Utoaji
wa mafunzo ya mara kwa mara ya jinsi ya kupambana na ugonjwa wa Corona (COVID-19) kwa wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) umewasaidia kuelewa namna ya kujikinga na ugonjwa huo na kuwahudumia wagonjwa bila ya kupata
maambukizi.
Mafunzo hayo
ambayo yamekuwa yanatolewa kwa
wafanyakazi wa Taasisi hiyo tangu ugonjwa huo ulipotangazwa hapa nchini mwanzoni
mwa mwezi wa tatu mwaka huu yamewasaidia kutokuwa na hofu na kuendelea kutoa huduma ya
matibabu kwa wagonjwa wanaotibiwa katika Taasisi hiyo kiufanisi zaidi.
Hayo
yamesemwa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Prof.
Mohamed Janabi wakati akizungumza na baadhi ya wafanyakazi wa Taasisi hiyo
waliohudhuria mafunzo hayo.
Prof. Janabi
alisema baada ya wafanyakazi wa JKCI kupewa mafunzo wameweza kuufahamu vizuri ugonjwa wa Corona, kufahamu
njia za kuzifuata ili wasipate maambukizi na wasiwaambukize wengine na kuondoa unyanyapaa kati yao na wagonjwa kwani
ugonjwa wa Corona hauchagui unaweza kumpata mtu yeyote.
“Katika
mafunzo tunayoyatoa kwa wafanyakazi wetu tunawafundisha jinsi ya kuwahudumia
wagonjwa kipindi hiki Kkigumu ambacho Dunia inapambana na janga la ugonjwa wa
Corona. Kwani baadhi ya dalili za
ugonjwa huu zinafanana na magonjwa ya moyo ambazo ni kushindwa kupumua na kukohoa
hivyo basi wakifahamu jinsi ya kujikinga kutawasaidia kuepuka kupata maambukizi’’, alisema Prof.
Janabi.
Mkurugenzi
huyo Mtendaji alisema ili kuwalinda wafanyakazi wa Taasisi hiyo wasipate maambukizi wamefunga mashine ya kutakasa mwili, wametoa vitakasa
mikono pamoja na barakoa kwa wafanyakazi wote pamoja na kuwapima joto la mwili .
Aidha kwa
wataalamu wa afya ambao wanawahudumia wagonjwa wanaohisiwa kuwa na ugonjwa wa
Corona wanavaa vifaa kinga na kufuata
mwongozo wa kuzuia maambukizi wa mwaka 2018 na wa uzuaiaji wa maambukizi ya
Virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Corona (COVID-19) wa mwezi wa kwanza mwaka 2020 wakati
wanawahudumia wagonjwa hao.
Prof. Janabi
alisema, “Wagonjwa wanaofika kutibiwa katika Taasisi yetu wanapimwa joto la mwili kabla ya
kuanza kupata huduma ya matibabu pia tumefunga mabomba ya maji pamoja na kuweka
vitakasa mikono katika maeneo mbalimbali ya Taasisi yetu hii inawafanya kupata
nafasi ya kunawa mikono mara kwa mara”,.
“Tunatoa
elimu ya ugonjwa huu kwa wagonjwa na ndugu wa wagonjwa kupitia vipindi mbalimbali vinavyorushwa
katika Televisheni zilizopo katika Taasisi yetu pia wataalamu wetu wanatoa
elimu kila siku kabla ya kuanza kwa kliniki
zetu’’
Prof.Janabi
aliongeza kuwa Taasisi hiyo imetenga wodi maalum kwa wagonjwa wanaohisiwa kuwa
na dalili za ugonjwa wa Corona ambao baada ya majibu ya vipimo kutoka na
kubainika kuwa na ugonjwa huo wanapelekwa katika kituo cha Amana na kuendelea kupewa huduma za matibabu ya moyo wakiwa huko.
Kwa upande
wake mratibu wa mafunzo hayo ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha utafiti na mafunzo Dkt. Naiz Majani alisema kuwepo kwa mafunzo
hayo kumesaidia kwa kiasi kikubwa kuwaondoa hofu wafanyakazi wa Taasisi hiyo
kuhusu ugonjwa wa Corona.
Dkt. Naiz
ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto alisema mafunzo
hayo yanatolewa katika vikundi vichache vya wafanyakazi kutokana na kada zao
hali ambayo inawasaidia kuelewa zaidi.
“Katika
Taasisi yetu tuna wafanyakazi wa kada ya afya na ambao siyo wa kada ya afya,
hata mafunzo tunayoyatoa tumewagawa
kutokana na kada zao na lugha
tunayotumia kufundishia ni tofauti hii yote tunataka wauelewe kwa undani zaidi
ugonjwa huu na jinsi ya kujikinga wao na kuwakinga wengine wanaowazunguka”,
alisema Dkt.Naiz.
Daktari huyo
bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto aliwaomba washiriki wa mafunzo hayo kutoa
elimu waliyoipata kwa watu wengine ili wajikinge na ugonjwa huo. Pia wafuate
maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya ambayo ni kuvaa barakoa, kunawa
mikono mara kwa mara kwa maji safi yanayotiririka na sabuni , kuepuka
mikusanyiko isiyo ya lazima na kukaa umbali wa zaidi ya mita moja kati ya mtu
na mtu.
No comments:
Post a Comment