoani humo kufanyakazi kwa kuzingatia maadili na miiko ya taaluma zao hususani kipindi hiki ambacho jamii inawategemea sana kutokana na janga la Corona.
Aidha alisema Wananchi wasisite kutoa taarifa za vitendo vya rushwa kwa kufika ofisini, kupiga simu ya bure 113, kutuma ujumbe kwenye namba 113 na kupakua TAKUKURU App.
No comments:
Post a Comment